Katika hali ambayo bei ya mafuta duniani inapanda siku hadi siku, mkutano wa 18 wa mafuta duniani ulifungwa tarehe 29 huko Johannesburg, Afrika ya kusini. Katika mkutano huo wa siku tano, wafanyabiashara wakubwa wa mafuta, maofisa wa serikali na wataalamu wapatao zaidi ya 4000 kutoka nchi mbalimbali duniani walikuwa wanatathmini hali sasa ya mafuta ilivyo duniani na mustakabali wake, na kujadili maendeleo endelevu ya nishati duniani. Waziri wa migodi na nishati wa Afrika kusini Bi. Lindiwe Hendricks kwenye sherehe ya ufungaji wa mkutano huo alisema kuwa, mkutano huo umeonesha matakwa ya nchi mbalimbali duniani hasa nchi za Afrika ya kutaka kufanya ushirikiano katika sekta ya mafuta.
Mkutano wa mafuta duniani ulianzishwa mwaka 1933, ni jumuiya isiyo ya kiserikali na isiyo ya kutafuta faida ya mafuta duniani, yenye nchi wanachama 59.
Mkutano huo ulifuatiliwa zaidi kuliko mikutano iliyopita kutokana na kwamba, kwanza katika miaka miwili ya karibuni, bei ya mafuta duniani imepanda juu kwa haraka, na imekuwa sababu kubwa ya kuathiri maendeleo ya uchumi duniani. Pili, hii ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika barani Afrika tangu uanzishwe miaka 72 iliyopita, na bara la Afrika lenye akiba kubwa ya mafuta limekuwa shabaha mpya inayogombewa na nchi kubwa zinazotumia sana mafuta duniani zikiwemo Marekani na Japan.
Shirika la OPEC limekadiria kuwa ifikapo mwaka 2020, mahitaji ya mafuta duniani yataongezeka kufikia mapipa milioni 107 kwa siku, na kiasi hicho kitafikia mapipa milioni 121 ifikapo mwaka 2030. Katika miaka kumi kadhaa ijayo, nishati zinazochimbwa zikiwemo mafuta na makaa ya mawe bado zitachukua asilimia 85 za mahitaji ya nishati duniani. Kwa hivyo jinsi ya kuhakikisha uwiano kati ya uzalishaji na mahitaji ya mafuta na kudumisha bei ya mafuta inayokubalika kwa pande zote mbili zinazozalisha mafuta na zinazoagiza mafuta, limekuwa suala linalohitaji kutatuliwa kwa haraka ili uchumi wa dunia unaendelea katika hali ya utulivu.
Kwenye mkutano huo jinsi ya kuzuia bei ya mafuta duniani isipande na jinsi ya kuwanufaisha watu wa Afrika kutokana na maliasili ya mafuta, imekuwa mijadala miwili muhimu yawashiriki wa mkutano huo.
Ili kuzuia bei ya mafuta duniani isipande haraka, mwenyekiti wa mkutano wa mafuta duniani bwana Eivalroren aliwataka wazalishaji, watumiaji na kampuni za mafuta zifanye juhudi kwa pamoja ili kutuliza soko la mafuta duniani. Rais Thabo Mbeki wa Afrika ya kusini kwenye ufunguzi aliainisha kuwa, bei kubwa ya mafuta itaathiri juhudi za kupambana na umaskini. Baadhi ya watu waliohudhuria mkutano huo pia walisema kuwa, mashindano mabaya kati ya makundi yanayojihusisha na biashara ya mafuta hatimaye yataleta hasara kubwa kwa maendeleo ya uchumi duniani na maslahi ya binadamu. Hivyo nchi zinazozalisha mafuta na nchi zanazotumia mafuta zinapaswa kushirikiana ili kukabiliana na changamoto za bei kubwa ya mafuta. Wakiainisha kuwa, Marekani ikiwa nchi inayotumia na kuagiza mafuta mengi kutoka nje, na yenye akiba kubwa zaidi ya mafuta ya kimkakati duniani inapaswa kuwajibika zaidi katika kuzuia kupanda kwa bei ya mafuta.
Hivi sasa akiba ya mafuta iliyogunduliwa barani Afrika inachukua nafasi ya tatu duniani, watalaamu wamekadiria kuwa ifikapo mwaka 2010, uzalishaji wa mafuta barani Afrika utachukua asilimia 20 ya jumla ya uzalishaji wa mafuta duniani. Lakini maliasili nyingi za mafuta bado haziwezi kuzisaidia nchi za Afrika kuondokana na umaskini, kwa sababu uzalishaji wa mafuta barani Afrika unadhibitiwa na makampuni kadhaa makubwa ya mafuta ya Marekani na nchi za Ulaya. Hivyo wajumbe walikosoa hali hiyo na wamezitaka nchi zilizoendelea na makampuni makubwa ya mafuta duniani yachukue hatua halisi ili kuhakikisha nchi za Afrika zinanufaika na maliasili zao za mafuta.
Vyombo vya habari vimeainisha kuwa, jumuiya ya kimataifa inapaswa kushirikiana ili kukabiliana na hali mbaya ya soko la mafuta duniani, kuimarisha mazungumzo na ushirikiano, na kufaidika na maliasili ya mafuta kwa pamoja.
Idhaa ya Kiswahili 2005-09-30
|