Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-14 20:18:54    
China yawasaidia wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi wa vyuo vikuu kumaliza masomo

cri
    Baada ya kuingia mwezi Septemba, wanafunzi wapya wa vyuo vikuu wanaanza kuripoti kwenye vyuo vikuu vilivyowaandikisha. Mwaka huu nchini China kuna wanafunzi wapya wa vyuo vikuu zaidi ya milioni 4. Serikali ya China na vyuo vikuu vinachukua hatua bora kuwasaidia wanafunzi waliotoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi kumaliza masomo yao.

    Hivi sasa elimu ya vyuo vikuu siyo ya lazima nchini China. Kila mwaka mwanafunzi anatakiwa kulipa karo kiasi cha Yuan elfu 6 pamoja na malipo mengine kama ya bweni na chakula, malipo ya jumla kwa mwaka yanaweza kufikia Yuan elfu 10. Kiasi hicho cha fedha si kitu sana kwa familia zenye pato zuri, lakini kwa familia zenye matatizo ya kiuchumi, hususan baadhi ya wanafunzi kutoka sehemu ya vijijini zinashindwa kukimudu.

    Msichana Liu Yu kutoka kijiji kimoja cha mkoani Anhui, mwaka huu alifaulu mtihani wa kuingia chuo kikuu cha mawasiliano cha Beijing. Baada ya kupata barua ya kumfahamisha kuwa ameandikishwa kujiunga na chuo kikuu hicho, alikuwa na furaha kubwa huku akiwa na wasiwasi kuwa hali ya kiuchumi ya familia yake siyo nzuri, tena katika familia yake kuna watoto wanne wanaosoma, hivyo si rahisi kwa familia yake kutoa kiasi hicho cha fedha za kumsomesha.

    Wakati alipopta barua ya chuo kikuu, msichana Liu Yu aliambiwa kuwa tatizo la karo ya chuo kikuu linaweza kutatuliwa kwa mkopo wa fedha unaotolewa na serikali. Alisema, "Niliporipoti katika chuo kikuu nilimwambia mwalimu kuwa nimeshindwa kumudu karo hiyo ya chuo kikuu, chuo kiliniambia nipite "njia ya kijani", nijiandikishe kwanza, kisha niende kuomba mkopo wa serikali ili kutatua tatizo la kulipa karo ya chuo kikuu."

    "Njia ya kijani" aliyosema Liu Yu ni njia ya iliyowekwa na vyuo vikuu ya kujiandikisha kwa wanafunzi wenye shida ya kiuchumi, wanafunzi kutoka familia zenye shida ya kiuchumi wanaweza kujiandikisha na kuanza masomo na kulala bwenini bila kulipa karo na malipo ya bweni.

    Hivyo msichana Liu Yu akaanza kutoa ombi kuhusu mkopo wa fedha kutoka serikalini ambao ni Yuan 6,000 kila mwaka. Kiasi hicho cha fedha kinaweza kumlipia karo ya chuo kikuu, wanafunzi wenye shida ya kiuchumi kama Liu Yu pia wanaweza kuomba kazi za chuoni za kusaidia masomo zikiwa ni pamoja na kufanya kibarua kantini, maktaba na supamaketi za chuoni, wataweza kulipia gharama ya chakula na bweni kwa malipo wanayopata katika kazi za vibarua.

    Aidha, serikali inatoa msaada wa Yuan 150 kwa mwezi kwa maisha ya wanafunzi wenye shida ya kiuchumi. Mbali na hayo, njia nzuri kwa wanafunzi hao ni kupata matokeo mazuri katika masomo yao ili kupata tuzo mbalimbali za masomo zinazotolewa na chuo na serikali.

    Takwimu zinaonesha kuwa, hivi sasa vyuo vikuu vya China vina wanafunzi milioni 13.5, wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi ni kiasi cha milioni 2 na laki 6 ikiwa ni 19%. Ili kuwasaidia wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi kumaliza masomo yao, serikali na vyuo vikuu vinawasaidia wanafunzi hao kwa kutoa mikopo ya masomo, tuzo ya masomo ya taifa, ajira za vibarua, kuwapunguzia ada za vyuo vikuu na kutoa msaada wa fedha.

    Tokea mwaka jana, idara husika za China zilibadilisha tuzo za taifa za kuwazawadia wanafunzi wenye mafanikio katika masomo, kuwa tuzo za masomo za kuwasaidia wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi, ambazo zimeongezeka na kufikia Yuan bilioni 1 kutoka Yuan milioni 200 hapo zamani.

    Ili kuhakikisha kutekelezwa vizuri sera za kuwasaidia wanafunzi wenye shida ya kiuchumi, wizara ya elimu ya China imeimarisha usimamizi. Ofisa wa wizara ya elimu ya China Bw. Cui alisema, "Wizara ya elimu iliziarifu idara husika na vyuo vikuu mwezi Julai kuwa, kabla ya kipindi kipya cha masomo kuanza, vinatakiwa kutekeleza vizuri sera za serikali za kutoa msaada kwa wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi."

Idhaa ya Kiswahili