Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-20 16:00:24    
Mabadiliko mapya yatokea katika sekta ya benki nchini China

cri

Katika muda wa zaidi ya miaka mitatu tangu China ijiunge na Shirika la Biashara Duniani WTO, soko la benki limeharakisha hatua za mageuzi na ufunguaji mlango, benki nyingi za kigeni zimeingia kwenye soko la China kwa njia mbalimbali, hivi sasa shughuli za benki zinapanuka kwa mfululizo.

Wakati huo huo benki za China pia zinajifunga kibwebwe kuukabili ushindani huo na kujiandaa kuingia kwenye soko la kimataifa. Katika kipindi hiki cha nchi yetu mbioni, nitawafahamisha mabadiliko mapya ya sekta ya benki yaliyotokea katika utekelezaji wa sera za kufungua mlango kwa nje na ushindani wa kimataifa.

Hapo zamani shughuli za benki za China zinachukua muda mrefu kutokana na mchakato mrefu. Katika miaka ya karibuni hali hiyo imebadlika sana. Kuhusu hayo, kiongozi wa idara ya mikopo ya kampuni ya ujenzi wa viwanda vya uyeyushaji madini ya China Bw. You Senlin alisema kuwa, yeye anafanya shughuli mara kwa mara katika benki kutokana na kazi anazofanya kuhusu utoaji zabuni, mikopo, ukusanyaji fedha na mikopo. Alisema kuwa hivi sasa aina za shughuli za benki zimeongezeka, mchakato wake umebadilika na ufanisi wa benki umeongezeka. Alisema,

"Hapo awali, kumaliza shughuli moja ya benki kutachukua zaidi ya wiki moja; hivi sasa inanichukua muda wa chini ya siku 3, hayo ni mabadiliko makubwa. Mameneja watendaji wa baadhi ya benki wanatutembelea kutueleza shughuli mpya za benki na kutaka kufahamu mahitaji na maoni ya kampuni kuhusu shughuli za benki."

Bw. You anaona kuwa chanzo cha kutokea kwa mabadiliko hayo, ni kuingia kwa mitaji ya nchi za nje. Takwimu zinaonesha kuwa hivi sasa shughuli za benki za nchi za kigeni zimepanuka hadi kwenye miji 18 ya China, benki hizo za kigeni zinaweza kuendesha shughuli na huduma za aina zaidi ya 100 zikiwemo za Yuan za Renminbi na shughuli za benki kwenye mtandao. Kutokana na kukabiliwa na hali ya kuingia kwa benki nyingi za kigeni, benki za China hazina budi kuinua kiwango cha huduma ili kuvutia wateja.

Naibu kiongozi wa idara ya mambo ya fedha ya chuo kikuu cha wananchi cha China profesa Zhao Xijun alisema kuwa, benki za kigeni zimeleta mtindo wa kazi na utaratibu wa usimamizi wao nchini China baada ya benki hizo kuingia nchini, soko la mambo ya fedha nchini limeboreshwa na kuwa la pande nyingi, ambapo wateja wanapata huduma nyingi nzuri. Alisema,

"Kuingia kwa benki za nchi za kigeni kumehimiza uboreshaji wa usimamizi wa benki za China na kukuza uwezo wa ushindani. Licha ya kuleta manufaa kwa wateja wa China, pia kunafanya soko la mambo ya fedha ya China liwe la pande nyingi; kwa upande mwingine inaleta ushindani kati ya benki za China na kuongeza ufanisi wa kazi za benki. Nadhani hili ni jambo muhimu linaloendana na utandawazi wa uchumi na soko la mambo ya fedha duniani."

Bw. Zhao Xijun alisema kuwa kutokana na ahadi ilizotoa China wakati ilipojiunga na WTO, ufunguaji mlango wa sekta ya benki una kipindi cha mpito chenye miaka 5. Utekelezaji wa sera za ufunguaji mlango unaanza kwenye sehemu ya pwani hadi miji mikubwa ya sehemu ya ndani na hatimaye katika miji yote ya wastani ya sehemu ya ndani; katika shughuli zake, kwanza ni kuhusu fedha za kigeni, kisha ni fedha za kichina na zitakuwa wazi kabisa mwishoni mwa mwaka 2006. Anaona kuwa ufunguaji mlango wa sekta ya benki ya China kwa nje unavutia benki za kigeni na kuleta ushindani mkubwa ambao unahimiza mageuzi ya utaratibu wa umilikaji wa hisa wa benki za China.

