Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-21 21:13:58    
Bw. Sharon azongwa na kashfa ya kupokea fedha kwa matumizi ya kisiasa

cri

Vyombo vya habari vya Israel katika siku za karibuni viliripoti kuwa, waziri mkuu wa Israel Bw. Ariel Sharon anatuhumiwa kujikusanyia fedha kwa ajili ya shughuli zake za kisiasa alipokuwa anahudhuria kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa. Tuhuma hizo zinamsumbua Bw. Sharon, ambaye sasa anajitahidi kulinda nafasi yake ya uwenyekiti wa chama cha Likud.

Bw. Sharon alifika New York tarehe 14 mwezi huu kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa. Kwenye mkutano huo, viongozi mbalimbali pamoja na rais Bush walimpongeza Bw. Sharon kwa kutekeleza mpango wa upande mmoja kwa mafanikio. Mbali na wakuu wa nchi na viongozi wa serikali, Bw. Sharon pia alikutana na viongozi wa jumuiya za wayahudi na wayahudi maarufu nchini Marekani. Vyombo vya habari vya Israel vyote vinasema kuwa ziara hiyo ya Bw. Sharon ni yenye mafaniko, kwani imeinua heshima na hadhi ya Israel kwenye jumuiya ya kimataifa.

Bw. Sharon alimaliza ziara yake kwenye Umoja wa Mataifa tarehe 19 na kurudi nyumbani. Lakini nyumbani hakupokelewa kwa maua na makofi, bali alipokelewa kwa ripoti kuhusu yeye kujikusanyia fedha kwa ajili ya shughuli zake za kisiasa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tarehe 18 Bw. Sharon pamoja na wanandoa 15 wayahudi ambao ni matajiri kabisa nchini Marekani walihudhuria tafrija kwenye nyumba moja iliyoko barabara ya 5 ya Manhattan. Mwandaaji wa tafrija hiyo aliwataka kila wanandoa wayahudi wachangia dola za kimarekani elfu 10, na fedha hizo zitahifadhiwa kwenye idara moja isiyo ya kibiashara yenye athari kote nchini Israel?kama fedha za kuendesha kampeni ya uenyekiti wa chama cha Likud.

Ripoti hiyo inaona kuwa, kitendo hicho cha Bw. Sharon kimekwenda kinyume na sheria. Kwa mujibu wa sheria ya vyama ya Israel, kwenye tafrija kama hiyo iliyoandaliwa kwa ajili ya kukusanya fedha kwa shughuli za kisiasa, kila wanandoa hawawezi kuchangia zaidi ya dola za kimarekani 7800. Ripoti iliyotolewa tarehe 10 na televisheni ya Israel inasema kuwa, makao makuu ya idara iliyopokea fedha hizo yako nchini Marekani, kwa mujibu wa sheria husika za Marekani, idara ya namna hiyo, ambayo haitozwi kodi, haina haki ya kupokea fedha kama hizo.

Habari hiyo inafuatiliwa na pande husika. Jumuiya ya Harakati za Kupambana na Ufisadi nchini Israel na baadhi ya wabunge wanamtaka mwendesha mashitaka mkuu wa serikali Bw. Menachem Mazuz amfanyie Bw. Sharon uchunguzi wa makosa ya jinai. Bw. Mazuz tarehe 20 alitangaza kuwa kwanza athibitishe ripoti hiyo ni ya kweli au la, ndipo ataamua kumfanyia Bw. Sharon uchunguzi au la.

Ripoti hizo zimeleta athari mbaya kwa juhudi za Bw. Sharon za kugombea nafasi ya mwenyekiti wa chama cha Likud. Katika miaka ya karibuni, kutokana na mpango wake wa mpango wa upande mmoja, uungaji mkono kwa Bw. Sharon ndani ya chama hicho umepungua kwa kiasi kikubwa. Kama kamati kuu ya chama cha Likud itakubali mapendekezo ya Bw. Benjamin Netanyahu kuhusu kufanya uchaguzi wa mkuu wa chama hicho mwezi Novemba kabla ya wakati uliowekwa, huku akikabiliana na chagamoto iliyoletwa na Bw. Netanyahu na ripoti hiyo yenye athari mbaya, maisha ya kisiasa ya Bw. Sharon yanaweza kubadilika.

Ingawa Bw. Sharon alipokutana na baadhi ya wajumbe wa kamati kuu ya chama cha Likud tarehe 20 alisema kithabiti kuwa ameamua kugombea na kushinda nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho, kwenye uchaguzi na kukiongoza chama hicho kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho, lakini ripoti hiyo imemletea athari mbaya, tutafuatilia kama yeye anaweza kujiepusha na athari hiyo na kuendelea na nafasi yake.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-21