Asubuhi ya tarehe 8 saa mbili na dakika 50 hivi matetemeko makubwa yenye ngazi ya Richter 7.6 yalitokea katika sehemu karibu na Kashmir upande wa Pakistan. Sehemu yote ya kaskazini ya India na mji mkuu wa Afghanistan Kabul iliathirika. Habari zinasema kuwa kiasi cha watu 3,000 walipoteza maisha katika matetemeko hayo.
Habari kutoka idara za matetemeko za Pakistan, India na Marekani zinasema kuwa kitovu cha matetemeko hayo kiko upande wa kaskazini mashariki wa mji mkuu wa Pakistan Islamabad kwa kilomita 95, na kilomita 70 mbali na mji mkuu sehemu ya Kashmir upande wa Pakistan Muzaffarabad. Chanzo cha matetemeko hayo kiko chini ya ardhi kwa kilomita 6. Nchi tatu za Pakistan, India na Afghanistan zote ziliathirika, na sehemu iliyoathirika vibaya zaidi ni sehemu ya kaskazini ya Pakistan na sehemu ya Kashmir upande wa Pakistan na upande wa India.
Serikali ya Pakistan imethibitisha kuwa watu zaidi ya 1,000 walikufa katika sehemu ya Kashmir upande wa Pakistan. Kutokana na maporomoko ya majumba katika miji mingi ya sehemu ya katikati na ya kaskazini ya Pakistan, idadi ya vifo itaongezeka. Habari nyingine zinasema kuwa idadi ya watu waliokufa katika sehemu ya mpakani ya kaskazini magharibi ya Pakistan imefikia 1,600 kutoka 500. Habari kutoka ubalozi wa China nchini Pakistan zimetangaza kuwa hadi jioni ya tarehe 8 wafanyakazi wanne wa China walikufa na mmoja alipotea.
Katika sehemu ya Kashmir upande wa India watu wasiopungua 250 walikufa na 850 walijeruhiwa, majumba 2,700 yaliporomoka na barabara zilikatika kutokana na maporomoko ya mlima. Hadi sasa huduma za maji, umeme na mawasiliano ya simu bado hazijarejeshwa, kwa makadirio ya serikali ya India, idadi ya watu waliokufa na kujeruhiwa itaongezeka. Vyombo vya habari vya India vilitangaza kuwa kuna upungufu mkubwa wa maji, chakula na mahema katika sehemu iliyoathirika. Hali ya hewa imekuwa baridi katika sehemu ya Kashmir upande wa India, halijoto imekuwa chini ya nyuzi 10 centigrade, kwa hiyo huduma za waathirika zinahitajika haraka. Afghanistan haikuathirika sana, lakini pia kuna mtoto mmoja kufariki kwa kuangukiwa na oromoko la nyumba.
Baada ya matetemeko, serikali za Pakistan na India zilipeleka askari na helikopta kufanya uokoaji. Waziri mkuu wa Pakistan Pervez Musharraf alikwenda kwenye sehemu iliyoathrika zaidi kukagua hali ya maafa, alisema matetemeko ni mtihani kwa wananchi wa Pakistan, serikali imeanza shughuli za uokoaji, askazi, polisi na wahudumu wa uokoaji wote wamekuwa vitendoni kushughulika na uokoaji, tiba na kuondoa vifusi. Waziri mkuu wa India Manmohan Singh alisema, serikali kuu ya India itafanya uokoaji kadiri iwezavyo, mfuko wa uokoaji umetenga fedha kuwasaidia waathirika.
Jambo linalostahili kutajwa ni kwamba waziri mkuu wa India Bw. Singh katika siku hiyo hiyo jioni alimpigia simu waziri mkuu wa Pakistan, Bw. Musharraf akitoa mkono wa pole kwa hasara kubwa ya watu na mali. Bw. Singh alisema, India iko tayari kutoa misaada kwa Pakistan. Kabla ya hapo, waziri na katibu wa mambo ya nje wa India walipeleka simu na kusema kwamba pindi Pakistan ikihitaji, India itatenda mara moja mambo ya kuisaidia Pakistan.
Maafa ya Pakistan na India kutokana na matetemeko hayo ya ardhi yanafuatiliwa sana kimataifa. Rais wa China Hu Jintao alituma salaam kwa Musharraf na kusema kwamba anaiamini serikali ya Pakistan itafanikiwa kupambana na shida na kujenga upya taifa. Rais wa Marekani Bw. Bush pia alitoa mbirambi kwa watu waliokufa. Hivi sasa nchi kadhaa zimeonesha kutaka kutoa misaada.
Idhaa ya kiswahili 2005-10-09
|