Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-06 20:45:28    
Vyama vya wafanyakazi vya China vyachangia kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi

cri

Maendeleo ya uchumi wa soko huria nchini China yamechomoza kwa mashirika mengi yenye umilikaji wa aina mbalimbali, ambayo yametatanisha uhusiano kati ya waajiri na waajiriwa. Ili kujipatia faida kubwa, baadhi ya mashirika binafsi hukiuka haki na maslahi ya wafanyakazi. Katika hali hiyo mpya, vyama vya wafanyakazi nchini China vinatakiwa kuimarisha jukumu lake ipasavyo ili kutetea haki na maslahi halali ya wafanyakazi. Hivi leo, wafanyakazi walionyimwa haki zao huomba msaada kutoka kwa vyama vya wafanyakazi.

Bwana Tong Guanghong mwenye umri wa miaka zaidi ya 30, mwaka mmoja na zaidi uliopita alisaini mkataba wa ajira wa mwaka mmoja na kampuni moja binafsi ya mji wa Yiwu, mkoani Zhejiang. Kwa mujibu wa mkataba, mwaka mmoja ulipokwisha, mwenye kampuni angetakiwa kumlipa mara moja mshahara wake wa mwaka mmoja wa Yuan za Renminbi elfu 25. Lakini kutokana na kampuni hiyo kudaiwa madeni, mwenye kampuni alikimbilia bila kumpa Bwana Tong Guanghong mshahara wake. Bwana Tong alikuwa hana njia nyingine ila tu kuomba msaada kutoka kwa shirikisho la wafanyakazi la mji wa Yiwu. Akisema:

"Nilipokelewa kwa ukarimu, watumishi wa shirikisho la wafanyakazi walinituliza kwa kuniambia kuwa, watashughulikia vizuri kesi yangu."

Kutokana na kutofahamu mambo ya sheria, Bw. Tong Guanghong alifahamishwa utaratibu husika wa kisheria na kusaidiwa kutayarisha mashtaka ambayo yalikabidhiwa kwenye kamati ya usuluhishi ya kazi ya mji wa Yiwu iliyoundwa na idara ya usimamizi ya kazi, shirikisho la wafanyakazi la mji huo na idara ya maendeleo ya kiuchumi. Kutokana na juhudi za kituo cha kutetea haki cha shirikisho la wafanyakazi, malalamiko yake yalikubaliwa haraka na kamati ya usuluhishi, na tena alifutiwa gharama ya kufungua kesi kutokana na matatizo yake ya kiuchumi.

Bwana Wang Yeqing kutoka kituo cha kutetea haki na maslahi cha shirikisho la wafanyakazi la Yiwu ni mjumbe wa kamati ya usuluhishi. Alisema:

"Hukumu ya usuluhishi bado haijatolewa, tutafuatilia kesi hiyo na kumsaidia Bw. Tong Guanghong mpaka apate mshahara wake."

Katika jumba la shirikisho la wafanyakazi la Yiwu, mwandishi wetu wa habari alishuhudia pilikapilika nyingi kwenye kituo cha kutetea haki kwa kutumia sheria cha shirikisho hilo. Kituo hicho kina ofisi ya kuwapokea wageni, ofisi ya kutoa maelekezo ya kisheria, ofisi ya kufanya usuluhishi na ofisi ya kupokea simu za waombaji msaada. Naibu mwenyekiti wa shirikisho la wafanyakazi la Yiwu Bwana Zhao Lan alifahamisha kuwa, kituo hicho licha ya kushughulikia huduma za kusuluhisha migongano ya kazi, kufungua mashtaka kwa niaba ya wafanyakazi, pia kitatoa mafunzo ya kisheria kwa wafanyakazi.

Yiwu ni mji wenye wafanyakazi wengi wanaotoka sehemu nyingine. Na wafanyakazi hao wanaridhishwa na mazingira ya kazi ya huko kutokana na haki na maslahi yao kuweza kuhakikishwa na shirikisho la wafanyakazi la mji huo.