Hatua moja muhimu ya mageuzi ya utaratibu wa umilikaji wa benki za biashara za China ni kuuza hisa zake katika masoko ya nchi za nje, hivi sasa benki nyingi zinafanya jitihada kutimiza lengo hilo. Mwaka huu Benki ya Mawasiliano ya China imeanza kuuza hisa zake huko Hong Kong. Benki ya China na Benki ya Ujenzi ya China hivi sasa ziko katika pilikapilika za maandalizi. Jambo moja lililo sawa katika mchakato wa kuuza hisa zake katika masoko ya duniani, ni kupata mwenzi wa ushirikiano wa kimkakati katika nchi za nje.

Mwezi Juni mwaka huu, Benki ya Amerika ilinunua 9% ya hisa za Benki ya Ujenzi ya China kwa dola za kimarekani bilioni 2.5, huo ni mtaji mkubwa kabisa kupatikana kwa benki za biashara za China kutoka nchi za nje. Mkurugenzi mkuu wa Benki ya Amerika Bw. Kenneth D. Lewis alisema kuwa, kuwa mwenzi wa ushirikiano na Benki ya Ujenzi kutaleta faida kwa Benki ya Amerika. Alisema,

"Kwanza, Benki ya Amerika ina wateja wengi nchini China, Benki ya Ujenzi nayo ina wateja wengi ambao wataingia katika nchi za nje. Ushirikiano wa pande hizo mbili kuhusu wateja utakuwa na mustakabali mzuri. Pili, katika siku za baadaye pande hizo mbili zitachunguza kama zinaweza kuwa na ushirikiano katika maeneo gani, huenda kutakuwa na uwezakano wa kuanzisha kampuni moja ya ubia. Tatu, uwekezaji huo ni mkubwa. Tutajitahidi kusaidia Benki ya Ujenzi, hii pia ni njia nzuri ya kujipatia faida kwa Benki ya Amerika."

Mkurugenzi mkuu wa Benki ya Ujenzi ya China Bw. Guo Shuqing alisema kuwa, ushirikiano kati ya Benki ya Ujenzi na Benki ya Amerika siyo kuhusu kuvitia mitaji ya kigeni peke yake, lengo lake kubwa ni kuingiza shughuli, uzoefu na usimamizi mzuri zaidi kutoka nje.

Hali halisi ni kuwa katika sekta ya benki ya China, siyo benki za biashara za taifa peke yake zinazojitahidi kuvutia uwekezaji wa kigeni, bali benki za serikali na za binafsi za miji ya wastani zinajitahidi kuvutia mitaji ya kigeni. Benki ya biashara ya mji wa Nanchong ya mkoa wa Sichuan ulioko sehemu ya kusini magharibi ya China, ni benki ya kwanza ya biashara ya mji wa wastani nchini inayoingiza uwekezaji wa nchi ya kigeni. Mwezi Julai mwaka huu, benki hiyo ilisaini mkataba wa umilikaji wa hisa na ushirikiano wa kiteknolojia na benki mbili kubwa za Ujerumani. Mafanikio ya Benki ya Biashara ya Nanchong yamedhihirisha kuwa ufunguaji mlango kwa nje wa sekta ya benki umepanuka na kufikia sehemu ya magharibi ya China.

Kuhusu mabadiliko yanayoletwa na ufunguaji mlango wa sekta ya benki ya China profesa Zhao Xijun alisema kuwa, mabadiliko mengi hivi sasa yanatokea nchini, mwelekeo wa ufunguaji mlango katika hatua ijayo ni benki za China kwenda katika nchi za nje ambazo zitaathiri masoko ya kimataifa. Alisema, "Ufunguaji mlango wa sekta ya benki kwa nje umevutia benki za nchi za nje kuingia nchini na kupanua shughuli zake, kuvutia benki za kigeni kufanya ubia na benki za China, hiyo ni athari kubwa zaidi iliyotokea nchini China kutokana na uvutiaji mitaji ya kigeni, hiki ni kipindi cha kwanza. Lakini siyo kuweko kipindi cha kwanza tu, katika kipindi cha pili ni kuhusu jinsi benki za China zinavyopanua shughuli zake katika nchi za nje, na kubadilika kuwa benki zinazofanya shughuli zake katika mazingira ya ufunguaji mlango na katika mazingira ya kimataifa."

Idhaa ya kiswahili 2005-09-20