Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-27 16:24:57    
Mkutano mkuu wa mafuta wafanyika katika Afrika Kusini

cri

Katika wakati huu ambapo bei ya mafuta imekuwa ikipanda bila kushuka, mkutano mkuu wa 18 wa mafuta ulianza kufanyika tarehe 25 huko Johannesburg, mji ambao unasifiwa kama ni "mji wa dhahabu". Wadau, maofisa waandamizi na wataalamu karibu 4,000 kutoka kila pembe ya dunia wanahudhuria mkutano huo ili kufanya makadirio ya soko la mafuta na hali ya baadaye ya mafuta duniani na kutafuta uwezekano wa maendeleo endelevu ya nishati.

Mkutano huo utafanyika kwa siku tano, na mada za mkutano huo ni pamoja na utafutaji na uchimbaji wa mafuta, usafishaji wa mafuta na mazao mengine yanayotokana kwa mafuta, gesi na nishati inayoweza kutumika tena na usimamizi wa viwanda husika.

Mwenyekiti wa mkutano huo alisema kuwa hivi sasa dunia imeingia katika zama za bei kubwa ya mafuta. Hapo zamani bei ya mafuta kwa kila mapipa kumi ilikuwa ni dola za Kimarekani 20 tu, lakini bei hiyo imekuwa ni historia na haitarudia tena, watu lazima wajirekebishe na kuzoea na hali ya sasa ya bei kubwa. Aliongeza kuwa nishati ya madini inachukua 85% ya nishati yote duniani, ni nishati muhimu kabisa katika mahitaji ya nishati hapa duniani, na mafuta yataendelea kuwa nishati muhimu katika miongo kadhaa ijayo.

Waziri wa madini na nishati wa Afrika Kusini kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, hivi sasa mawaziri wa nishati wa nchi mbalimbali za Afrika wamekuwa wakijadiliana kuunda shirika la kutafuta na kuzalisha mafuta katika Afrika nzima ili kuongeza uwezo wa kushindana na makampuni ya kimataifa na kuongeza uwazi wa ugawaji wa mapato ya mafuta yaliyozalishwa na kila nchi ili kuhakikisha maliasili ya mafuta inanufaisha watu wa nchi za Afrika kwa kiwango kikubwa.

China imepeleka ujumbe wenye watu 121 kuhudhuria mkutano huo unaofanyika katika mji wa Johannesburg na maonesho ya kimataifa ya mafuta na gesi nchini Afrika Kusini ili kufahamu hali ilivyo sasa ya viwanda vya mafuta duniani na kushiriki kwenye maingiliano na ushirikiano wa teknolojia katika nyanja ya mafuta.

Nchi zinazozalisha mafuta na utajiri wa mafuta katika sehemu ya kusini ya Jangwa la Sahara barani Afrika:

Mkutano mkuu wa 18 wa mafuta duniani unafanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini, kuanzia tarehe 25 hadi 29. Huu ni mkutano wa kwanza unaofanyika barani Afrika katika muda wa miaka 72 iliyopita tokea bodi ya wakurugenzi wa mafuta duniani ianzishwe, sababu ya bodi hiyo kuamua mkutano huo ufanyike barani Afrika inatokana na kutambua nafasi muhimu ya nchi za Afrika katika katika soko la mafuta duniani.

Hivi sasa, utajiri wa mafuta unaofahamika uliopo barani Afrika ni mapipa bilioni 80 hadi 100, ambayo ni asilimia 7 hadi 9 ya hzina yote ya mafuta duniani. Katika miaka ya karibuni, kutokana na kutumia teknolojia ya kisasa ya kutafuta mafuta ndani ya bahari, kwenye Ghuba ya Guinea limegunduliwa eneo la mafuta, na utajiri wa mafuta uliothibitishwa unaongezeka miaka hadi miaka na mpaka sasa umekuwa tu nyuma ya Mashariki ya Kati na Amerika ya Kusini. Hadi mwaka 2010, uzalishaji mafuta barani Afrika unatazamiwa kuongezeka hadi asilimia 20 ya uzalishaji wa mafuta duniani. Mwaka 2004, mafuta yaliyozalishwa yalifikia mapipa milioni nane, takriban asilimia 10 ya mafuta yote duniani yaliyozalishwa mwaka huu. Bodi ya wakurugenzi wa mafuta duniani inakadiria kuwa, kadiri nchi mpya zinazozalisha zinavyotokea zaidi uzalishaji wa mafuta barani Afrika utaongezeka kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na takwimu zilizotolewa na wizara ya nishati ya Marekani, nchi muhimu zinazozalisha mafuta katika sehemu ya kusini ya Jangwa la Sahara ni zifuatazo:

Nigeria, mapipa milioni 2.5 kwa siku

Angola, mapipa laki 9.20 kwa siku

Guinea ya Ikweta, mapipa laki 3.5 kwa siku

Gabon, mapipa laki 2.879 kwa siku

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mapipa laki 2.355 kwa siku

Chad, mapipa laki 2 kwa siku

Cameroon, mapipa laki 6.7 kwa siku

Cote d'Ivoire, mapipa 3.3 kwa siku

Idhaa ya kiswahili 2005-09-27