Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-30 16:05:22    
Maliasili ya Ardhi ya China

cri

China ni nchi yenye eneo kubwa, maliasili ya ardhi ni ya aina nyingi, ardhi ya kilimo, misitu, ardhi yenye majani, jangwa na fukwe, zote zinapatikana nchini China kwa maeneo makubwa. Lakini sehemu kubwa ya ardhi ya China ni milima, sehemu za tambarare ni chache, na sehemu ya ardhi ya kilimo na misitu ni ndogo. Ardhi ya kilimo inapatikana zaidi katika tambarare na mabonde mashariki mwa China, na sehemu nyingi zaidi yenye misitu iko katika sehemu ya kaskazini-mashariki na kusini-magharibi mwa China, na ardhi kubwa zaidi zenye majani ziko katika nyanda za juu na sehemu za milima.

Ardhi ya kilimo:

Hivi sasa nchini China kuna hekta milioni 1.27 za ardhi ya kilimo, tukiigawa China katika sehemu ya mashariki, katikati na ya magharibi, ardhi hiyo ya kilimo katika sehemu ya katikati inachukua 43.2%, na sehemu za mashariki na magharibi, kila sehemu inachukua 28.4, na sehemu kubwa ya ardhi hiyo iko katika tambarare ya kaskazini-mashariki, tambarare ya kaskazini ya China, tambarare iliyoko katikati na ya mwisho ya Mto Changjiang, delta ya Mto Zhujiang na bonde la Sichuan. Ardhi katika tambarare ya kaskazini-mashariki ni ardhi nyeusi yenye rutuba nyingi, mimea inayolimwa zaidi katika sehemu hiyo ni ngano, mahindi, mtama, soya, mkonge na viazisukari. Ardhi katika tambarare ya kaskazini ya China ina rangi ya kahawia, mimea inayolimwa katika ardhi hiyo ni ngano, mahindi, uwele, mtama, pamba na njugunyasa. Katika tambarare kwenye sehemu ya katikati na ya mwisho ya Mto Chanjiang mimea inayopandwa zaidi ni mpunga, machungwa na rapa. Na katika bonde la Sichuan mimea inayolimwa zaidi ni mpunga, rapa, miwa, chai, machungwa na mabalungi.

Misitu:

Hivi sasa nchini China kuna hekta milioni 158.94 za misitu ambazo ni 16.55% ya eneo lote la China, kwa hiyo China ni nchi yenye misitu michache na ikilinganishwa na kiasi cha misitu kinachofunika 30.8% ya ardhi ya dunia kwa wastani China bado iko mbali. Misitu ya asili inapatikana zaidi katika sehemu ya kaskazini-mashariki na kusini-magharibi mwa China, na katika tambarare ya mashariki ya China yaani sehemu yenye watu wengi na maendeleo ya kiuchumi, na katika sehemu kubwa ya kaskazini- magharibi mwa China misitu ni michache sana.

Misitu ya China ina aina za miti karibu 2800, na miti yenye thamani kubwa ni metasequoia na ginkgo. Ili kukidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi, China imefanya harakati za kupanda misitu. Hivi sasa misitu iliyopandwa imekuwa hekta milioni 33.79, na kuifanya China kuwa nchi yenye eneo kubwa la misitu iliyopandwa duniani.

Sehemu kubwa ya misitu ya kiasili nchini China iko katika kaskazini-mashariki mwa China, ikiwa ni pamoja na sehemu ya mlima Daxinganling, Xiaoxinganling na mlima Changbai. Sehemu ya kusini-magharibi ya China ni sehemu ya pili yenye misitu mingi. Na sehemu ya kusini-mashariki ya China ni sehemu ya misitu iliyopandwa. Licha ya misitu hiyo, nchini China kuna utando wa misitu ya hifadhi, mathalan, kanda za misitu hifadhi iliyoenea katika China ya kaskazini-mashariki, kaskazini, na kaskazini-magharibi, jumla zina kilomita 7000 kwa urefu na hekta milioni 260 kwa maeneo ambayo ni robo ya nchi kavu ya China, huu ni mradi mkubwa kabisa duniani wa hifadhi ya mazingira.

Ardhi yenye majani:

Kuna hekta milioni 266.06 za ardhi yenye majani ambazo zinafaa kwa malisho nchini China, kuna aina za majani ambazo zinafaa kwa malisho ya mifugo ya aina mbalimbali katika majira tofauti. Ardhi yenye majani ni karibu robo ya eneo lote la China, na kuifanya China kuwa nchi yenye ardhi kubwa yenye majani duniani. Mbuga za majani ya kiasili nyingi ziko katika sehemu ya kaskazini-mashariki mwa China kuanzia mlima Daxinganling, mlima Yinshan hadi nyanda za juu za Qinghai-Tibet. Na mbuga za majani yaliyopandwa ziko katika sehemu ya kusini-mashariki ya China ambapo ziko pamoja na ardhi ya kilimo na sehemu za misitu.

Sehemu kubwa ya malisho iko katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani, mifugo iliyofugwa huko ni farasi Sanhe na ng'ombe Sanhe. Katika sehemu ya malisho mkoani Xinjiang wanafugwa kondoo wa Xinjiang wenye manyoya laini, kondoo wa Altai wenye mkia mnene na farasi wa Yili. Na katika sehemu ya malisho mkoani Qinghai waliofugwa wengi zaidi ni yak, ng'ombe wenye manyoya marefu, na farasi maarufu wa Hequ. Katika sehemu ya malisho mkoani Tibet wanaofungwa zaidi ni yak.