Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-27 21:19:18    
Watu wa China bara na Taiwan wanatarajia kunufaika pamoja na matunda ya siku za usoni

cri

     Wasikilizaji wapendwa, ingawa kuna mlango wa bahari kati ya China bara na Taiwan, lakini pande hizo mbili ni za nchi moja tangu enzi na dahari. Watu wa pande hizo mbili wana asili moja na historia, utamaduni, desturi na mila za pamoja. Hivi sasa kutokana na sababu za kisiasa, ndugu wa pande hizo mbili bado hawajaweza kufanya mawasiliano huria, lakini historia, utamaduni, desturi na mila za pamoja na hisia za kindugu za pande hizo mbili haziwezi kukatizwa. Katika kipindi hiki cha leo tunawaletea makala ya 4 ya shindano la chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Taiwan-kisiwa cha hazina cha China.

Wasikilizaji wapendwa mliyosikia ni rekodi ya sauti za wanafunzi wa shule ya msingi wa Taiwan wakati waliposoma maandishi maarufu ya China "Hoja za Adabu". Waliyosoma yanahusu hoja za mwanafikra maarufu wa China ya kale Confucius, kuhusu jamii bora inayotarajiwa na watu wote, kwamba jamii bora inayotarajiwa na watu wote inapaswa kuwa ni jamii ambayo watawala wanaichukulia nchi kuwa ni nchi ya wananchi wote, ambapo watu wenye busara na uwezo wanachaguliwa kuwa watawala wa nchi; katika jamii hiyo watu wanafuata moyo wa dhati na uamini, na kujenga uhusiano wa masikilizano.

Katika miaka mingi iliyopita, wakazi wa Taiwan kama walivyokuwa wakazi wa China bara, walipewa elimu ya utamaduni wa jadi wa China tangu utotoni mwao, hata mpaka zama za karibu, aina ya elimu ya nchi za magharibi iliingizwa, utamaduni wa jadi wa China bado unachukua kiasi kikubwa katika elimu ya shuleni, na bado unafuatwa na watu. Mpaka sasa watu wa China bara na Taiwan bado wanatumia maandiko ya pamoja na kuongea lugha ya pamoja, hata kilugha wanachotumia wakazi wa Taiwan, chanzo chake ni mikoa ya Fujian na Guangdong ya China bara. Wakati huo huo wakazi wa Taiwan pia wanadumisha utamaduni wa pamoja na desturi nyingi za pamoja za maisha na zile za China bara, hayo yameonekana katika maisha yao ya kila siku na shughuli zao za kidini.

Mzee Zhu Fulai mwenye umri wa miaka 81 alipokuwa kijana alifika Xiamen, mkoani Fujian kutoka kando nyingine ya Mlango wa bahari wa Taiwan, tangu hapo akafanya shughuli na kufunga ndoa China bara, hakurudi tena Taiwan. Alipozungumzia desturi na mila za pande mbili China bara na Taiwan mzee huyo alisema, alipokuwa Taiwan, kila ifikapo sikukuu ya jadi ya mwaka mpya wa kichina, ambayo ni sikukuu kubwa na muhimu kabisa kwa taifa la China, watu wa kila familia hutengeneza chakula cha Niangao yaani chakula kilichotengenezwa kwa unga wa mchele. Mzee Zhu akisema:

Nilipokuwa mtoto, nyumbani kwetu Taiwan, kila ifikapo sikukuu ya jadi ya mwaka mpya wa kichina, mama yangu alikuwa anasaga mchele na kutengeneza Niangao. Naona desturi na mila za China bara na Taiwan karibu ni sawasawa kabisa.

