Upigaji kura ulifanyika tarehe 11 katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Liberia. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kufanya uchaguzi mkuu baada ya kukomeshwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 14 mwezi Agosti mwaka 2003. Vyombo vya habari vinaona kuwa uchaguzi huo umeonesha kuwa hatua nyingine kubwa ya kihistoria imepigwa katika mchakato wa amani ya Liberia, ambayo ina umuhimu mkubwa katika kutimiza amani na utulivu kwa pande zote.
Ofisa wa tume ya uchaguzi ya nchi nzima ya Liberia alifahamisha kuwa, wapiga kura zaidi ya milioni moja waliojiandikisha siku hiyo walipiga kura kwenye vituo zaidi ya 3000 kote nchini. Chini ya usimamizi wa wachunguzi wa kimataifa na ulinzi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini humo, upigaji kura ulifanyika katika hali yenye utaratibu, hakutokea matukio yoyote ya kimabavu. Baada ya kumalizika kwa upigaji kura, kazi ya kuhesabu kura ikaanzishwa mara moja. Habari zinasema kuwa, matokeo rasmi ya uchaguzi huo yatajulikana ndani ya wiki mbili.
Wagombea 22 akiwemo "Bwana soko bora duniani" wa Mwaka 1995 George Weah walishiriki kugombea nafasi ya rais na umakamu wa rais. Aidha wajumbe zaidi ya 700 walioteuliwa na makundi mbalimbali ya kisiasa ya Liberia watagombea viti 94 kwenye baraza la juu na baraza la chini la bunge la Liberia. Kutokana na sheria ya uchaguzi ya Liberia, kama wagombea wa rais hawataweza kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa, basi wagombea wawili watakaopata kura nyingi zaidi wataingia duru la pili la upigaji kura.
Wachambuzi wanaona kuwa, kutokana na wagombea wengi kugombea nafasi ya urais kwenye uchaguzi huo, katika duru la kwanza la uchaguzi, huenda hakuna mgombea yeyote atakayepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa. Lakini hivi sasa Bwana Weah anayeungwa mkono na watu wengi zaidi nchini humo na mgombea mwingine ambaye alikuwa waziri wa fedha Bibi Ellen Johnson Sirleaf huenda watapata kura nyingi zaidi kuliko wengine katika duru la kwanza la upigaji kura na kuingia kwenye duru la pili.
Mwezi Desemba mwaka 1989, vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka nchini Liberia, vita hivyo vilidumu kwa miaka 14 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya laki 2, ambapo raia wengi walipoteza makazo yao na uchumi wa nchi hiyo ulikaribika na nchi kufilisika. Mwezi Agosti mwaka 2003, rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor alilazimika kujiuzulu, na kukimbia Nigeria, na vita vya wenyewe kwa wenyewe vikakomeshwa rasmi, makundi mbalimbali ya kisiasa yalisaini makubaliano ya amani na kuanzisha serikali na bunge la mpito, na kuamua kufanya uchaguzi mkuu mwezi Novemba mwaka huu.
Wachambuzi wanaona kuwa, hali ya Liberia inayoelekea kuwa tulivu baada ya vita, na uchaguzi wa kwanza nchini humo umehimizwa na sababu mbalimbali nchini Liberia.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyofanyika kwa miaka mingi vimewaletea balaa kubwa wananchi wa Liberia, makundi mbalimbali ya kisiasa yametambua siku hadi siku umuhimu wa kufufua amani ya nchini humo. Makundi mbalimbali yamefanya juhudi za kutekeleza makubaliano ya amani, kunyang'anya silaha na kusaidia kutuliza hali ya mambo baada ya vita, hivyo hali ya mambo nchini Liberia ikatulia siku hadi siku na kuweka mazingira ya lazima kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
Wachambuzi wanaeleza pia kuwa, uchaguzi mkuu wa kwanza ni hatua moja tu katika mchakato wa amani ya nchi hiyo, mgombea yoyote atakayeshinda katika uchaguzi huo atakabiliwa na changamoto nyingine. Lakini watu wana matumaini na imani kuwa, kutokana na maendeleo ya mchakato wa amani na ukarabati wa nchi hiyo, wananchi wa Liberia hakika watashinda taabu mbalimbali na kufanya juhudi katika kulinda amani, utulivu na maendeleo ya uchumi wa nchi hiyo.
Idhaa ya Kiswahili 2005-10-12
|