Mawaziri wa mambo ya nje wa India na Pakistan Bwana Natwar Singh na Khursheed Kasuri tarehe 4 walimaliza mazungumzo ya siku mbili huko Islamabad, mji mkuu wa Pakistan. Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo, pande hizo mbili zimesema kuwa, India na Pakistan zitaendelea kusukuma mbele mchakato wa mazungumzo kwa pande zote, na kufanya juhudi halisi kwa ajili ya kutatua kiamani suala la Kashmir.
Waziri Singh alifanya ziara nchini Pakistan kuanzia tarehe 1 kutokana na mwaliko wa waziri Kasuri. Katika mazungumzo hayo, mawaziri wa mambo ya nje wa Pakistan na India walikumbusha pamoja hali ya maduru mawili ya mazungumzo kati ya nchi hizo mbili, na kufikia maoni ya pamoja juu ya hali husika ya duru lijalo la mazungumzo hayo. Katika taarifa ya pamoja, pande hizo mbili zimesisitiza kuwa, suala la Kashmir linapaswa kutatuliwa kwa njia ya kufanya majadiliano ya amani, na kamwe hazitaruhusu nguvu ya ugaidi izuie mchakato wa amani ya nchi hizo mbili.
Baada ya mazungumzo kumalizika, pande hizo mbili pia zilitangaza kuwa, duru la tatu la mazungumzo kati ya India na Pakistan litafanyika wakati wa mwezi Januari hadi Julai, ambapo pande hizo mbili zitajadili masuala kuhusu Jamu and Kashmir, milima ya barafu ya Siachen, mradi wa uelekezaji wa usafiri wa Talbot, mipaka kwenye bahari ya Sir Creek, mapambano dhidi ya ugaidi na shughuli za magendo ya dawa za kulevya. Pande hizo mbili pia zimejadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na kutuma maofisa wa kidiplomasia kwa kila upande.
Chini ya juhudi za pamoja za pande hizo mbili India na Pakistan, mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamepata matokeo mengi. Mambo yanayostahiki kutajwa ni kuwa, mkutano wa kamati ya pamoja ya uchumi ya India na Pakistan umeitishwa tena tarehe 4 baada ya kukomeshwa karibu kwa miaka 16. Mkutano huo ulijadili kuhusu kuinua kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili. Katibu anayeshughulikia mambo ya kidiplomasia wa India Bwana Shyam Saran amesema kuwa, kufanyika tena kwa mkutano wa kamati ya pamoja ya uchumi ya India na Pakistan kumeonesha kuwa, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya India na Pakistan unaboreshwa siku hadi siku.
Vyombo vya habari vimeona kuwa, mazungumzo hayo ya mawaziri wa mambo ya nje wa India na Pakistan hayajaweza kupata maendeleo yoyote kuhusu suala la Kashmir linalofuatiliwa zaidi na pande hizo mbili. Katibu anayeshughulikia mambo ya kidiplomasia wa India Bwana Shyam Saran tarehe 3 baada ya mazungumzo kumalizika alisema kuwa, India inapenda kushirikiana na Pakistan katika kuchukua hatua zote kuboresha suala la ubinadamu huko Kashmir. Lakini alisema pia, India itadumisha tahadhari yake kabla ya kutokomezwa kwa vitendo vya Pakistan vya kuvuka mipaka na kujipenyeza. Juu ya hiyo, katibu anayeshughulikia mambo ya kidiplomasia wa Pakistan Bwana Riaz Mohammed Khan tarehe 4 alisema kuwa, Pakistan imefanya juhudi kubwa katika kupambana na ugaidi na kuzuia vitendo vya kuvuka mipaka na kujipenyeza.
Wachambuzi wanaona kuwa, utatuzi wa suala la Kashmir ni suala muhimu la kutimiza amani na utulivu wa kudumu katika sehemu ya Asia ya kusini. Kutatuliwa kwa suala hilo kunazitaka India na Pakistan kutoa busara na juhudi za pamoja. Kudumisha mazungumzo na majadiliano kati ya nchi hizo mbili kunasaidia kutatua masuala mengine yaliyoko kati ya nchi hizo mbili. Na utatuzi wa masuala hayo hakika utaweka hali ya kusaidia kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili na ufumbuzi wa suala la Kashmir.
|