Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-21 21:19:07    
Umoja wa Ulaya wataka kuwasilisha suala la nyuklia la Iran kwenye baraza la usalama

cri

Umoja wa Ulaya tarehe 20 ulisambaza rasimu ya azimio kuhusu Iran kwa wanachama wa bodi ya wakurugenzi ya shirika la nishati ya atomiki duniani, na kutaka ripoti kuhusu suala la nyuklia la Iran iwasilishwe kwenye baraza la usalama na baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Lakini rasimu hiyo haikutaja suala la kulitaka baraza la usalama liiwekee vikwazo Iran.

Rasimu hiyo inasema kuwa kutokana na Iran kutotekeleza wajibu uliowekwa kwenye mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia, Umoja wa Ulaya unataka kutoa ripoti kuhusu suala la nyuklia la Iran kwa wanachama wote wa shirika la nishati ya atomiki duniani, pamoja na baraza la usalama na baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Rasimu hiyo pia inalitaka baraza la usalama liihimize Iran kuruhusu shirika hilo lifanye ukaguzi kwenye sehemu zinazopigwa marufuku na sheria husika ya Iran kwa ukaguzi, na kuihimiza tena Iran isimamishe kabisa shughuli za kubadilisha uranium.

Umoja wa Ulaya na Marekani zote zimechukua mpango wa uranium nzito wa Iran kama sehemu ya mpango wa silaha za nyuklia wa nchi hiyo na kuona kuwa iwapo Iran ina uwezo wa kuzalisha yenyewe nishati ya nyuklia, basi yumkini itajitoa katika mkataba wa kutosambaza silaha za nyuklia wakati wowote, kwani ikirekebisha kidogo tu zana na kutumia uranium nzito, itaweza kutengeneza silaha za nyuklia haraka. Umoja wa Ulaya ulieleza kuwa mapendekezo mapya ya umoja huo kuhusu suala la nyuklia la Iran yamepingwa na Iran na umoja huo hauna chaguo lingine, ila tu kufikisha suala hilo kwenye baraza la usalama.

Wachambuzi wanaona kuwa kutokana na dalili mbalimbali, kuliacha baraza la usalama liingilie suala la nyuklia la Iran, sio nia asili ya umoja huo, ambapo unajaribu kuweka shinikizo zaidi kwa Iran ili kuilazimisha irudi kwenye meza ya mazungumzo.

Iran imejibu mara moja kitendo hicho cha Umoja wa Ulaya. Mjumbe wa kwanza wa mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran Bw. Ali Larijani tarehe 20 alieleza kuwa, kama suala hilo litafikishwa kwenye baraza la usalama, Iran itafikiri kujitoa kutoka mkataba wa kutosambaza silaha a nyuklia na nyongeza ya nyaraka za mkataba huo na kuanzisha upya shughuli za uranium nzito. Habari zinasema kuwa upande wa Iran ulieleza kuwa, Iran itaweka vikwazo kwa uuzaji wa mafuta dhidi ya nchi zinazounga mkono mswada huo wa Umoja wa Ulaya.

Hivi sasa, nchi wanachama 35 za shirika la nishati ya atomiki duniani zimefanya mazungumzo kuhusu mswada wa Umoja wa Ulaya. Habari zinasema kuwa Marekani na Japan zimeeleza hadharani kuunga mkono mswada huo, lakini nchi nyingi zinazoendelea pamoja na Russia, China na India zina maoni tofauti kuhusu rasimu hiyo. Kutokana na makadirio, nchi nyingi zitatoa maoni ya kuirekebisha, ili ipitishwe kwa makubaliano ya pamoja, lakini kama Marekani na Umoja wa Ulaya zikikataa kurekebisha sana rasimu hiyo, na kutaka kufanya upigaji kura, basi rasimu hiyo itapasishwa kwa kura 18 za ndiyo. Vyombo vya habari vinaona kuwa yote mawili yanawezekana.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-21