Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-27 21:26:06    
Kiwango cha kujitosheleza nishati cha China kimefikia asilimia 94

cri

Naibu mkurugenzi wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya taifa ya China Bw. Zhang Guobao, tarehe 13 kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanywa na ofisi ya habari ya baraza la serikali la China alisema kuwa, msingi wa sera za maendeleo ya nishati za China unajengwa nchini, hivi sasa kiwango cha kujitosheleza nishati cha China kimefikia asilimia 94, na kiwango cha kutegemea nchi za nje ni asilimia 6 tu. Pia alisema kuwa, maendeleo ya China katika sekta za uchumi na nishati yanaletea fursa kubwa ya biashara kwa dunia nzima, na China itaimarisha ushirikiano kati yake na nchi mbalimbali duniani katika sekta ya nishati katika siku zijazo.

Kuanzia mwaka 2004, bei ya mafuta ghafi ya kimataifa inaendelea kupanda, hali ambayo inaifanya jumuiya ya kimataifa ifuatilie suala la nishati. Baadhi ya watu wa nchi za nje wanaona kuwa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta inatokana na ongezeko la matumizi ya mafuta ghafi ya nchi zinazostawi kama vile China na India. Kwenye mkutano huo, Bw. Zhang Guobao alisema kuwa, maoni hayo hayaoneshi kwa usahihi hali ya soko la nishati la kimataifa.

"China ni nchi inayoendelea, msingi wa maendeleo ya nishati ni kujitegemea. Matumizi ya nishati ya China hayategemei sana nishati duniani, ambayo yanachukua asilimia 6 tu, na kiwango cha kujitosheleza nishati cha China kimefikia asilimia 94. Kiwango hicho kinazidi kwa asilimia 20 kiwango cha wastani wa kujitosheleza kwa nishati cha nchi za jumuiya ya ushirikiano na maendeleo ya uchumi."

Alisema kuwa, hivi sasa, China ni nchi ya pili inayotumia na kuzalisha nishati kwa wingi duniani, uzalishaji wa makaa ya mawe umekuwa wa kwanza duniani kwa miaka mingi, na mwaka huu uzalishaji wa mafuta ghafi unatazamiwa kufikia tani milioni 180. Lakini kwa kuwa katika miaka ya karibuni uchumi wa China umekuwa ukiongezeka kwa kasi, hivyo mahitaji ya nishati pia yanaongezeka. Mwaka 2004, uagizaji wa mafuta ghafi wa China kutoka nchi za nje ulikuwa tani milioni 117, ambao ulichukua asilimia 6.3 hivi ya ujumla wa biashara ya mafuta ghafi duniani.

Wakati China inapoagiza mafuta ghafi kutoka nchi za nje, pia inauza nishati kwa nchi nje. Mwaka jana China iliuza tani zaidi ya milioni 80 ya makaa ya mawe kwa nje, ambayo yametoa mchango kwa maendeleo ya nchi nyingine.

Imefahamika kwamba, ili kuhakikisha nishati, na kuunga mkono maendeleo ya uchumi wa nchini, China imetunga mpango wa maendeleo ya nishati wa kipindi cha karibu na cha muda mrefu. Bw. Zhang alifahamisha,

"Mpango huo unaeleza kuwa kubana nishati na kuongeza tija ya matumizi ya nishati ni kazi ya kipaumbele ya kutatua suala la nishati. Aidha, unasisitiza kurekebisha miundo ya nishati, na kuharakisha uzalishaji wa umeme kwa nishati ya nyuklia, nishati zinazoweza kutumika tena, na kukuza uzalishaji umeme kwa nguvu ya maji."

Hivi sasa nchini China, kiwango cha uzalishaji wa umeme kwa nishati ya nyuklia hakijafikia asilimia 2, ambacho ni chini ya kiwango cha asilimia 17 cha wastani duniani. Katika siku za usoni China itahimiza maendeleo ya uzalishaji wa umeme kwa nishati ya nyuklia, na kutumai kuwa ifikapo mwaka 2020, kiwango cha uzalishaji wa umeme kwa nguvu za nyuklia kitafikia asilimia 4; idara ya utungaji wa sheria ya China imepitisha sheria ya nishati zinazoweza kutumika tena, ambayo inatoa uhakikisho wa kisheria kwa maendeleo ya nishati zinazoweza kutumika tena kama vile nishati ya upepo. Aidha, China ina maliasili nyingi kabisa ya maji duniani, lakini inayotumika sasa haijafikia asilimia 20, hivyo uwezo wa kukuza uzalishaji wa umeme kwa nguvu ya maji ni mkubwa.

Licha ya hayo, China pia itaendelea kuchimba maliasili mpya ya mafuta na gesi. Kwa mujibu wa mpango uliotungwa na kamati ya maendeleo na mageuzi ya taifa, katika miaka 20 ijayo China itaweza kuzalisha tani milioni 180 za mafuta ghafi kwa mwaka.

Bw. Zhang alisisitiza kuwa, mbali na kutatua suala la nishati kwa msingi wa kujitegemea, China pia itapanua mawasiliano na ushirikiano na nchi nyingine duniani.

"Nchi mbalimbali duniani zinapotatua suala la nishati, zinafuata hali halisi ya maliasili za nchi yake yenyewe, na kushirikiana na nchi nyingine, hali hiyo sio ya ajabu. Katika siku za usoni, China itaendelea kushikilia sera za kupanua mlango katika kukuza nishati na kuhakikisha kazi ya usalama wa nishati, na kuimarisha na kuzidisha mazungumzo na ushirikiano kati yake na nchi mbalimbali duniani, jumuiya mbalimbali za kimataifa na kampuni za kimataifa katika sekta ya nishati. Kwa kweli, ushirikiano kati ya China na nchi nyingine katika sekta ya nishati ni wa kunufaishana."

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-27