Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-30 16:12:11    
Thamani ya uwekezaji ya China barani Afrika yazidi Dola za kimarekani bilioni moja

 


cri

Tarehe 12 mwezi Septemba mwaka huu, shirika la kuhimiza biashara la China liliendesha maonesho ya biashara na uwekezaji kati ya China na Afrika hapa Beijing. Kwenye ufunguzi wa maonesho hayo, naibu mkuu anayeshughulikia mageuzi ya kiuchumi wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya China Bwana Li Haiyan alisema kuwa, katika miaka ya karibuni makampuni ya China yamewekeza miradi katika nchi 49 za Afrika, ambapo thamani ya uwekezaji huo imezidi dola za kimarekani bilioni moja.

Bwana Li Haiyan alifahamisha kuwa, katika miaka ya karibuni, China na nchi za Afrika zimeweka msingi mzuri wa kufanya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara. Mwaka 2004 thamani ya biashara kati ya China na Afrika iliongezeka na kufikia dola za kimarekani bilioni 30 kutoka ile ya bilioni 10.8 ya mwaka 2000, bidhaa muhimu za China zilizosafirishwa barani Afrika ni pamoja na zana za kilimo, pikipiki, bidhaa za umeme zinazotumika nyumbani na bidhaa za teknolojia ya juu, na bidhaa zilizoagizwa na China kutoka nchi za Afrika ni pamoja na mafuta ghafi, magogo, madini ya chuma, almasi, pamba na shaba.

Bwana Li Haiyan alisema kuwa, biashara kati ya China na Afrika inachukua asilimia 2 tu ya bidhaa zilizosafirishwa nje na kuagizwa kutoka nje, na kuchukua asilimia 3.5 tu ya biashara ya nje ya nchi za Afrika, hivyo bado kuna uwezo mkubwa wa kushirikiana. Katika miaka ya karibuni, miradi iliyowekezwa na makampuni ya China barani Afrika imebadilika kutoka mashirika ya kibiashara hadi mashirika ya kutengeneza bidhaa kwa kutumia malighafi za huko, kama vile kutengeneza bidhaa zilizohitajika katika nchi za Afrika, uchimbaji wa malighafi, mawasiliano ya barabara, na maendeleo ya kilimo.

Isitoshe, miradi ya mkataba na ushirikiano wa nguvukazi kati ya China na nchi za Afrika pia imekuwa ikiongezeka siku hadi siku. Thamani ya jumla ya miradi ya mkataba imezidi dola za kimarekani bilioni 30, ambapo miradi mingi mikubwa inashughulikia sekta za mafuta, umeme, mawasiliano ya barabara, mawasiliano ya simu na maji, na idadi ya wachina wanaofanya kazi barani Afrika imezidi laki moja.

Naibu mkuu wa idara inayoshughulikia mikutano ya shirika la kuhimiza biashara la China Bwana Du Zetian alifahamisha kuwa, ilipofika tarehe 31 Desemba mwaka 2004, serikali ya China ilisaini mikataba ya kusameheana ushuru na nchi 25 za Afrika zilizo nyuma kabisa kichumi duniani, na kuanzia tarehe mosi Januari mwaka 2005, bidhaa 190 za nchi hizo 25 zilizosafirishwa kuja nchini China zinafutiwa ushuru wakati wa kuingia kwenye soko la China. Ilipofika mwezi Juni mwaka 2004, China ilianzisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi na sehemu 53 za Afrika, na kusaini makubaliano ya biashara ya pande mbili na nchi 41, kusaini makubaliano ya kuhimiza na kuhakikisha uwekezaji vitega uchumi na nchi 26 za Afrika, na kusaini makubaliano ya kukwepa kutoza ushuru maradufu na nchi 8 za Afrika.

Naibu mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa Ethiopia Bwana Solomon Afewerki kwenye maonesho hayo alisema kuwa, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Afrika una uwezo mkubwa wa kusaidiana katika mahitaji. Afrika ni bara lenye maliasili nyingi, hali yake nzuri ya kimaumbile inafaa sana kwa wanakampuni wa China kuendeleza kilimo, misitu, ufugaji na uvuvi. Pia alisema kuwa, faida ya uwekezaji katika sekta ya kilimo ya nchi za Afrika mashariki itafikia asilimia 40 hadi 45, na maliasili za dhahabu, almasi, mafuta na gesi za Afrika zinahitajiwa sana nchini China.

Maonesho ya biashara na uwekezaji kati ya China na Afrika ni moja ya shughuli zilizofanywa kwenye semina ya wanaviwanda na wafanyabiashara kati ya China na Afrika. Wenyeviti wa vyama vya wafanyabiashara na maofisa wa kiuchumi na kibiashara 30 kutoka Ethiopia, Afrika ya Kusini, Uganda na Guinea ya Ikweta walishiriki katika semina hiyo kuhusu namna ya kusimamia chama cha wafanyabiashara. Watu walioshiriki kwenye semina hiyo pia walitembelea Guangzhou na Zhuhai, kusini mwa China, na kufanya majadiliano na wanaviwanda wa China.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-30