Hadi tarehe 10 katika muda wa siku tatu tu, mashambulizi na matukio ya utekaji nyara yalitokea mara nyingi, hali hiyo imewatia watu wasiwasi kuhusu mazungumzo ya amani yanayoendelea sasa kuhusu mgogo wa Darfur.
Hivi sasa Umoja wa Afrika umepanga askari wake 6,000 huko Darfur kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusimamisha vita yaliyopatikana mwezi Aprili mwaka jana kati ya serikali ya Sudan na makundi yenye silaha yanayopinga serikali. Tarehe 8 tukio la kuwashambulia askari wa Umoja wa Afrika ni tukio la kwanza tokea jeshi la Umoja huo lipelekwe huko Darfur. Katika tukio hilo askari watatu waliuawa na madereva wawili wenyeji kujeruhiwa. Umoja wa Afrika umetoa taarifa ya dharura na kushutumu wazi kuwa kundi la "Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan" (Sudan Liberation Movement) lazima lilaaniwe. Mwenyekiti wa ujumbe wa "Vuguvugu la Haki na Usawa" (the Justice and Equality Movement) uliohudhuria kwenye mazungumzo ya amani ya Dafur huko Abuja alitangaza kuwa katika siku mbili za tarehe 9 na tarehe 10 kiongozi wa watu waliowateka nyara watu kumi kadhaa wa Umoja wa Afrika ni mwanachama wa kundi hilo, na kinara huyo alifukuzwa nusu mwaka uliopita, na hivi sasa anafanya shughuli zake kwenye mpaka wa Sudan na Chad, na kusema kwamba Vuguvugu la Haki na Usawa lingependa kushirikiana na Umoja wa Afrika kumtafuta mtu huyo.
Habari nyingine zinasema kuwa msemaji wa Umoja wa Afrika nchini Sudan Bw. Moureddine Muzni tarehe 10 alitangaza kuwa kundi linaloipinga serikali la Sudan katika sehemu ya Darfur limewaachia huru watu 36 wa Umoja wa Afrika, lakini wengine wawili bado wanashikiliwa.
Mgogoro katika sehemu ya Darfur ulitokea mwezi Februari mwaka 2003, makundi mawili yanayopinga serikali yanayoundwa na wenyeji, yaani "Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan" na "Vuguvugu la Haki na Usawa" yalianza kupinga serikali na kutaka seehmu ya Darfur ijitawale na kuanzisha nchi mpya. Kutokana na usuluhishi wa jumuyia ya kimataifa, serikali ya Sudan na makundi hayo mawili yamewahi kufanya maduru matano ya mazungumzo, lakini hayakupata mafanikio yoyote kuhusu kumaliza mgogoro. Mazungumzo ya duru la sita yalianza tarehe 15 mwezi uliopita, hivi sasa mazungumzo yamekuwa katika kipindi muhimu kuhusu ugawaji wa raslimali na usalama.
Ni wazi kwamba lengo la makundi yanayopinga serikali kuzusha matukio ni kuishinikiza serikali ya Sudan ili yajipatie maslahi makubwa zaidi katika mazungumzo. Na kuhusu vikundi vyenye silaha kushiriki katika utekaji nyara wa askari wa Umoja wa Afrika, ofisa wa serikali ya Sudan alisema, lengo lao ni kujulisha pande mbalimbali kuwa vinataka pia nafasi katika madaraka ya taifa.
Wachambuzi wanaona kuwa matukio yaliyotokea hivi karibuni ya utekaji nyara yameletea wingu jeusi kwenye mazungumzo ya amani ya sehemu ya Darfur yanayoendelea sasa, lakini huku kwa upande mwingine mazungumzo hayo yameanza kuelekea kwenye makubaliano. Mwezi Januari mwaka huu rais wa Sudan na mwenyekiti wa Vuguvugu la Ukombozi wa Watu wa Sudan (Sudan People's Liberation Movement) walisaini makubaliano ya amani na kumaliza vita vilivyodumu kwa miaka 21 kusini mwa Sudan. Mwezi Septemba serikali mpya ya umoja wa kitaifa iliapishwa, na mazingira ya mazungumzo ya amani nchini Sudan yakawa mazuri zaidi. Kwa hiyo Ingawa mzungumzo ya amani ya Darfur yanakabiliana na changamoto, lakini watu hawajafa moyo na kutumai kuwa mazungumzo yangeleta ufumbuzi wa tatizo la Darfur lililokuwa likisumbua watu kwa muda mrefu.
Idhaa ya kiswahili 2005-10-11
|