Sikukuu ni sehemu moja muhimu ya utamaduni wa jadi wa taifa moja, sikukuu za jadi za wakazi wa Taiwan ni sawasawa na zile za wakazi wa China bara, na desturi na mila pia ni sawasawa. Kwa mfano, katika wakati wa sikukuu ya jadi ya mwaka mpya wa kichina, wakazi wa pande hizo mbili huwa wanatambika kwa mababu; kwenye mkesha wa sikukuu watu wa familia moja hukusanyika pamoja, kula chakula na kuagana na mwaka uliopita na kukaribisha mwaka mpya; sikukuu ya taa yaani Tarehe 15 Januari ya kalenda ya kilimo ya China, wakazi wa pande hizo mbili wote wanashiriki kwenye tamasha la taa; na sikukuu ya Qingming ya Tarehe 5 Aprili, wakazi wa pande hizo mbili wote wanakwenda kutoa heshima kwenye makaburi ya jamaa zao; na Tarehe 5 Mei ya kalenda ya kilimo ya China, watu wa familia zote za China bara na Taiwan wote wanapenda kula chakula cha Zongzi; katika sikukuu ya mbala mwezi ya tarehe 15 Agosti ya kalenda ya kilimo ya China, katika China bara na Taiwan, watu wa familia moja hukusanyika pamoja nyumbani, wanaburudika chini ya mbalamwezi huku wakila keki za Yuebin mithili ya mwezi na kumaanisha watu wote wa familia wamekusanyika pamoja.

Mbali na sikukuu za pamoja, wakazi wa China bara na Taiwan wanaabudu miungu ya pamoja, hata shughuli husika za kutambika karibu ni sawasawa, kwa mfano kila mwaka wakazi wa pande hizo mbili hufanya shughuli za kufanya matambiko kwa mungu Guandi.

Jina la Guandi ni Guanyu ambaye alikuwa jenerali maarufu wa China wakati wa karne ya 3. Alikuwa ni jenerali mwenye ustadi mkubwa wa kijeshi, alikuwa haogopi kila kitu, na alikuwa ni mtiifu kabisa wa bwana wake, vilevile ni mtu aliyethamini zaidi uaminifu na aliyewasaidia kwa dhati watu wengine, wachina walimpenda sana, hata baadaye walimwabudu kama mungu. Katika mlango wa bahari wa Taiwan, kwenye eneo la bahari ya karibu lililo karibu na upande wa China bara kuna kisiwa kimoja kinachoitwa Dongshan, kwenye kisiwa hicho kuna hekalu moja la Guandi lililojengwa karne ya 14, wakazi wengi wa Taiwan kila mwaka wanakwenda kwenye hekalu hilo kufanya matambiko kwa Guandi.

Tarehe 19 Juni ni siku ya kuzaliwa kwa Guandi. Mwaka huu, mapema ya siku hiyo, kwenye hekalu hilo, mishumaa inawashwa, sadaka za matunda, keki na nguruwe na kondoo waliochinjwa zinawekwa mbele ya sanamu ya Guandi. Watu wa pande mbili za Mlango wa bahari wa Taiwan walifika kwenye hekalu hilo, kufanya shughuli ya pamoja ya matambiko kwa Guandi.

Bwana Zhang kutoka mji wa Taibei kisiwani Taiwan alisema kuwa, nyumbani kwake kuna sanamu ya Guandi, kila siku wanatoa heshima mbele ya sanamu hiyo, alipokuwa mtoto alimfahamu Guandi na kuanza kumwabudu, katika miaka ya hivi karibuni karibu kila mwaka anakwenda kwenye kisiwa cha Dongshan kushiriki kwenye shughuli za kumtambika. Akisema:

Kisiwani Taiwan kuna waumini wengi wa Guandi, ambao wanafanya shughuli za aina mbalimbali za kumwabudu na kumtambika.

Malaika Mazhu ni malaika maarufu sana anayeabudiwa na wakazi wa China bara na Taiwan kwa pamoja. Inasemekana kuwa Mazhu ni malaika anayelinda usalama wa wavuvi wanaokwenda baharini kuvua samaki, ambaye alitokana na mwanamke mmoja wa enzi ya Song ya China ya kale ya miaka 1000 iliyopita. Wakazi wa pwani ya kusini mashariki ya China, kisiwa cha Taiwan na sehemu nyingi za Asia ya kusini mashariki wote wanamwabudu sana Mazu, na mahekalu ya Mazu yamejengwa katika sehemu nyingi mbalimbali, katika kisiwa cha Taiwan tu kuna mahekalu 74 ya Mazu, na makao makuu ya mahekalu ya Mazu yako kwenye kisiwa cha Meizhou ambacho ni kisiwa kidogo kilichoko kwenye mkoa wa Fujian wa China bara. Mpaka sasa bado kuna waumini wengi sana wa Mazu China bara na Taiwan, na mahekalu ya Mazu kila siku yanawapokea waumini wengi wanaokwenda kumwabudu Mazu.

