Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-29 15:52:56    
Wajumbe wanawake tena mjini Beijingwa nchi mbalimbali duniani wakutana

cri

Huu ni mwaka wa maadhimisho ya miaka 10 tangu mkutano wa nne wa wanawake duniani wa Umoja wa Mataifa ufanyike mjini Beijing. Ili kuadhimisha miaka 10 tangu mkutano huo ufanyike, serikali ya China ilifanya mkutano wa maadhimisho mwishoni mwa mwezi Agosti. Wajumbe wengi waliohudhuria mkutano huo wa maadhimisho ni marafiki waliowahi kuhudhuria mkutano wa nne wa wanawake duniani. Kufika kwao tena mjini Beijing kumewapa mshangao mkubwa, kwani wamekuta maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii yamepatikana nchini China katika muda huo wa miaka 10, pamoja na kuinuka kwa hadhi ya wanawake wa China. Wajumbe hao wameeleza matumaini yao ya kuimarisha maingiliano na ushirikiano kati yao na China katika mambo ya wanawake na watoto.

Zaidi ya miaka 10 iliyopita, mkutano wa nne wa wanawake duniani wa Umoja wa Mataifa ulifanyika hapa Beijing, mkutano uliwashirikisha wajumbe wengi kabisa wa idara za serikali na jumuiya zisizo za kiserikali (NGO) katika historia ya Umoja huo. Wajumbe zaidi ya elfu 40 kutoka nchi na sehemu mbalimbali duniani walikusanyika hapa Beijing. Mkutano huo ulipitisha Taarifa ya Beijing na Mpango wa utekelezaji ambavyo hadi leo bado ni nyaraka zinazoelekeza maendeleo ya wanawake duniani.

Tarehe 29 hadi 31 Agosti, mkutano wa maadhimisho ulifanyika mjini Beijing.

Wajumbe zaidi ya 800 kutoka nchi kumi kadhaa na mashirika ya kimataifa walikusanyika hapa Beijing wakikagua kwa pamoja hali ya utekelezaji ya Taarifa ya Beijing na Mpango wa utekelezaji, na kujadiliana kuhusu namna ya kuimarisha maingiliano na ushirikiano katika maendeleo ya wanawake duniani. Serikali ya China ilitilia maanani sana mkutano huo, ambapo rais Hu Jintao wa China alitoa hotuba kwenye ufunguzi akiahidi kuwa, China itashirikiana na nchi mbalimbali duniani kusukuma mbele jitihada ya wanawake duniani.

Wajumbe wengi waliowahi kuhudhuria mkutano wa nne wa wanawake duniani walikuja tena Beijing. Kwenye bustani ya maadhimisho ya mkutano wa nne wa wanawake duniani iliyoko katika wilaya ya Huairou, mwitishaji mkuu wa baraza la NGO Bi. Khunying Supatra Masdit kutoka Thailand alisema:

"Bustani hiyo inanikumbusha shughuli za aina mbalimbali za NGO zilizofanyika hapa zaidi ya miaka 10 iliyopita, ambapo wanawake kutoka nchi mbalimbali duniani tulikusanyika pamoja kujadiliana kuhusu mambo ya wanawake. Nafurahi sana kurudi na kupata nafasi ya kukutana tena na marafiki kutoka nchi mbalimbali duniani."

Bi. Supatra alisema kuwa, safari hii alikuwa na picha tofauti kabisa kuhusu mji wa Beijing. Yaani mji wa Beijing umestawi zaidi na kupendeza zaidi kuliko miaka 10 iliyopita, miche ya miti iliyopandwa na wajumbe wanawake inayoashiria urafiki na matumaini, sasa imekuwa miti mikubwa.

