Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-12 22:07:23    
Mashirika mengi ya Xinjiang yaendelea kwa kasi kutokana na kutilia maanani katika uvumbuzi wa teknolojia

cri
Mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uyghur uko kaskazini magharibi mwa China. Katika muda mrefu uliopita, kutokana na sehemu hiyo kuwa nyuma katika upashanaji wa habari na teknolojia za kuzalisha bidhaa za hatua ya mwanzo, mashirika mengi ya huko yanazalisha bidhaa kwa hatua ya mwanzo tu, kwa hivyo bidhaa zao hazina ushindani mkubwa sokoni. Lakini mwandishi wetu wa habari hivi karibuni ameona kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, mashirika mengi ya huko yameendelea kwa kasi kutokana na kutilia maanani uvumbuzi wa teknolojia, na bidhaa za mashirika hayo zimekuwa na uwezo mkubwa wa ushindani mkubwa katika soko la nchini China na hata soko la kimataifa.

Kiwanda cha ya zana za umeme cha Tebian cha mkoani Xinjiang ni moja ya viwanda vya huko. Mwaka jana, mapato ya kiwanda hicho yalizidi yuan bilioni 5. lakini ni ajabu kwa kiwanda hicho kikubwa kinachotengenza zana nyingi zaidi za kubadilisha nguvu ya umeme nchini China kuendelea na kufikia hatua hiyo kutoka kampuni ndogo iliyokaribia kufilisika. Mkuu wa bodi ya kiwanda hicho Bw. Zhang Xin alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kiwanda hicho kinatokana na kampuni ndogo ya kuzalisha zana za kubadilisha nguvu ya umeme iliyokuwa na pato lisilozidi yuan laki mbili lakini deni lake lilizidi yuan laki saba. Bw. Zhang Xin alisema kuwa, ili kuondokana na hali ngumu ya kiuchumi, kiwanda hicho kiliweka ilitoa kipaumbele katika uvumbuzi wa teknolojia na kuongeza nguvu ya ushindani wa bidhaa kwenye soko. Alisema:

"zamani, bei ya zana ndogo za kubadilisha nguvu ya umeme zilizozalishwa na kiwanda chetu ilikuwa yuan 15 tu, lakini hivi sasa, bei ya zana hizo za kisasa imefikia dola za kimarekani milioni 5. zana hizo zinatumika katika miradi muhimu ya taifa. sasa bidhaa zetu zinachukua asilimia 20 sokoni, na kuchukua nafasi ya kwanza miongoni mwa viwanda vya sekta hiyo kote nchini China."

Bw. Zhang Xin alieleza kuwa, bidhaa zinazotengenezwa na kiwanda hicho zinatumika katika miradi muhimu ya nchini na ya nchi za nje, ikiwemo mradi wa magenge matatu, mradi wa ujenzi wa majumba na viwanja vya michezo ya Olimpiki ya Beijing, mradi wa kurusha chombo cha safari za anga ya juu cha "Shenzhou No. 5" na mradi wa kurekebisha mtandao wa umeme wa sehemu ya Magharibi ya Marekani. Bidhaa za kiwanda hicho zinauzwa katika nchi na sehemu zaidi ya 60 duniani. Hivi sasa kiwanda hicho kimebadilika na kuwa kiwanda kikubwa chenye wafanyakazi zaidi ya elfu 10, na thamani ya jumla ya mali zaidi ya yuan bilioni 8.

Ingawa mafanikio hayo makubwa yamepatikana, lakini maneja wa kiwanda hicho bado hajaridhika. Bw. Zhang Xin alisema kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, kiwanda hicho kimewekweza zaidi katika utafiti wa teknolojia mpya.

"mwaka jana, fedha zilizotumika katika utafiti wa teknolojia zilichukua asilimia 4.7 ya mapato ya jumla, na zilizidi yuan milioni 300, na bajeti yetu kwa mwaka huu ni asilimia 5. kutokana na uwekezaji huo, kila mwaka kiwanda chetu kinapata aina 100 za tekenolojia zenye hakimiliki, ambazo idadi hiyo inachukua nafasi ya kwanza katika sekta hiyo."

Katika miaka ya karibuni, pia kiwanda hicho kimewaingiza wataalamu wa nchini na kutoka nchi za nje na kushirikiana na taasisi mbalimbali za utafiti, ili kuinua zaidi kiwango cha utafiti wa teknoloijia.

