Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-12 20:28:46    
Kwanini Bibi Rice amefanya ziara ya Asia ya kati?

cri

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice tarehe 11 alifanya ziara ya siku 1 nchini Kyrgyzstan. Na pia atafanya ziara nchini Afghanistan, Kazakhstan na Tajikistan. Wachambuzi wanaona kuwa lengo la ziara ya Bibi Rice ni kuboresha uhusiano kati ya Marekani na nchi hizo, na kudumisha na kukuza athari yake katika sehemu hiyo.

Baada ya kusambaratika kwa Urusi ya zamani, ili kubana nafasi ya kimkakati ya Russia, na kudhoofisha athari yake katika shughuli za kimataifa na kikanda, Marekani ilianza kujipenyeza kwa nguvu kwenye sehemu nzima ya Jumuiya ya Madola Huru. Pamoja na kupanuka kwa vita nchini Afghanistan, Marekani ikitumia kisingizio cha kupambana na ugaidi imefaulu kutimiza lengo lake la kuweka askari kwenye sehemu hiyo muhimu ya kimkakati wa vita, ambayo iko kwenye ua wa nyuma wa Russia na kujaribu kudhibiti sehemu hiyo nzima.

Lakini nia yake hiyo ya Marekani kwenye Asia ya kati haikufanikiwa. Mapema mwaka huu wakati yalipotokea "mapinduzi ya rangi" nchini Kyrgyzstan, ingawa mapinduzi hayo yalifanikiwa lakini rangi yake bado haijadhihirika wazi. Serikali mpya ya Kyrgyzstan haikubadilisha sera za utawala wa zamani wa kutopendelea upande wowote kati ya Russia na Marekani. Zaidi ya hayo, baada ya "mapinduzi ya rangi" nchini Kyrgyzstan na kutulia kwa ghasia ya Andijan nchini Uzbekistan, Kazakhstan na Uzbekistan ziliacha matarajio yao kuhusu Marekani na sera zao za kubadilikabadilika kati ya Russia na Marekani.

Wachunguzi wanaona kuwa hali ya hivi sasa inaonesha kuwa ikiwa tunasema Marekani imeitangulia jumuiya ya madola huru katika ushindani wao kwenye sehemu ya Ulaya na sehemu nyingine za karibu, basi imekuwa nyuma kwa muda katika ushindani kati yake na Russia kwenye sehemu ya Asia ya kati.

Mapinduzi ya Kyrgyzstan haijabadilisha hali yake ya kuitegemea sana Russia katika mambo ya siasa na uchumi, kuondokana na Russia ambayo ni jirani yake muhimu kwa kiongozi yeyote yule ni kama kuharibu mustakabali wa nchi. Licha ya hayo, mapinduzi ya Kyrgyzstan yametoa onyo kali kwa nchi nyingine za Uzbekistan na Kazakhstan na kuimarisha chaguo la nchi hizo, mambo hayo yamezifanya nchi hizo kuwa mbali zaidi na Marekani na kuwa karibu zaidi na Russia. Si siku nyingi zilizopita, Uzbekistan iliweka siku ya mwisho kwa Marekani kuondoka kutoka kwenye kituo cha kijeshi nchini Uzbekistan, ambapo uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikuwa wa kiwango cha chini kabisa. Kinyume na hayo ni kuwa hivi karibuni kwenye mkutano wa wakuu wa nchi ulioandaliwa na jumuiya ya ushirikiano ya nchi za Asia za kati na kufanyika mjini St. Petersburg, viongozi wa nchi mbalimbali wa sehemu hiyo walikuwa na maoni na uhamasa wa namna moja na kusisitiza kuimarisha uhusiano wa kirafiki pamoja na Russia.

Kutokana na kukabiliwa na hali ya maendeleo ya namna hiyo kwa sehemu ya Asia ya kati, Marekani ina wasiwasi mkubwa lakini haina mbinu ya kuibadilisha hali hiyo. Hivyo Marekani haina budi kulegeza msimamo wake na kubadilisha mbinu ili kupunguza hali ya wasiwasi kati yake na Russia na baadhi ya nchi za Asia ya kati na kujitahidi kuhifadhi maslahi yake kwenye sehemu hiyo. Wachambuzi wanasema kuwa hilo ni lengo la msingi la ziara ya Bibi Rice.

Katika wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Sergey Lavrov anayefanya ziara nchini Lebanon, siku hiyo alisema kuwa hakuna mgogoro kati ya Marekani na Russia katika sehemu hiyo. Alidokeza kuwa kabla ya kutembelea Asia ya kati, Bibi Rice alizungumza naye kwa simu akisema kuwa, Russia na nchi wenzake wa magharibi zinatambua maslahi ya nchi nyingine kwenye sehemu ya Asia ya kati. Lakini anatarajia kuwa vitendo vya nchi za magharibi vya kujitafutia maslahi vingekuwa wazi, na atafanya ziara katika sehemu ya Asia ya kati katika nusu ya pili ya mwezi huu.

Wachambuzi wanasema kuwa Marekani na Russia kulegeza misimamo yao kuhusu suala la Asia ya kati ni sera zao za muda, wala siyo suluhisho au urafiki wa kwenda wa pande hizo mbili. Katika siku za mbele, sehemu ya Asia ya kati itakuwa sehemu muhimu inayogombewa na nchi hizo mbili.

Idhaa ya Kiswahili 2005-10-12