Kama ulivyofanya mji wa Yiwu, mashirikisho ya wafanyakazi katika sehemu nyingine nchini China pia yanawajibika vizuri katika juhudi za kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi. Shirikisho la wafanyakazi la mji wa Tianjin, kaskazini mwa China, limeanzisha kituo cha huduma cha wafanyakazi. Kituo hicho kina watumishi zaidi ya 100, simu za kupokea maombi au maswali ya wateja zinafanya kazi saa 24 kwa siku. Kina mifumo 7 inayopokea maombi kwa haraka ambayo ni pamoja na kutoa msaada kwa wafanyakazi wenye matatizo ya kiuchumi, usalama wa kazini, kusawazisha uhusiano kati ya wafanyakazi vibarua na wenye kampuni .

Mwenyekiti wa shirikisho la wafanyakazi la mji wa Tianjin Bwana San Xiangjun alisema:

"Kwa mfano, tukipata habari kuhusu kampuni fulani kutokewa na ajali ya kazini, tutakwenda mara moja kupiga picha za video kuhusu namna kampuni hiyo inavyoshughulikia tukio hilo. Kama wafanyakazi waliohusika wakiwa na malalamiko kuhusu matokeo ya utatuzi, video hiyo ni ushahidi bayana. Ikiwa maslahi ya waathirika yanakiukwa, tunawasaidia kufungua mashtaka."

Bwana San alisema kuwa, kituo kinachoshughulikia kutoa msaada kwa wafanyakazi wenye matatizo ya kiuchumi ni kituo chenye shughuli nyingi sana, baadhi ya wakati kwa siku kinawapokea watu karibu mia moja wanaoomba msaada. Katika miaka mitatu iliyopita, kituo hicho kimewasaidia watu laki moja na elfu 60.

Sehemu ya Xinyang mkoani Henan, katikati ya China ni sehemu ya kilimo. Kutokana na maendeleo ya kilimo cha kisasa, nguvukazi ya ziada inaongezeka siku hadi siku, wakulima wengi wanamiminikia mijini kutafuta kazi za vibarua. Imefahamika kuwa, hivi sasa wakulima zaidi ya milioni 1.4 wa sehemu hiyo wanafanya kazi za vibarua nchini kote. Ili kutetea haki na maslahi yao, shirikisho la wafanyakazi la mji wa Xinyang limeanzisha mfumo wa kutetea haki na maslahi ya wakulima hao vibarua katika sehemu wanazotoka na sehemu wanazokwenda kufanya kazi. Mwenyekiti wa shirikisho hilo bwana Chen Ming alisema:

"Kabla ya kuondoka nyumbani, wakulima hao wanaambiwa wajiunge na shirikisho la wafanyakazi kwa kufuata utaratibu uliowekwa, na tunawapa kadi ya uanachama. Baada ya kufika kwenye sehemu zao za kazi, tunahamisha mafaili yao kwenye chama cha wafanyakazi cha huko waliko. Kwa kufanya hivyo wakulima hao wanapokumbwa na tukio lolote, haki zao za kimsingi zitahakikishwa kwa ufanisi."

Bwana Chen alisema kuwa, mafanikio makubwa yamepatikana katika miaka mitatu iliyopita tangu mji huo uanzishe mfumo wa kutetea haki na maslahi katika pande mbili, umeanzisha mtandao wa kutetea haki za wafanyakazi katika ngazi nne za mji, wilaya, tarafa na vijiji. Kwa ujumla limewasaidia wakulima vibarua kurudisha mishahara zaidi ya Yuan milioni 140 iliyocheleweshwa au kunyimwa, kusaini mikataba ya kazi zaidi ya laki tatu, kushughulikia kesi kadhaa zilizokiuka haki za wakulima vibarua kutokana na kukumbwa na matukio ya kujeruhiwa kazini.