Maelfu ya Wamarekani wanaopinga vita walifanya maandamano huko Washington na miji mingine wikiendi iliyopita, wakiitaka serikali ya Bush iondoe jeshi haraka iwezekanavyo kutoka Iraq. Mnamo miaka miwili na nusu tangu serikali ya Bush ianzishe vita dhidi ya Iraq, wimbi kubwa la kupinga vita limetokea tena nchini Marekani, jambo ambalo limefuatiliwa sana na vyombo vya habari vya Marekani na vya nchi za nje.
Wachambuzi wanaona kuwa, sababu za kuibuka tena kwa wimbi la kupinga vita nchini Marekani ni zifuatazo:
Kwanza, matumizi ya vita dhidi ya Iraq yameiletea matatizo makubwa serikali ya Bush. Hivi sasa, kuna wanajeshi wa Marekani laki 1.35 nchini Iraq, na wastani wa matumizi kwa mwezi unafikia dola za kimarekani bilioni 5. Tangu vita hivyo vianze, wanajeshi wa Marekani zaidi ya 1900 wameuawa nchini humo, na idadi hiyo bado inaongezeka siku hadi siku.
Pili, serikali ya Bush inazidi kutoaminiwa na wananchi wake kuhusu suala la Iraq. Matokeo mapya ya kura za maoni ya raia yanaonesha kuwa, asilimia 59 wa raia wa Marekani walioulizwa wanaona kuwa, kuzusha vita dhidi ya Iraq peke yake ni kosa, na asilimia 63 wanakubali kuondoa wanajeshi wote au badhi ya wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq.
Tatu, wanasiasa wa Marekani wanazidi kupinga vita. Tunaweza kusema kuwa, kuzusha vita dhidi ya Iraq kwa Marekani kuliungwa mkono kwa viwango tofauti na vyama mbalimbali vya Marekani. Lakini kutokana na malengo ya uchaguzi mkuu wa awamu mpya wa Marekani mwaka 2008, wanachama wa chama cha demokrasia cha Marekani akiwemo rais wa zamani Bill Clinton wameanza kushutumu serikali ya Bush. Bw. Clinton alipohojiwa na waandishi wa habari aliikosoa sera ya serikali ya Bush kuhusu Iraq akisema kuwa, vita dhidi ya Iraq vinaelekeza ufuatiliaji wa Marekani kwenye mapambano dhidi ya ugaidi, na kutumia vibaya huruma na uungaji mkono wa nchi nyingi kwa Marekani. Waziri wa mambo ya nje wa zamani wa Marekani Bi. Madeleine Albright tarehe 24 alionya vikali kuhusu sera ya serikali ya Bush kuhusu Iraq akieleza kuwa, vita hivyo vilivyozushwa na serikali ya Bush vimesababisha mabalaa mbalimbali, havikuipatia Marekani marafiki, badala yake vinadhuru uhusiano kati ya Marekani na nchi za mashariki ya kati na nchi za Kiislam. Bi. Albright alisema kuwa, serikali ya Bush haina chaguo zuri zaidi kuhusu suala la Iraq, na matatizo yatakuwa magumu zaidi mbele yake. Pia alieleza dhahiri kuwa, sera ya upande mmoja wa Marekani inayotekelezwa katika miaka ya karibuni haifanyi kazi, aidha upinzani kutoka chama cha Republican cha Marekani unaongezeka siku hadi siku.
Bila shaka, kuzusha vita dhidi ya Iraq kunakwenda kinyume cha sheria. Marekani ilitumai visingizio viwili kuzusha vita hivyo, yaani Iraq kuwa na silaha kali za maangamizi na utawala wa Saddam wa zamani wa Iraq kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda. Ripoti ya uchunguzi ya serikali za Marekani na Uingereza imeonesha kuwa sababu hizo si za kweli. Serikali ya Bush pia inafahamu kuwa hayo si ya kweli.
Ni kama waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bw. Philippe Douste-Blazy alivyosema, rais Bush wa Marekani anajidai kuibadilisha Iraq kuwa nchi yenye amani na demokrasia, lakini hali tunayoiona ni Iraq yenye migongano ya kimabavu, vifo, na kushindwa kwa muungano wa kitaifa kutokana na usimamizi unaoingiliwa na pande mbalimbali. Kutokana na hali ilivyo hivi sasa nchini Iraq, wimbi la wamarekani la kupinga vita linaloibuka tena linatoa onyo kali kuwa, serikali ya Bush lazima isimamishe mara moja sera ya ukaidi, kwa sababu mabavu hayasaidii kutatua suala la Iraq.
Idhaa ya Kiswahili 2005-09-26
|