Mbali na kiwanda hicho viwanda vingine vingi pia vimenufaika na uvumbuzi wa teknolojia, na kiwanda cha Zhonghe ya Xinjiang ni moja kati ya viwanda hivyo. Kiwanda hicho kinachozalisha bidhaa za aluminium kina historia ya zaidi ya miaka 50. katibu wa bodi ya maneja ya kiwanda hicho Bw. Yang Bo alisema kuwa, kutokana na kiwango cha chini cha teknolojia, zamani kiwanda hicho kiliweza kutengeneza bidhaa za kawaida za aluminium, kwa kutumia nishati nyingi na kutoa uchafuzi mwingi kwa mazingira. Lakini katika miaka kadhaa iliyopita, kiwanda hicho kimeinua sana kiwango cha teknolojia kutokana na utafiti na uvumbuzi wa teknolojia, hivi sasa kinazalisha tu bidhaa za hali ya juu za aluminium zenye thamani kubwa. Kutokana na uvumbuzi wa teknolojia, hivi sasa kiasi cha nishati kinachohitajika kuzalisha tani moja ya aluminium ya hali ya juu katika kiwanda hicho kimepungua kwa nyuzi 4000 za umeme, kiasi ambacho ni cha juu kabisa katika sekta hiyo. Bw. Yang Bo alieleza kuwa, uvumbuzi wa teknolojia umeongeza nguvu ya ushindani ya kiwanda, na kuhimiza kiwango cha ufundi wa uzalishaji na sifa ya bidhaa za kiwanda hicho zifikie kiwango cha kimataifa. Alisema:

"hivi sasa, bidhaa zetu za aluminium ya hali ya juu zinachukua zaidi ya asilimia 80 kwenye soko la nchini. Kuanzia mwaka 2004, bidhaa zetu zilianza kuuzwa Japan na nchi nyingine za Asia ya Kusini Mashariki."

Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hivi sasa, kiwanda hicho kimekuwa kituo kikubwa kabisa cha kuzalisha aluminium ya hali ya juu nchini China, na pato la jumla kwa mwaka jana lilikuwa zaidi ya yuan milioni 550. alisema kuwa, kampuni hiyo itaweka mkazo katika kuzalisha aluminium ya hali ya juu zaidi katika siku za baadaye.

Ikilinganishwa na viwanda hivyo viwili, kampuni ya nishati mpya ya Xinjiang ilianzishwa kwa muda mfupi zaidi, miaka 5 tu. lakini kwa kutegemea uwezo mkubwa wa utafiti wa teknolojia, kiwanda hicho kinachotengeneza mitambo ya kuzalisha umeme kwa nishati ya jua kilianza kuendelea kwa kasi baada ya miaka miwili tu. mwaka 2002, ili kutatua suala la matumizi ya umeme kwemye vijiji vya mbali, serikali ya China ilianzisha mradi wa kupeleka umeme vijijini, na kutumia fedha nyingi kujenga vituo vya kuzalisha umeme kwa nishati ya jua kwenye vijiji visivyo na umeme. Msaidizi wa Maneja mkuu wa kiwanda hicho Bw. Huang Xindong alisema,

"wakati mradi wa kupeleka umeme vijijini ulipoanzishwa, kutokana na kuwa kiwanda chetu kilifanya utafiti kuhusu teknolojia muhimu za kuzalisha umeme kwa nishati ya jua katika kipindi cha mwanzo, hivyo tuligombea zabuni na kupata asilimia 40 ya ujenzi wa mradi huo, ambayo ilikuwa kiasi kubwa kabisa kuliko hicho cha makampuni mengine 50."

Bw. Huang Xindong alieleza kuwa, hivi sasa kiwanda hicho kimekamilisha miradi yote iliyofanya, ambayo inaenea kwenye vijiji zaidi ya 200 katika mikoa mingi ikiwemo Xinjiang na Sichuan. Suala la umwagiliaji maji mashambani na matumizi ya umeme kwa wafugaji na wakulima wa vijiji hivyo limetatuliwa. Aidha, mitambo ya nishati ya jua iliyotengenezwa na kiwanda hicho inatumika kwenye miradi mingi mikubwa ya ujenzi nchini China, ikiwemo reli ya Qinghai - Tibet, na mitambo ya kiwanda hicho pia imeuzwa kwa nchi nyingi. mwaka jana, pato la jumla la kiwanda hicho lilizidi yuan milioni 200, likiwa limeongezeka mara 20 kuliko pato la miaka ya mwanzo.

Bw. Huang Xindong alisema kuwa, hivi sasa kiwanda hicho kimekuwa kiwanda kikubwa kabisa cha teknolojia mpya za hali ya juu katika sekta ya kuendeleza na kutumia nishati ya jua. Ili kuimarisha zaidi uwezo wa uvumbuzi wa teknolojia, hivi sasa kiwanda hicho kinatumia robo ya pato la jumla katika utafiti wa teknolojia mpya.

Takwimu husika zinaonesha kuwa, katika miaka mitano ya karibuni, mashirika makubwa na ya wastani ya mkoa wa Xinjiang yametumia zaidi ya yuan bilioni 50 katika kuvumbua na kurekebisha teknolojia. Hivi sasa mashirika mengi zaidi ya mkoa huo yanaendelea kwa kasi kwa kutegemea uvumbuzi wa teknolojia.

Idhaa ya Kiswahili 2005-10-12