Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-19 18:11:57    
Maonesho ya Kimataifa ya Shughuli za Matangazo ya Redio na Televisheni Mjini Beijing

cri

Maonesho ya kimataifa ya shughuli za matangazo ya redio na televisheni yalimalizika siku chache zilizopita mjini Beijing. Hayo ni maonesho kabambe yaliyohusisha maonesho ya michezo ya televisheni, biashara, kongamano na kutoa tuzo kwa filamu bora na vipindi vya televisheni.

Maonesho hayo yalianza kufanyika mwaka 2003. Ni maonesho ambayo licha ya kuonesha maendeleo ya shughuli za matangazo ya redio na televisheni pia ni shughuli ya maingiliano na ushirikiano wa kimataifa, hivi sasa yamekuwa ni soko kubwa la biashara ya matangazo ya redio na televisheni barani Asia.

Ikilinganishwa na maonesho ya miaka miwili iliyopita, maonesho ya mwaka huu ni makubwa zaidi. Eneo la maonesho ni mita za mraba elfu 70, shughuli zilizokuwa katika maonesho hayo ni pamoja na maonesho ya michezo ya filamu na televisheni, vifaa vya matangazo ya redio na televisheni, baraza la watangazaji wa vipindi vya redio na televisheni na sherehe ya kutoa tuzo kwa michezo bora ya televisheni na filamu za China. Vyombo vya habari na mashirika mengi kutoka Marekani, Ufaransa, Japan na Korea ya Kusini karibu elfu moja yalihudhuria maonesho hayo.

Maonesho ya vifaa vya matangazo ya redio na televisheni yalivutia mashirika mengi maarufu kama ya Sony, Panasonic na Thomson. Maonesho ya Kituo Kikuu cha Televisheni cha China, CCTV, yalikuwa na nafasi ya mita za mraba 800, ambayo yalionesha kwa pande zote maendeleo ya teknolojia ya kisasa na uwezo wa kutosha kwa kutangaza duniani michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2008 mjini Beijing.

Maonesho ya kimataifa ya michezo ya televisheni yaliwaletea wataalamu wa michezo hiyo fursa ya maingiliano na ushirikiano. Kwenye baraza la michezo ya katuni, Bw. Yoshikawa aliyetoka Japan alisema, "Soko la michezo ya televisheni ni kubwa nchini China. Sababu ya kuwa baadhi ya mashirika kutoingia nchini China hadi sasa ni kutoelewa hali ilivyo ya soko la China, bado wana wasiwasi kuhusu kutoheshimu hakimiliki, hata hivyo haifai kupoteza soko hilo."

Maonesho hayo yaliwashirikisha wafanyabiashara wengi na michezo mingi ya televisheni. Mwaka jana mashirika ya Korea ya Kusini zaidi ya kumi ya michezo ya katuni yalishiriki kwenye maonesho hayo. Mwaka huu vituo vya televisheni vya Korea ya Kusini, MBC na KBS vilileta michezo mingi. Katika miaka ya karibuni michezo ya televisheni ya nchi hiyo imekuwa inakaribishwa sana na watazamaji wa China. Mkurugenzi wa kitengo cha kimataifa katika Kituo cha Televisheni cha Korea ya Kusini, MBC, Bw. J.B. Park alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, "Mwaka huu tumeleta michezo 50. Michezo yetu inakaribishwa sana na Wachina, ndio kutokana na sababu hiyo inatupasa tuifanye michezo yetu iwe inavutia zaidi."

Mwaka huu ni mwaka wa 60 tokea China ipate ushindi katika vita dhidi ya wavamizi wa Japan, kwa hiyo michezo yenye maudhui hayo ilikuwa mingi. Zaidi ya michezo hiyo, pia kuna michezo ya katuni kwa watoto na vijana. Shirika la "Star Q" la Taiwan lilileta michezo ya katuni inayosimulia hadithi za kale za China. Katika michezo hiyo riwaya za kale za China zinaelezwa kwa hadithi za kuvutia. Msaidizi wa meneja mkuu wa shirika hilo Bw. Shi Hao alisema, "Tuna hamu ya kupata mwenzi wetu wa ushirikiano, michezo hiyo ya katuni tumeyarisha, lakini kutokana na gharama kubwa za kuikamilisha tunahitaji ushirikiano na mashirika kutoka China."

Kwenye maonesho pia kulikuwa na "baraza la kimataifa kuhusu matangazo ya michezo mwaka 2005", viongozi wa vyombo vya habari, nyanja za michezo na mashirika kama ya Coca-Cola, Volkswagen na Adidas walishiriki kwenye baraza hilo kutokana na michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2008 mjini Beijing. Naibu mkuu wa Idara Kuu ya Matangazo ya Redio na Televisheni na Filamu ya China Bw. Tian Jin kwenye baraza hilo alisema, "Michezo ya Olimpiki mwaka 2008 Beijing itakuwa ni Olimpiki ya utamaduni na sayansi ya kisasa. Tunapenda kupokea sayansi ya kisasa na kuyafanya matangazo yetu ya michezo ya Olimpiki kupitia televisheni yawe burudani kwa watu wote na kuwaletea wafanyabaishara duniani fursa kubwa."

Sherehe ya kutoa tuzo kwa ajili ya filamu na michezo bora ya televisheni ilifanyika katika maonesho hayo. Inasemekana kwamba mwaka 2004 sekta ya filamu ilipata mafanikio makubwa, mwaka huu filamu 212 zilitengenezwa na zilipata yuan bilioni 1.6 kwa mauzo ya tikti, hili ni ongezeko la 60% kuliko mwaka uliotangulia.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-19