Mtaalamu wa utafiti wa suala la Taiwan katika Taasisi ya sayansi ya jamii ya China Bibi Zeng Runmei alifahamisha kuwa, asilimia 98 ya wakazi wa Taiwan, mababu zao walikuwa wa China bara. Ingawa wakazi hao wengi wanaishi Taiwan kizazi baada ya kizazi, wanapenda ardhi hiyo ya Taiwan, lakini wakati huo huo pia hawawezi kusahau maskani yao ya zamani. Mkazi wa Taiwan Bwana Yang Kezheng, mababu zake walikuwa wa Kisiwa cha Dongshan ndicho kisiwa kile tulichokitaja hapo kabla ambacho kuna hekalu moja la kale la Guandi, alisema, maskani yake siku zote yanavuta hisia zake. Bwana Yang aliwekeza China bara na kuanzisha kiwanda zaidi ya miaka 10 iliyopita, sasa shughuli zake zinaendelea vizuri. Hivi karibuni ana mpango wa kuwekeza Yuan milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa "kituo cha maonesho ya utamaduni wa China bara na Taiwan" kwenye kisiwa cha Dongshan. Kituo hicho cha maonesho kitaonesha muziki wa jadi, nyimbo na mila za raia wa mkoa wa Fujian wa China bara na Kisiwa cha Taiwan vinavyotazamana, katikati yao kuna bahari ya mlango wa Taiwan. Bwana Yang akisema:

Utamaduni wa Taiwan na utamaduni wa Dongshan ya China bara ni wa pamoja. Nataka kuonesha utamaduni wa pamoja wenye chanzo cha pamoja wa maskani ya mababu zangu ya China bara na utamaduni wa Taiwan, ili kuimarisha mawasiliano kati ya watu wa China bara na Taiwan, na kujenga mazingira ya masikilizano kati ya watu wa pande hizo mbili.

Mtaalamu Zeng Runmei alisema:

Chanzo cha utamaduni wa taifa la China kiko China bara, wataalamu wa Taiwan wanatarajia sana kuanzisha mawasiliano na upande wa China bara; na Taiwan inahifadhi vizuri sana utamaduni wa jadi, mambo mengi ya huko yanastahili kuingwa na upande wa China bara.

Bibi Zeng alisema kuwa, akiwa mchina, anajivunia sana maendeleo ya pande mbili za China bara na Taiwan, hasa hivi leo hadhi ya China inainuka siku hadi siku duniani, hivyo anatarajia zaidi pande hizo mbili zitaunganishwa pamoja mapema iwezekanavyo, ili watu wa pande hizo mbili waweze kunufaika kwa pamoja na fahari ya ustawi wa taifa la China.

Wasikilizaji wapendwa, mliosikia ni wimbo maarufu unaopendwa na watu wa China bara na Taiwan uitwao: Watu wa vizazi vya dragon, wimbo huu ulitungwa na mwanamuziki maarufu wa Taiwan Bwana Hou Dejian. Wimbo huu unaeleza hivi: Mashariki ya kale ya dunia kuna dragon moja, jina lake ni China; mashariki ya kale ya dunia kuna watu wengi, wote ni vizazi vya baadaye vya dragon. Nakua chini ya miguu ya dragon mkubwa, nikawa mtu wa kizazi cha baadaye cha dragon, nina macho meusi, nywele nyeusi na ngozi ya kimanjano, daima milele ni mtu wa kizazi cha baadaye cha dragon.

Wasikilizaji wapendwa, kufikia hapa ndio tumemaliza kuwasomea makala ya nne ya shindano la chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Taiwan-kisiwa cha hazina cha China. Sasa tunatoa maswali mawili ili mjibu.

1. Taja sikukuu tatu za jadi za pamoja kati ya China bara na Taiwan.

2. Wakazi wa Taiwan ambao mababu zao waliwahi kuzaliwa na kuishi China bara wanachukua asilimia ngapi ya idadi ya jumla ya wakazi wa Taiwan?

Na hadi hapo ndio kwa leo tumemaliza kuwasomea makala zote za shindano la chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Taiwan ?kisiwa cha hazina cha China. Tunashukuru kwa kujiunga nasi na tunawatakia mafanikio katika chemsha bongo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-27