Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-22 20:27:44    
Wachina washerehekea kwa njia mpya sikukuu ya jadi ya mwezi

cri

Tarehe 18 Septemba yaani tarehe 15 Agosti kwa kalenda ya kichina, ni sikukuu ya jadi ya Wachina, yaani sikukuu ya mwezi. Hiyo ni moja ya sikukuu muhimu kwa Wachina. Kutokana na desturi ya jadi ya China, katika siku hiyo watu wa familia hujikusanya pamoja kula keki za mviringo na kuangalia mwezi mpevu. Hivi sasa, licha ya kula keki na kuangalia mwezi mpevu, Wachina wamekuwa na njia nyingi mpya za kusherehekea sikukuu hiyo.

Siku hiyo iko katikati ya majira ya mpukutiko, hivyo inaitwa sikukuu ya katikati ya majira ya mpukutiko. Kila sikukuu hiyo inapofika, watu wa familia za Wachina hujumuika nyumbani wakikaa uani kuangalia mwezi mpevu, huku wakila keki za mviringo zinazoashiria mwezi mpevu, matunda na vitafunwa, na kuungana kwa familia. Katika siku hiyo, Wachina si kama tu wanakula keki nyumbani, bali pia huwazawadia jamaa na marafiki keki zilizofungwa vizuri.

Hivi sasa mtazamo wa Wachina wengi wa kusherehekea sikukuu hiyo umebadilika. Bwana Lao Yibo anayefanya kazi katika shirika la utalii alisema:

"Mwaka huu mimi na familia yangu tutasherehekea sikukuu ya mwezi kwa kutalii nchini Thailand, ili kuburudika na mwezi mpevu ng'ambo. Inasemekana kuwa, huko Thailand watu wanaweza kuangalia mwezi kwa kupanda Tembo."

Bwana Zhou Zhigang anafanya kazi katika idara ya serikali ya mji wa Tianjin, lengo lake kubwa wakati wa kusherehekea sikukuu hiyo ni kuungana na ndugu zake. Akisema:

"Kutokana na kuwa na pilikapilika nyingi za kazi, siku za kawaida sipati nafasi ya kuwapeleka wazazi wangu kutembelea nje. Mwaka huu nitawapeleka wanafamilia wote kusherehekea sikukuu hiyo kwenye ufukwe. Tofauti na mjini, sehemu ya ufukwe ni kimya sana, itakuwa ni burudani kwa familia nzima kukaa ufukweni kuangalia mwezi, kupunga upepo, kula keki na matunda, na kupiga soga."

Vijana wa China wana njia za kisasa za kusherehekea sikukuu hiyo, kama vile kusalimiana kwa kutumiana ujumbe kwa simu za mkononi, kuagiza kadi za maua na kuchagua keki ya mwezi kwenye tovuti na kuwazawadia marafiki. Msichana Liu Menghua aliyehitimu mwaka huu kutoka chuo kikuu anafanya kazi katika shirika lililowekezwa na mfanyabiashara kutoka nje, huko Tianjin. Kutokana na kuwa na kazi nyingi, yeye hakuweza kurudi nyumbani kusherehekea sikukuu hiyo pamoja na wazazi wake, hivyo alichagua njia ya kuwasalimia wazazi, jamaa na marafiki kwa kuwatumia ujumbe. Akisema:

"Tofauti na kupiga simu, ujumbe wa simu ya mkononi unaweza kumfikia wakati wowote anapofungua simu, naweza kueleza hisia zangu zote kwa ujumbe, kweli ujumbe wa simu za mkononi umerahisisha mawasiliano."

Vijana wengi wa China wana mawazo sawa na msichana Liu, wanaona kuwa kutumiana ujumbe kwa simu za mkononi, au kuandikiana barua pepe na kadi kwa njia ya Internet kutakiana heri na baraka, ni njia rahisi na ya kuvutia.

Vijana wengine hata wanawapatia marafiki keki ya mwezi kwa kupitia Internet, wanaopokea keki hizo kwa kugonga panya ya kompyuta tu, basi keki inayopendeza inaonekana kwenye kioo cha kompyuta.

Inasemekana kuwa, katika siku hiyo mwezi unang'aa zaidi kuliko siku nyingine za mwaka mzima. Ili kukidhi matakwa ya wakazi wanaoishi mjini Chendu, ambao hufunikwa na mawingu mazito, shirika moja la safari za ndege la mkoani Sichuan limeanzisha shughuli za kuwapeleka watu kwa ndege, kuruka juu angani kwenda kuuangalia mwezi. Bwana Zuya anayeshughulikia kazi hiyo alisema:

"Ndege za abiria za China huruka angani kwenye urefu wa mita 9000 hadi 10000 kutoka usawa wa bahari, ambako hakuna mawingu yoyote. Huko unaona kama uko karibu sana na mwezi, hivyo ni njia nzuri sana ya kuangalia mwezi."

Shirika hilo pia limeandaa shughuli nyingi, kila ndege iliyotiwa saini mkataba ina maudhui yake, kama vile ndoa ya romantiki, na uhusiano bora kati ya majirani.

Tarehe ya sikukuu ya mwezi ya mwaka huu ni pia ni tarehe ya kutokea kwa tukio la Septemba 18 mwaka 1931, ambapo wavamizi wa Japan walianza kuishambulia sehemu ya kaskazini mashariki ya China. Wanafunzi kadhaa wa chuo kikuu cha Lanzhou cha kaskazini magharibi cha China waliamua kupanda mlima na kuangalia mwezi, ili kuadhimisha siku hiyo na kutosahau aibu ya taifa. Mwanafunzi wa shahada ya pili wa chuo kikuu hicho Bwana Liu Shaochen akisema:

"Sikukuu ya mwezi ya mwaka huu ni maalum sana. Tunapanga kupanda mlima wa Gaolan wenye urefu mkubwa na wenye mazingira mazuri. Tunatarajia kukaa pamoja kubadilishana mawazo ili kuadhimisha tukio la Septemba 18.

Wachina wana mila nyingi za kusherehekea sikukuu ya mwezi kutokana na tofauti kati ya sehemu mbalimbali, lakini desturi zote zina maana moja, yaani kuwa na furaha ya kuungana familia, kufurahia maisha bora na kutathmini amani.

Idhaa ya kiswahili 2005-09-22