Waziri wa mambo ya nje wa Israel Bw. Silavan Shalom tarehe 20 alipohutubia majadiliano ya kawaida ya awamu ya 60 ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa alieleza kuwa, kutekelezwa bila vikwazo kwa mpango wa upande mmoja wa Israel kumeboresha hali ya kidiplomasia ya nchi hiyo, hasa uhusiano kati yake na dunia ya kiarabu na kiislam, na Israel itajitahidi kujipatia "nafasi mwafaka" zaidi katika mambo ya Umoja wa Mataifa. Hotuba hiyo ya Shalom imeonesha kwamba Israel itajitahidi kupanua taathira yake katika mambo ya kidiplomasia kwa fursa ya kutekeleza mpango wa upande mmoja.
Katika hotuba hiyo, Bw Shalom alisema kuwa katika siku kadhaa baada ya kufunguliwa kwa awamu hiyo ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa, alifanya mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kiarabu na kiislam zipatazo zaidi ya kumi, ambapo hali hiyo haikuonekana hapo zamani. Kadiri Israel ilivyoondoka kutoka sehemu ya Gaza, "ukuta wa chuma" uliotenganisha Israel na nchi nyingine za Kiislamu kwa muda mrefu umekuwa ukibomoka. Uhusiano kati ya pande hizo mbili umeendelezwa kwa kasi kubwa. Alieleza matumaini yake kuwa hatimaye nchi hizo zitaanzisha uhusiano kamili wa kibalozi. Bw Shalom alisema pia, hatua nzuri kabisa ya dunia ya kiarabu na kiislam kuwasaidia Wapalestina ni kuanzisha uhusiano wa kibalozi na Israel, ambapo jambo hilo litakuwa sehemu muhimu ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati.
Bw. Shalom alitangaza kuwa Israel itajitahidi kushiriki kwenye mambo mengi ya Umoja wa Mataifa na kutumai kupata nafasi kwenye baraza la usalama siku za usoni. Alisisitiza kuwa Israel ikiwa nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa iliyo na haki kamili inaomba kujiunga na baraza la usalama kwa ajili ya kutafuta nafasi yake inayostahiki kwenye Umoja wa Mataifa. Msemaji wa ujumbe wa Israel unaoshiriki kwenye awamu hiyo ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa alisema kuwa, Israel inatumai kutimiza lengo hilo mapema ya mwaka 2017.
Siku hizi, Israel imeanzisha kampeni kubwa ya kidiplomasia kwa kutumia ufanisi wa kutekeleza mpango wa upande mmoja bila vikwazo na kujaribu kuyeyusha barafu kwenye uhusiano kati yake na dunia ya kiarabu na kiislam na kupata mafanikio.
Wakati huo huo, utekelezaji wa mpango wa upande mmoja pia umeleta nafasi kwa Israel kuboresha uhusiano na Umoja wa Mataifa na kujitia zaidi kwenye jumuiya ya kimataifa. Kwa upande mmoja, Israel ilikuwa katika hali ya kujitenga na Umoja wa Mataifa kutokana na kupingwa na nchi nyingi kwa sera yake ya kuikalia Palestina, kwa upande mwingine, Israel iliulalamikia Umoja wa Mataifa kutotekeleza msimamo wa haki kwa nchi hiyo na ilikataa kutekeleza maazimio kuhusu suala la Palestina na Israel yaliyopitishwa kwenye Umoja wa Mataifa.
Katika miaka ya karibuni, Israel imeona upungufu wake wa mambo ya kidiplomasia ya kuzingatia Marekani tu, na kubadili hatua kwa hatua msimamo wake wa kususia Umoja wa Mataifa na kufuatilia kujiunga na jumuiya ya kimataifa. Serikali ya Sharon pia imetekeleza mpango wa upande mmoja kwa juhudi na kusifiwa na jumuiya ya kimataifa na hali ya Israel imeboreshwa katika Umoja wa Mataifa. Mwezi Juni mwaka huu, mjumbe wa kudumu wa Israel katika Umoja wa Mataifa Bw. Dan Gillerman alichaguliwa kuwa makamu wa mwenyekiti kati ya makamu wenyeviti 21 wa awamu ya 60 ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa, na majadiliano ya kawaida ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa ya tarehe 20 yameendeshwa na Dan Gillerman.
Vyombo vya habari vinaona kuwa ikilinganishwa na Israel, nchi za kiarabu na kiislam zimechukua msimamo wa tahadhari kwenye suala la kuboresha uhusiano kati yao. Dunia ya kiislam inaona kuwa ingawa Israel kuondoka kutoka Gaza ni hatua mwafaka, lakini hatua hiyo bado haijatatua mgogoro kati yao kimsingi. Msimamo wa kikanuni wa dunia ya kiarabu na kiislam kuhusu mgogoro kati ya Palestina na Israel haujabadilika. Kwa hiyo, waziri wa mambo ya nje wa Israel Shalom hana budi kukiri kuwa hakuna uwezekano wa kupata maendeleo makubwa kwenye uhusiano kati ya Israel na dunia ya kiislam hivi karibuni.
Idhaa ya Kiswahili 2005-09-22
|