Mkutano usio rasmi wa mawaziri wa ulinzi wa jumuiya ya NATO uliofanyika kwa siku mbili ulifungwa tarehe 14 huko Berlin. Baada ya kufanya majadiliano, mawaziri wa ulinzi wa nchi wanachama 26 wa jumuiya ya NATO waliohudhuria mkutano huo walifikia muswada kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya operesheni ya kulinda amani nchini Afghanistan inayoongozwa na NATO na shughuli za kupambana na ugaidi zinazoongozwa na Marekani. Lakini wachunguzi wameona kuwa, muswada huo umeonesha tofauti mbalimbali kati ya nchi wanachama wa NATO kuhusu suala hilo.
Katibu mkuu wa NATO Bwana Jaap de Hoop Scheffer alisema kuwa, nchi wanachama wa NATO zimeona kwa kauli moja kuwa, kuna haja ya kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi rafiki na Marekani. Akitumai kuwa NATO itafanya uamuzi rasmi kuhusu muswada huo wa maafikiano kwenye mkutano unaotarajia kufanyika mwezi ujao.
Kutokana na muswada huo, nchi wanachama wa NATO zimekubali kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati yao na Marekani kuhusu suala la Afghanistan. Siku za usoni, makamanda wa NATO wataongoza jeshi la Marekani na jeshi la kulinda amani la kimataifa yaliyoko nchini Afghanistan.
Mwishoni mwa mwaka 2003, Marekani iliwahi kutoa pendekezo kama hilo, lakini kwa sababu pendekezo hilo lilitaka jeshi la kimataifa libebe wajibu wa kupambana na magaidi ili kupunguza mzigo wa jeshi la Marekani, hivyo lilipingwa na nchi kadhaa za NATO zikiwemo Ujerumani, Ufaransa na Uturuki zilizokuwa na wasiwasi kuwa, askari wao huenda watakabiliwa na hatari kubwa.
Wachunguzi wameona kuwa, japokuwa pande hizo mbili zimeshaafikiana, lakini bado hazikuweza kuficha tofauti kati yao.
Kwanza, pendekezo lililotolewa na waziri wa ulinzi wa Marekani Bwana Donald Rumsfeld kuhusu kuunganisha majeshi hayo mawili halikukubaliwa.
Pili, ingawa baadhi ya mawaziri wa ulinzi wa nchi wanachama wa NATO wameafikiana na Marekani kuhusu suala hilo, lakini kwa kweli bado zina tofauti. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Bwana Peter Struck alisema kuwa, shughuli hizo mbili nchini Afghanistan zinazoongozwa na NATO na Marekani zinaweza kuendelea kwa pamoja katika nchi moja, lakini alisisitiza kuwa, zitaendelea kuendeshwa kwa mbalimbali katika muda unaotarajiwa. Hii inamaanisha kuwa, hata kama shughuli hizo mbili zikiongozwa na kamanda mmoja, bado hazitaunganishwa.
Waziri wa ulinzi wa Hispania Bwana Jose Bono Martinez alichukulia kuwa, shughuli hizo mbili lazima ziendeshwe kwa tofauti, jambo pekee linaloweza kuziunganisha pamoja ni kuwa, wote wako nchini Afghanistan.
Kwa hivyo ingawa nchi wanachama wa NATO zimekubaliana kuhusu vitendo vyao vya kijeshi nchini Afghanistan, lakini kutokana na tofauti kati yao, bado haijulikani lini Marekani na nchi wanachama wengine wa NATO zitaanza ushirikiano wa kijeshi kati yao, na kama zinaweza kuunganishwa pamoja.
2005-09-15 Idhaa ya Kiswahili
|