Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-29 21:10:08    
Mito na Milima nchini China

cri
Mito

Nchini China kuna mito mingi, miongoni mwao mito zaidi ya 1500 ambayo kila mto ni wenye eneo la kilomita za mraba 1000. Mito hiyo inagawanyika katika mito ambayo maji yake yanatiririka na kuingia baharini na mito isiyoingia baharini. Eneo la mito ambayo maji yake yanaingia baharini, linachukua 64 % ya eneo la jumla la nchi kavu ya China. Mto Changjiang, Mto Huanghe, Mto Heilongjiang, Mto Zhujiang, Mto Liaohe, Mto Haihe na Mto Huihe ni mito ambayo maji yake yanatiririka kuelekea mashariki na kuingia kwenye Bahari ya Pasifiki; Mto Yaluzhangbujiang wa Tibet unatiririka kuelekea mashariki na kutoka nje, tena kuelekea kusini na kuingia bahari ya Hindi, ambapo unapita Bonde kubwa la kwanza duniani la Yaluzhangbujiang lenye urefu wa kilomita 504.6, na kimo cha mita 6009; Mto Erqisi wa Xinjiang ni mto ambao maji yake yanatoka nje na kuingia kwenye Bahari ya Arctic. Mito ile ambayo maji yao yanaingia kwenye maziwa au kupotelea kwenye jangwa na sehemu ya maji yenye chumvi, eneo lake linachukua 36 % ya eneo la jumla la eneo la nchi kavu ya China.

Mto Changjiang ni mto mkubwa wa kwanza wa China, urefu wake wa jumla ni kilomita 6300, ambao ni mto wa tatu kwa ukubwa duniani, ukiifuata Mto Nile wa Afrika na Mto Amazon wa Amerika ya kusini. Eneo la juu ya Mto Changjiang linapita milima na mabonde makubwa, ambapo maliasili nyingi ya maji zinalimbikizwa kwenye sehemu hizo. Mto Changjiang pia ni mto wa kimaumbile wa shughuli za uchukuzi toka mashariki hadi magharibi nchini China. Hali ya hewa ya eneo la katikati na chini la Mto Changjiang ni ya joto na unyevunyevu, kuna mvua za kutosha, na ardhi yenye rutuba, ambapo ni sehemu iliyoendelea kiviwanda na kilimo nchini China.

Mto Huanghe ni mto mkubwa wa pili wa China, urefu wa jumla wa mto huo ni kilomita 5464. Kwenye eneo la huo kuna malisho na mbuga na maliasili nyingi za madini, katika historia yake eneo hilo lilikuwa moja ya machimbuko muhimu ya ustaarabu wa zama za kale za China.

Mto Heilongjiang ni mto mkubwa wa kaskazini ya China, urefu wake ni kilomita 4350, miongoni mwake maji ya eneo la mto huo la kilomita 3101 yanapita sehemu za nchini China.

Mto Zhujiang ni mto mkubwa wa kusini ya China, urefu wake ni kilomita 2214.

Mto Talimu wa kusini ya Xinjiang ni mto mrefu kabisa wa China ambao maji yake hayaingii baharini, urefu wake ni kilomita 2179.

Mbali na mito ya kiasili, nchini China pia kuna mfereji mmoja maarufu unaopita kusini na kaskazini. Mfereji huo ulichimbuliwa kwa nguvu za binadamu kuanzia karne ya 5, ambao ulianzia Beijing, kaskazini ya China hadi Hangzhou wa mkoa wa Zhejiang, mashariki ya China, mfereji huo unapitisha mifumo mitano mikubwa ya Mto Haihe, Mto Huanghe, Mto Huaihe, Mto Changjiang na Mto Qiantangjiang, urefu wa mfereji huo ni kilomita 1801, ambao ni mfereji mrefu zaidi kuliko mingine duniani uliochimbuliwa kwa nguvu za binadamu mapema zaidi duniani.

Milima mikubwa maarufu ya China ni: Milima Himalaya, Milima Kunlun, Milima Tiansha, Milima Tanggula, Milima Qinling, Milima Daxinganling, Milima Taihang, Milima Qilian, na Milima Hengduan.

