Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-15 20:00:41    
Maoni ya vijana wa China kuhusu vita dhidi ya uvamizi wa Japan na uhusiano kati ya China na Japan

cri

Tokea tarehe 7 Julai mwaka 1937 Japan ianzishe vita ya kuivamia China kwa pande zote, hadi tarehe 15 Agosti mwaka 1945 Japan ilipotangaza kusalimu amri bila masharti, watu wa China walipambana vikali na wavamizi wa Japan kwa miaka minane, na kutoa mhanga mkubwa wa kimaisha. Takwimu zinaonesha kuwa, katika kipindi hicho wanajeshi na wananchi wa China zaidi ya milioni 35 walikufa na kujeruhiwa, hasara za mali na gharama za kivita zilifikia dola za kimarekani bilioni 560. Ikiwa sehemu moja muhimu ya vita dhidi ya ufashisti duniani, ikilinganishwa na sehemu nyingine, mapambano yaliyotokea nchini China yalianza mapema zaidi, kuendelea kwa kipindi kirefu zaidi na kuwa ya kikatili zaidi. Ingawa miaka 60 imeshapita, lakini madhara ya vita hiyo bado yanaendelea kuwaathiri vibaya wachina.

Mwanafunzi wa chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Nanjing Bwana Song Jiangnan alipozungumzia vita hiyo aliona kuwa, mapambano dhidi ya wavamizi wa Japan, yalikuwa ni mapambano kati ya nguvu za haki dhidi ya uovu. Akisema:

"Vita hiyo haisahauliki kwa wachina wote, kwani hayo ni mafunzo yaliyopatikana kwa kumwaga damu, na ilikuwa aibu kwa taifa. Japokuwa sijawahi kushuhudia vita mwenyewe, lakini kwa kutazama televisheni na filamu, na kusoma vitabu nimeona kuwa, vita hiyo ilikuwa ni ya kikatili sana. Tukiwa vijana wa zama mpya, tunapaswa kukumbuka historia hiyo."

Suala la historia linahusiana na ufahamu wa vita iliyoleta madhara makubwa kwa watu wa nchi zote mbili za China na Japan, pia linahusiana na hisia ya kitaifa ya watu wa China. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na tovuti ya SOHO, asilimia 66 ya wachina wanaona kuwa, suala kuhusu namna ya kushughulikia historia ni sababu kuu inayoathiri uhusiano kati ya China na Japan. Na uchunguzi mwingine ulionesha kuwa, asilimia 97 ya wachina wanapinga vikali vitendo vya viongozi wa Japan kutoa heshima kwenye hekalu la Yasukumi , ambalo vimewekwa vibao vya mizimu ya wahalifu wa kivita walioshiriki kwenye vita kuu ya pili ya dunia.

Uchunguzi mwingine uliofanywa na gazeti moja la kiingereza nchini China ulionesha kuwa, asilimia 77 ya wachina, wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa vyuo vikuu wanaona kuwa, suala kuhusu namna ya kushughulikia historia ni suala linalopaswa kutatuliwa kwa dharura kati ya China na Japan.

Mwanafunzi kutoka chuo kikuu cha ualimu cha Anyang, mkoani Henan Bwana Han Bingzhao ni mmoja kati ya vijana wengi waliolaani kwenye tovuti vitendo vya waziri mkuu wa Japan Junichiro Koizumi kutoa heshima kwenye hekalu la Yasukumi, na nguvu za mrengo wa kulia kujaribu kupotosha historia. Bw. Han Bingzhao anasema:

"Vitendo vya kupotosha na kukanusha historia ni vitendo vya kujidanganya, ushahidi wa kihistoria hauwezi kufutwa, kama vile mauaji makubwa ya Nanjing, madhara yaliyosababishwa na silaha za sumu yaliyogunduliwa katika mji wa Qiqihar, kaskazini mashariki mwa China, na mkoani Guangdong, kusini mwa China. Hatuwezi kufahamu kwa nini baadhi ya wajapan wanataka kukanusha ukweli wa mambo, tumeghadhabishwa sana."

Hivi sasa vijana wengi wa China wanatoa maoni yao kupitia baraza la kuadhimisha ushindi wa vita dhidi ya wavamizi wa Japan. Tovuti ya data za mauaji makubwa ya Nanjing ni moja ya tovuti zilizoadhimisha miaka 60 tangu China ipate ushindi katika vita dhidi ya uvamizi wa Japan, ambayo imeonesha picha nyingi zinazohusu mauaji makubwa ya Nanjing, makala zilizotolewa na vyombo vya aina mbalimbali nchini China na nchi za nje kuhusu ukweli wa kihistoria, na hukumu ya haki zilizotolewa na mahakama ya kimataifa na ya China dhidi ya uhalifu wa wavamizi wa Japan.

Japan kutoweza kutambua na kushughulikia kwa usahihi suala la historia, kumewafanya vijana wa China kupinga Japan kwa jaribio lake la kujipatia ujumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Mwanafunzi wa shahada ya pili katika chuo kikuu cha ualimu cha Beijing Bi. Wang Ying alisema kuwa, kama Japan inataka kukubaliwa kuwa mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama na kufanya kazi muhimu kubwa zaidi kwenye jukwaa la kimataifa, kwanza kabisa inapaswa kupata uaminifu na uelewano kutoka kwa watu wa nchi za Asia, hasa wa nchi jirani. Akisema:

"Ikiwa ni nchi inayotarajia kuliwakilisha bara la Asia na kutaka kutoa mchango mkubwa zaidi kwenye Umoja wa Mataifa, kama haiwezi kushughulikia vizuri uhusiano kati yake na nchi jirani, hakika uwakilishi wake kwenye Umoja wa Mataifa unatiwa mashaka. Mwaka huu ni mwaka wa kuadhimisha miaka 60 tangu Japan ishindwe vita, ni fursa nzuri kwa nchi hiyo kuzingatia na kushughulikia suala la historia."

Hata hivyo, vijana wengi wa China wanachukua msimamo wenye juhudi kuhusu namna ya kukuza uhusaino na Japan. Uchunguzi umeonesha kuwa, asilimia 51 ya wachina walieleza kuwa, wanapenda kuwasiliana na vijana wa Japan na kuwa na urafiki nao.

Bw. Han Bingzhao alisema kuwa, hivi sasa ni zama ya amani, tunaamini watu wengi kabisa wa Japan pia wanapenda kuwa na urafiki na China. Hivyo tunapaswa kuwatofautisha watu wa kawaida wa Japan na wajapan wachache wenye mrengo wa kulia, kuzidisha maelewano kati ya watu wa nchi hizo mbili, hasa kuwa na matumaini kwa vijana wa nchi hizo mbili

Wachina wengi wanaweza kuyashughulikia vizuri masuala yaliyotokea katika uhusiano kati ya China na Japan. Mchina anayefanya kazi katika tawi la Shanghai la kampuni ya Dragon Ease Bi. Wang Haiying alisema kuwa, baadhi ya masuala ya uhusiano kati ya China na Japan yanaweza kutatuliwa hatua kwa hatua katika mchakato wa maendeleo. Akisema:

"Maingiliano ya kiuchumi kati ya China na Japan yameleta manufaa mengi halisi kwa watu wa nchi hizo mbili, ambayo ni ya kunufaishana, hivyo natumaini kuwa, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Japan utapata maendeleo mazuri, na uhusiano wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili utaweza kuondoa kivuli kilichosababishwa na historia.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-15