Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-30 20:06:06    
Tamasha la utamaduni wa China kufanyika Marekani

cri
    Tamasha la utamaduni wa China litazinduliwa Tarehe 1 mwezi Oktoba huko Washington, mji mkuu wa Marekani. Wasanii zaidi ya 900 watawaonesha watu wa Marekani utamaduni na sanaa za China kwa muda wa mwezi mmoja.

    Tamasha la utamaduni wa China, ambalo limeandaliwa na wizara ya utamaduni ya China na kituo cha maonesho ya sanaa cha Kennedy, Marekani, litakakuwa maonesho makubwa kuhusu mambo ya utamaduni ya China nchini Marekani.

    Ofisa kutoka wizara ya utamaduni ya China Bw. Pu Tong alisema kuwa tamasha hilo la utamaduni litakuwa na shughuli nyingi na mtindo mpya ambao unawakilisha kiwango cha juu cha sanaa ya utamaduni ya China kwa hivi sasa. Alisema, "Tumetayarisha mambo ya aina zaidi ya 30 ambayo yataoneshwa kwenye tamasha la utamaduni la China kwenye kituo cha sanaa cha Kennedy. Kutokana na hali ya vikundi vya wasanii na maonesho, ninaona kuwa kiwango chao ni cha kuwakilisha mafanikio mapya katika eneo la uvumbuzi wa sanaa wa China bara, tena ni cha kiwango cha juu kabisa. Tunaamini kuwa tamasha hilo la utamaduni itaimarisha maelewano na urafiki kati ya watu wa nchi mbili za China na Marekani."

    Habari zinasema kuwa tamasha hilo la utamaduni litaonesha mitindo 24 ya michezo kwa mara 43, ambayo itaoneshwa na wasanii wa kiwango cha juu kabisa kutoka China. Kwa mfano kikundi cha michezo ya opera ya Beijing cha China, ambacho ni cha kiwango cha juu cha uimbaji wa opera ya Beijing nchini China, kitaonesha opera ya Kibeijing ya "Jemadari wa kike wa ukoo wa Yang". Kikundi cha sanaa ya wananchi cha Beijing ambacho kilianzishwa miaka mingi iliyopita, kitaonesha "mgahawa wa chai".

    Tarehe 1 mwezi Oktoba ni siku ya taifa ya China, tamasha la utamaduni la China litaanza na shughuli za "Wiki ya Utamaduni wa Beijing" yakiwemo maonesho kwenye sherehe ya ufunguzi. Mkurugenzi wa ofisi ya habari ya serikali ya mji wa Beijing bibi Wang Hui alisema, "Tutaonesha wiki ya utamaduni wa Beijing kwenye kituo cha sanaa cha Kennedy nchini Marekani kwa shughuli 17 zenye kaulimbiu ya 'ushawishi wa Beijing, utamaduni wa michezo ya Olimpiki' ambazo ni pamoja na maonesho, michezo, mihadhara na shughuli za kusherehekea kwenye uwanja ili kuonesha sura ya Beijing ambayo ni kituo cha utamaduni, mji mkuu maarufu wa kale na mji wa kisasa duniani, na kuongeza ufahamu wa watu wa Marekani kuhusu Beijing."

    Bibi Wang alisema kuwa wiki ya utamaduni wa Beijing itakuwa na maonesho kuhusu "Ushawishi wa Beijing, utamaduni wa michezo ya olimpiki", picha 80 zitakazoonesha utamaduni wa kale, historia, utamaduni na sura ya mji wa Beijing, licha ya hayo kuna picha 40 zitakazoonesha maendeleo mapya ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 ikiwa ni pamoja na kuhusu viwanja na majumba ya michezo na hali ya kushiriki katika maandalizi ya michezo ya Olimpiki kwa wakazi wa Beijing.

    Habari zinasema kuwa tokea mwezi Mei, kituo cha sanaa cha Kennedy kilianza kushughulikia matangazo kuhusu tamasha la utamaduni wa China pamoja na uuzaji wa tiketi za maonesho, hivi sasa tiketi nyingi zimenunuliwa. Takwimu za mwanzo zinaonesha kuwa watu karibu laki 4 wataangalia maonesho ya michezo ya sanaa ya tamasha la utamaduni wa China, licha ya hayo kutakuwa na watu milioni 1 ambao wataangalia tamasha la utamaduni wa China kwenye televisheni na Internet.

Idhaa ya Kiswahili