Milima Himalaya: Milima hiyo wa umbo wa upinde unatambaa kwenye sehemu ya mipaka kati ya China na India na Nepal, urefu wake ni zaidi ya kilomita 2400, mwinuko wake kutoka usawa wa bahari ni mita 6000, ambayo ni milima mikubwa na mirefu zaidi kuliko mingine yote duniani. Mwinuko wa kilele chake kikuu Jomolangma kutoka usawa wa bahari ni mita 8848.13, kilele hicho ni cha juu zaidi kuliko vingine vyote duniani.

Milima Kunlun: Milima hiyo inaanzia Uwanda wa juu wa Pamil katika upande wa magharibi, na upande wake wa mashariki unafikia kaskazini magharibi ya Mkoa wa Sichuan, China, urefu wake ni zaidi ya kilomita 2500, wastani wa mwinuko kutoka usawa wa bahari ni mita 5000-7000, kilele chake cha juu zaidi cha Gonggeer kina mwinuko wa mita 7719 kutoka usawa wa bahari.

Milima Tianshan: Milima Tianshan inasimama kwenye sehemu ya katikati ya Mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur wa kaskazini magharibi ya China, wastani wa mwinuko wake kutoka usawa wa bahari ni mita 3000-5000, kilele chake cha juu zaidi Tomoer kina mwinuko wa mita 7455.3 kutoka usawa wa bahari.

Milima Tanggula: Milima hiyo iko kwenye sehemu ya katikati ya Uwanda wa Juu wa Qinghai-Tibet, wastani wa mwinuko kutoka usawa wa bahari ni mita 6000, kilele chake cha juu zaidi Geladandong kina mwinuko wa mita 6621 kutoka usawa wa bahari, ambapo ni chanzo cha Mto Changjiang ambao ni mto mrefu zaidi nchini China.

Milima Qinling: Upande wa magharibi wa milima hiyo inaanzia mashariki ya Mkoa wa Gansu, upande wake wa mashariki kufika sehemu ya magharibi ya Mkoa wa Henan, wastani wa mwinuko wake ni mita 2000-3000 kutoka usawa wa bahari, kilele chake kikuu Taibai kina mwinuko wa mita 3767 kutoka usawa wa bahari. Milima hiyo ni mstari muhimu wa kijiografia kati ya kusini na kaskazini nchini China.

Milima Daxinganling: Upande wake wa kaskazini unaanzia sehemu iliyo karibu na Mto Mo wa mkoa wa Heilongjiang, kaskazini mashariki ya China, upande wake wa kusini unafika eneo la juu la Mto Laoha, umbali kutoka kusini hadi kaskazini ni kilomita 1000, wastani wa mwinuko wa kutoka usawa wa bahari ni mita 1500, kilele chake kikuu Huanggangliang kina mwinuko wa mita 2029 kutoka usawa wa bahari.

Milima Taihang: Toka kaskazini hadi kusini milima hiyo inatambaa kwenye ukingo wa mashariki ya Uwanda wa Juu wa Huangtu, urefu wake ni zaidi ya kilomita 400, wastani wa mwinuko kutoka usawa wa bahari ni mita 1500-2000, kilele chake cha juu zaidi Xiaowutaishan kina mwinuko wa mita 2882 kutoka usawa wa bahari.

Milima Qilian: Milima hiyo inatambaa katika sehemu ya ukingoni mwa kaskazini mashariki ya Uwanda wa Juu wa Qinghai-Tibet, wastani wa mwinuko wa kutoka usawa wa bahari ni zaidi ya mita 4000, na kilele chake kikuu kina mwinuko wa mita 5547 kutoka usawa wa bahari.

Milima Hengduan: Milima hiyo iko kwenye sehemu ya kusini mashariki ya Uwanda wa Juu wa Qinghai-Tibet na katika sehemu ya makutano kati ya mipaka ya mikoa mitatu ya Tibet, Sichuan na Yunnan, wastani wa mwinuko kutoka usawa wa bahari ni mita 2000-6000, kilele chake kikuu Gongga kina mwinuko wa mita 7556.

Milima Taiwan: Milima hiyo inapita upande wa mashariki ya Kisiwa cha Taiwan , wastani wa mwinuko wake kutoka usawa wa bahari ni mita 3000-3500, kilele chake kikuu Yushan kina mwinuko wa mita 3952 kutoka usawa wa bahari.

Zaidi ya hayo, nchini China pia kuna milima mingine maarufu kama vile Mlima Huang, Mlima Tai, Mlima Hua, Mlima Song, Mlima Heng, Mlima Ermei, Mlima Lu, Mlima Wudang na Mlima Yandang.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-29