Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-20 18:48:11    
Serikali ya China yafanya juhudi za kusukuma mbele mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China bara na Taiwan

cri

       Katika kipindi kilichopita tuliwaletea makala ya pili ya shindano la chemsha bongo kuhusu ujuzi wa "Taiwan-kisiwa cha hazina cha China" ambapo tuliwafahamisha Sera ya kimsingi na juhudi za serikali ya China ya kutatua suala la Taiwan. Leo tunawaletea makala ya tatu kuhusu juhudi za Serikali ya China katika kusukuma mbele mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China bara na Taiwan, ili kuwanufaisha wananchi wa pande hizo mbili.

Tokea mwaka 1949 hali ya kutenganishwa kwa pande mbili China bara na Taiwan ianze, ndipo mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili yalipokomeshwa. Mwaka 1979, upande wa China bara ulitangulia kutoa pendekezo la kufanya mawasiliano ya moja kwa moja ya biashara, posta na usafiri kati ya China bara na Taiwan. Baadaye hali ya wasiwasi ya kisiasa iliyopungua kati ya pande hizo mbili iliweka mazingira na hali mwafaka kwa ufufuzi na maendeleo ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili.

Mwaka 1987, upande wa Taiwan ulianza kuwaruhusu wakazi wa Taiwan kuja China bara kuwatembelea jamaa zao, baadaye wafanyabiashara wengi wa Taiwan pia walianza kuja China bara kufanya ukaguzi wa hali ya biashara kwenye soko. Wakati huo, kwa kuwa matumizi ya nguvukazi kisiwani Taiwan yaliongezeka siku hadi siku, shughuli zile zilizohitaji nguvu kazi nyingi kisiwani humo zilihitaji kwa dharura mazingira yanayoweza kuzisaidia kupunguza matumizi ili ziendelezwe zaidi, ambapo China bara ilikuwa iko katika hali ambayo ilikuwa na kiu ya maendeleo ya uchumi, lakini serikali na raia walikuwa hawana mitaji ya kutosha, hivyo China bara ilikuwa sehemu mpya ya uwekezaji kwa mashirika ya Taiwan, ambapo hisia za kindugu kati ya wananchi wa China bara na Taiwan zilikuwa nguvu kubwa ya kusukuma mbele maendeleo ya haraka ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili. Mfanyabiashara wa Taiwan Bwana Lin Yanhong ndiye aliyeanza kufanya ukaguzi wa kibiashara China bara wakati huo na kuanzisha biashara yake na China bara. Bwana Lin akikumbusha hali hiyo alisema:

Niliingia China bara mara ya kwanza mwaka 1989, nilifanya biashara ya chuma na chuma cha pua, biashara yangu ilifanyika vizuri, nilipata uagizaji kutoka Taiwan, nilitengeneza bidhaa China bara, halafu nilizisafirisha hadi Marekani.

Ili kuhimiza maingiliano ya kiuchumi na kiteknolojia kati ya China bara na Taiwan, upande wa China bara ulitoa sheria na hatua kadha wa kadha kama vile "Kanuni za kuhifadhi uwekezaji wa wafanyabiashara wa Taiwan". Kwa kutiwa moyo na sera na hatua hizo, na chini ya mvuto wa nguvu za uhai zilizoonekana katika maendeleo ya uchumi wa China bara, wafanyabiashara wengi wa Taiwan walianzisha ushirikiano kiuchumi na kibiashara wa aina mbalimbali, ambapo wafanyabiashara wengi waliongeza uwekezaji wao na kuongeza shughuli zao katika China bara. Kwa mfano mfanyabiashara Bwana Lin Yanhong tuliyemtaja hapo kabla, mbali na biashara ya chuma na chuma cha pua, Bwana Lin pia alinunua nafaka za China bara kama vile mtama, choroko na kunde nyekundu mekundu, halafu aliziuza kisiwani Taiwan na nchi ya Vietnam.

Katika miaka ya hivi karibuni, mabadiliko yametokea katika uwekezaji wa mashirika ya Taiwan katika China bara. Zamani wafanyabiashara wa Taiwan walipendelea zaidi kuwekeza vitega uchumi katika mkoa wa Fujian, kusini mashariki ya China na mkoa wa Guangdong, kusini mwa China, kwani mikoa hiyo iko karibu na Taiwan. Kutokana na maendeleo ya haraka ya uchumi wa China bara, ili kuimarisha uwezo wa ushindani kwenye soko la China bara, mashirika mengi ya Taiwan yameingia sehemu ya magharibi ya kati ya China bara hatua kwa hatua, na pia wameanza kuwekeza kwenye shughuli zinazohitaji teknolojia nyingi badala ya shughuli zinazohitahi nguvu kazi nyingi, na mashirika kadha wa kadha makubwa ya Taiwan pia yameharakisha hatua zao za kuwekeza China bara. Mtafiti wa idara ya utafiti wa Taiwan katika Taasisi ya sayansi ya jamii ya China Bwana Zhang Guanhua alipofahamisha hali hiyo alisema:

Baada ya kipindi cha katikati ya miaka ya 90 ya karne iliyopita, mashirika ya mitambo, mafuta na kemikali ya Taiwan yalianza kuwekeza China bara, hata mashirika ya teknolojia za hali ya juu kama vile Vioo vya kompyuta pia yalianza kuwekeza vitega uchumi vingi China bara, ambapo shughuli za mashirika hayo zilichukua hadhi ya shughuli za jadi za China bara, na zimekuwa nguvu kubwa ya uwekezaji wa Taiwan katika China bara.

