Tukio la mfululizo wa mashambulizi kumi ya kujiua lilitokea tarehe 14 mjini Baghdad, Iraq na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 152 na wengine 542 kujeruhiwa. Kundi la Jihad la Al-Qaeda linaloongozwa na Abu Al-Zarqawi, kiongozi nambari tatu wa kundi la Al-Qaeda alitangaza kuwajibika na tukio hilo.
Ofisa wa wizara ya mambo ya ndani ya Iraq alieleza kuwa, tarehe 14 asubuhi mashambulizi ya kujiua kwa mabomu yalifanyika huku na huko mjini Baghdad na mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu wengi kabisa yalifanyika katika mtaa wa Kazimiyah wa makazi ya Waislam wa madhehebu ya Shiya. Wakati huo, washambulizi walisimamisha basi ndogo iliyowekwa kiasi kikubwa cha baruti katika uwanja ulioko kwenye mtaa wa Kazimiyah, na kuwavutia vibarua waliotafuta kazi na kulipua baruti yenye uzito wa kilo 220. Hadi hivi sasa, watu 114 wamekufa katika milipuko hiyo na wengine 156 kujeruhiwa. Polisi wa Iraq walitangaza kuwa mfululizo wa milipuko hiyo ilipangwa kwa makini.
Kundi la Jihad la Al-Qaeda siku hiyo lilitoa taarifa likieleza kuwa, lengo la mashambulizi hayo ni kulipiza kisasi kwa mashambulizi yaliyofanywa mapema wiki hii na jeshi la muungano la Marekani na Iraq katika kuwasaka watu wenye silaha wa nchi za nje mjini Tal Afar, kaskazini ya Iraq. Kundi hilo lilisema kuwa linapanga kufanya mashambulizi mengine ya kujiua kwa mabomu katika sehemu mbalimbali nchini Iraq.
Wachambuzi wanaona kuwa mashambulizi hayo huenda yalifanywa na kundi la Al-Qaeda na matawi yake kwa kujibu mashambulizi ya jeshi la muungano la Marekani na Iraq. Tangu tarehe 10, mwezi huu, jeshi hilo liliwasaka watu wenye silaha na kuwaua 150 na kuwakamata wengine zaidi ya 400. Usakaji huo bado unaendelea. Kundi moja lililo chini ya kundi la Al-Qaeda lilitishia kuwa kama jeshi la muungano halitasimamisha mashambulizi yake mjini Tal Afar, kundi hilo litashambulia jeshi hilo na waziri mkuu wa serikali ya mpito kwa silaha za kikemikali.
Zaidi ya hayo, hivi karibuni matukio ya kushambuliana kati ya madhehebu ya Shiya na Suni yalitokea mara kwa mara kutokana na uhusiano kati yao kuwa mbaya. Watu wenye silaha tarehe 14 walichukua Waislam wa Shiya kama shabaha kwa madhumuni ya kuzidisha kutokuelewana kati ya madhehebu hayo mawili na kuzuia mchakato wa ukarabati wa kisiasa wa Iraq.
Wachambuzi wameainisha kuwa mashambulizi ya kujiua yaliyotokea tarehe 14 yametoa tahadhari tena kwa jeshi la Marekani lililoko nchini Iraq na serikali ya Iraq kuwa, mazingira ya usalama yanayohitajiwa katika upigaji kura za maoni ya raia kuhusu katiba ya taifa hayaridhishi.
Idhaa ya kiswahili 2005-09-15
|