Kikao cha pili cha mkutano wa maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa kilifanyika tarehe 15, rais Hu Jintao wa China alishiriki kwenye mkutano huo na kutoa hotuba kuhusu "kufanya jitihada kujenga dunia yenye amani, ustawi na mapatano" na kueleza maoni na msimamo wa China kuhusu hali ya dunia ya hivi sasa pamoja na masuala makubwa ya kimataifa, na kutoa mapendekezo kuhusu kuhimiza maendeleo na ushirikiano duniani.
Kikao cha pili cha mkutano wa wakuu wa nchi kilisimamiwa na rais Goran Persson wa Sweden ambayo ni nchi mwenyekiti wa baraza kuu la 60 la Umoja wa Mataifa pamoja na rais El Hadj Omar Bongo wa Gabon ambayo ni nchi mwenyekiti wa baraza kuu la 59 la Umoja wa Mataifa. Wakuu wa nchi na viongozi wa serikali walioshiriki mkutano huo walijadiliana kuhusu kuendeleza mageuzi ya Umoja wa Mataifa, kulinda amani ya dunia na kuhimiza maendeleo na ushirikiano.
Bw. Hu Jintao alisema kuwa kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa ni jambo muhimu sana katika historia ya binadamu. Katika miaka 60 iliyopita Umoja wa Mataifa ulifanya kazi muhimu na kupata mafanikio makubwa katika kulinda amani ya dunia, kuhimiza maendeleo na ustaarabu wa binadamu. Alitoa mapendekezo ya China akisema,"Umoja wa Mataifa ukiwa kitovu cha mfumo wa usalama wa pamoja, umuhimu wake unapaswa kuimarishwa zaidi na wala siyo kudhoofishwa. Tunatakiwa kuwa na mtazamo mpya wa kuaminiana, kunufaishana, kutendeana kwa usawa na kushirikiana, na kujenga mfumo wenye ufanisi wa usalama wa pamoja na wa haki; Tunatakiwa kuhimiza na kuunga mkono utatuzi wa migogoro na mapambano ya kimataifa kwa njia ya amani; Tunatakiwa kuimarisha ushirikiano na kupambana kithabiti na ugaidi."
Suala la maendeleo linahusiana na maslahi ya watu wa nchi mbalimbali, vilevile linahusiana na kukomesha chanzo cha matishio dhidi ya usalama wa dunia, suala hilo limezingatiwa na jumuiya ya kimataifa katika miaka ya karibuni.
Mwaka 2000, mkutano wa milenia wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Mataifa ulipitisha lengo la maendeleo la milenia linalokusudia kumaliza hali ya umaskini na njaa ambalo limekuwa waraka wa mpango unaoelekeza maendeleo na ushirikiano duniani. Kuhusu suala la maendeleo, Bw. Hu Jintao alisema,"Umoja wa Mataifa unatakiwa kuchukua hatua halisi na kutekeleza lengo la maendeleo la milenia, hususan kuhimiza nchi zinazoendelea kuharakisha maendeleo yake na kufanya karne ya 21 iwe karne halisi ya 'Kila mtu kupata maendeleo'. Tunatakiwa kuhimiza kuanzishwa kwa utaratibu wa biashara wa nchi nyingi unaofungua mlango, wa haki na kutokuwa na ubaguzi, na kuboresha zaidi utaratibu wa mambo ya fedha ya kimataifa; Tunatakiwa kuimarisha mazungumzo na ushirikiano ya kimataifa kuhusu nishati na kuhifadhi usalama wa nishati na utulivu wa soko la nishati; tunatakiwa kufanya jitihada kuhimiza na kulinda haki za binadamu na kufanya kila mtu awe na nafasi na haki ya kufuatilia maendeleo ya pande zote kwa usawa. Aliongeza kuwa nchi zilizoendelea zinatakiwa kubeba majukumu mengi zaidi katika kuleta maendeleo ya uwiano duniani."
Bw. Hu Jintao alisema kuwa, hivi sasa hali ya dunia imekuwa na mabadiliko makubwa. China inaunga mkono Umoja wa Mataifa kufanya mageuzi mwafaka na ya lazima. Alisema kuwa mageuzi hayo yanatakiwa kuhimiza Umoja wa Mataifa uwekeze zaidi katika shughuli za maendeleo. Mageuzi ya baraza la usalama yanatakiwa kufikiria kwanza kuongeza uwakilishi wa nchi zinazoendelea hasa nchi za Afrika, ili kuzipatia nafasi nchi nyingi zaidi hasa nchi za wastani na ndogo za kushiriki kwenye maamuzi ya baraza la usalama.
Idhaa ya Kiswahili
|