Alipochambua sababu hiyo, Bwana Zhang Guanhua aliainisha kuwa, mashirika kadhaa ya Taiwan yaliendelea mapema kuliko yale ya China bara, lakini China bara ina nguvu zaidi katika soko na raslimali kuliko Taiwan, pande hizo zinaweza kusaidiana katika miundo ya kiuchumi, na kuziwezesha pande mbili zipate maendeleo kwa pamoja.

Kuhusu hali ya jumla ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China bara na Taiwan katika zaidi ya miaka 10 iliyopita, mkurugenzi wa Idara ya uchumi katika ofisi ya mambo ya Taiwan ya Baraza la serikali la China Bwana He Shizhong alifahamisha kwenye mkutano na waandishi wa habari akisema:

Ilipofika mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, thamani ya jumla ya biashara isiyo ya moja kwa moja kati ya China bara na Taiwan ilifikia zaidi ya dola za kimarekani bilioni 430, thamani ya uagizaji bidhaa wa China bara kutoka Taiwan ilifikia zaidi ya dola za kimarekani bilioni 360. Hivi sasa China bara imekuwa soko la kwanza kwa Taiwan la kuuza bidhaa nje na pia imekuwa sehemu kubwa ya chanzo cha urali wa biashara kwa Taiwan.

Ingawa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara umekuwa mkubwa kati ya China bara na Taiwan, lakini kama alivyosema Bwana He, biashara ya hivi sasa kati ya pande hizo mbili bado ni biashara isiyo ya moja kwa moja. Sababu ya kuzifanya China bara na Taiwan kutoweza kufanya biashara ya moja kwa moja mpaka sasa ni kwamba, utawala wa Taiwan siku zote hautaki kuitikia mwito wa China bara na wakazi wengi wa Taiwan kuhusu kutimiza lengo la kufanya mawasiliano ya moja kwa moja ya biashara, posta na usafiri kati ya pande hizo mbili, na unafanya chini juu kuzuia mawasiliano ya moja kwa moja ya biashara, posta na usafiri. Wafanyabiashara wa Taiwan wanalalamikia zaidi vitendo hivyo vya utawala wa Taiwan. Mwanakampuni wa Taiwan Bwana Chen Guoyuan ambaye amefanya biashara kati ya China bara na Taiwan kwa miaka mingi alisema:

Kama mawasiliano ya moja kwa moja ya biashara, posta na usafiri, yatafanyika kati ya China bara na Taiwan yakiruhusiwa, yatasaidia kupunguza nguvu kazi nyingi na raslimali nyingi kwa biashara kati ya pande hizo mbili, hata yataongeza usalama wa biashara hiyo, na hayawezi kuleta madhara hata kidogo. Mawasiliano hayo ya moja kwa moja yataweza kuongeza zaidi mawasiliano kati ya watu wa pande hizo mbili, ambayo hayahusiani tu na maslahi ya wafanyabiashara wa Taiwan katika China bara, bali yanalingana maslahi ya watu wa pande hizo mbili.

Bwana Chen ameutaka utawala wa Taiwan uweze kufuata mawimbi ya zama na kuheshimu nia ya watu, isiahirishe mawasiliano hayo kwa kisingizio cha kisiasa, kufuta haraka iwezekanavyo sera ya biashara ya kibaguzi dhidi ya China bara, kufuta vizuizi visivyo vya halali juu ya wafanyabiashara wanaowekeza China bara, na kuchukua hatua halisi za kusukuma mbele maendeleo ya maingiliano na ushirikiano kati ya China bara na Taiwan katika sekta za uchumi na biashara.

Hali tofauti kabisa ni kuwa, upande wa China bara siku zote unafanya juhudi za kutafuta na kuhimiza maingiliano na ushirikiano kati ya China bara na Taiwan, na kutafuta njia za kuleta maslahi kwa wananchi wa pande hizo mbili hasa wakazi wa Taiwan. Tuliwafahamisha kwenye makala ya kwanza ya shindano la chemsha bongo juu ya ujuzi wa "Taiwan?kisiwa cha hazina cha China", kwamba Taiwan inazalisha mazao mengi ya kilimo kama vile mpunga na matunda ya aina mbalimbali. Katika miaka ya hivi karibuni, mazao ya kilimo hasa matunda yalikutana na tatizo la soko huko Taiwan. Ili kuwasaidia wakulima wa Taiwan waondoe taabu hiyo, hivi karibuni China bara imechukua hatua kadha wa kadha kuhimiza uuzaji wa mazao ya kilimo katika China bara. Takwimu zinaonesha kuwa, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, matunda ya Taiwan yaliyouzwa katika China bara yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 kuliko mwaka jana wakati kama huu. Tarehe 1 Agosti, China bara ilianza kutekeleza hatua mpya ya kusamehe ushuru wa forodha kwa aina 15 za matunda ya Taiwan yanayoruhusiwa kuingia kwenye soko la China bara, wahusika wamekadiria kuwa, uuzaji wa matunda ya Taiwan katika China bara utaongezeka zaidi katika siku zijazo.

Wasikilizaji wapendwa hadi hapo ndio tumemaliza kuwasomea makala ya tatu ya chemsha bongo kuhusu serikali ya China kufanya juhudi za kuhimiza mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China bara na Taiwan, ili kuleta manufaa kwa wananchi wa pande hizo mbili.

Sasa tunatoa maswali mawili ili mjibu:

1. Hivi sasa lipi ni soko kubwa la kwanza na chanzo kikuu cha kuleta urali wa biashara kwa biashara ya nje ya Taiwan?

2. Kati ya China bara na Taiwan, ni upande gani unaotaka kuwe na mawasiliano ya moja kwa moja ya biashara, posta na usafiri? Na ni Kwanini lengo hilo mpaka sasa halijaweza kutimizwa?

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-20