Bi.Anisa Zeb Tahirkheli kutoka Pakistan ni waziri wa habari na utangazaji. Alisema kuwa, anapongeza sana mafanikio waliyopata wanawake wa China katika kazi zao na maisha yao. Akisema:

"Wanawake wa China wanajishughulisha na kazi za aina mbalimbali kama wanaume walivyo, wanawake wa Pakistan wanataka kujifunza uzoefu na maarifa kutoka kwa wanawake wa China katika kujipatia mafanikio kweney sekta za uchumi na biashara."

Kama alivyosema Bi. Anisa , wajumbe wengi kutoka nchi nyingine pia wanatarajia kuimarisha maingiliano kati yao na wanawake wa China, na kujifunza maarifa ya wanawake wa China kuhusu namna ya kujiendeleza na kujitegemea, ili kusukuma mbele maendeleo ya wanawake. Pia walifanya majadiliano kwa kina na wajumbe wa China kuhusu namna ya kuwashirikisha wanawake katika shughuli za utungaji sera, namna ya kuwalinda wanawake dhidi ya matishio ya matumizi ya mabavu, ugonjwa wa Ukimwi na mambo mengine.

Kwenye hoteli ya Beijing, mjumbe wa Beijing Bi Chen Huilai ambaye ni naibu katibu mkuu wa shirikisho la mameya wanawake la China alipojulisha hali ya maendeleo ya wanawake wa China alisema kuwa, kati ya marafiki zake, wengi ni wanakampuni wanawake, ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi nchini China. Alisema kuwa, zaidi ya miaka 10 iliyopita, idadi ya mameya wanawake nchini China ilikuwa zaidi ya 300 tu, sasa idadi hiyo imeongezeka maradufu. Wanawake hao wanafanya kazi kwa makini wakiwa na ari na ukakamavu mkubwa katika kujishughulisha katika mambo ya kisiasa.

Bi. Chen Huilai alisema kuwa, wanawake wa China wana usawa na wanaume katika mambo ya nyumbani, elimu ya watoto na haki ya kiuchumi. Akisema:

"Kwa mfano katika familia yangu, mimi na mume wangu kila mmoja anatumia mshahara wake mwenyewe, lakini kila tunapokula chakula kwenye mikahawa, mimi hulipa. Kufanya hivyo kunaonesha uwezo wangu na hadhi yangu nyumbani, hivyo naona furaha kubwa."

Lakini maendeleo ya wanawake nchini China na hali yao ya kimaisha bado ina tofauti kubwa katika sehemu tofauti. Katika sehemu kadhaa ambazo ziko nyuma kiuchumi, hali ya wanawake na watoto bado si ya kufurahisha. Kwa mfano, wanawake hawawezi kujitegemea kiuchumi, wasichana wa familia maskini wanakabiliwa na tishio kubwa zaidi la kutoweza kwenda shule kuliko wavulana. Suala hilo limefuatiliwa na wajumbe kadhaa waliohudhuria mkutano huo, ambao walieleza matumaini yao ya kushirikiana na China katika kuhimiza maendeleo ya jitihada za wanawake na watoto nchini China.

Mjumbe kutoka Australia Bi. Jane Zimmerman alikuwa amechangisha fedha nyingi katika kuwasaidia watoto wa kike wa familia zenye matatizo ya kiuchumi wa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani wa China kuendelea na masomo yao. Akisema:

"Naona wanawake wa China wamepata mafanikio makubwa, lakini bado kuna kazi nyingi zinazotakiwa kufanywa. Nafurahi sana kutoa mchango wangu ipasavyo katika kuhimiza maendeleo ya wanawake wa China."

Mkuu anayeshughulikia mambo ya kimataifa ya shirikisho kuu la wanawake la China Bi. Zhou Xiaoqiao alisema kuwa, China pia itajifunza uzoefu kutoka kwa wanawake wa nchi nyingine katika kuhimiza usawa wa kijinsia, na maendeleo ya wanawake, kuanzisha uhusiano mzuri zaidi na nchi mbalimbali na kuhimiza maingiliano na ushirikiano wa kirafiki kati ya China na nchi nyingine duniani.

Idhaa ya kiswahili 2005-09-29