
Waziri wa mambo ya ndani wa Syria Bw. Ghazi Kanaan tarehe 12 alijiua ofisini kwake. Vyombo vya habari vya serikali ya Syria vimetangaza kuwa katika siku hiyo Bw. Kanaan alijiua ofisini kwake kwa bastola, na havikueleza zaidi. Muda mfupi baadaye serikali ya Syria ilitoa taarifa na kuonesha maombolezo kwa kifo cha Bw. Kanaan, na kusema kwamba imeagiza idara husika kufanya uchunguzi.
Waziri huyo mwenye umri wa miaka 63 ni ofisa wa pili wa ngazi ya juu aliyejiua baada ya waziri mkuu wa zamani wa Syria kujiua miaka 10 iliyopita kutokana na kuhusika na ufisadi. Bw. Kanaan alihitimu katika chuo kikuu cha kijeshi mwaka 1965 na kushughulika katika idara ya upelelezi kwa muda wa miaka 20, bali hakuwahi kuwa na wadhifa katika baraza la serikali, kwa hiyo yeye alikuwa ni mtu mwenye athari kubwa katika mambo ya siasa nchini Syria.
Habari ya kujiua kwa Bw. Kanaan imekuja ghafla, lakini yeye mwenyewe alionekana kama alikuwa amejiandaa mapema. Katika asubuhi ya siku ya kujiua kwake Bw. Kanaan aliomba kuhojiwa na waandishi wa habari wa redio ya "Sauti ya Syria" na kutoa maoni kuhusu kuwa shahidi wa tukio la Rafik al-Hariri kwa tume ya uchunguzi wa kimataifa. Katika mahojiano na waandishi wa habari Bw. Kanaan alieleza kirefu uhusiano mzuri kati ya Syria na Lebanon katika miaka kumi kadhaa na kusisitiza kuwa ametoa mchango mkubwa usiofutika katika juhudi za kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, kurudisha hali ya utulivu nchini Lebanon na kusaidia kukomboa ardhi iliyokaliwa ya Lebanon, na kukanusha habari nyingi zisizo za kweli kuhusu uhusiano mbaya baada ya kuuawa kwa Hariri mwezi Februari mwaka huu na shutuma nyingi kwake. Kwa kumaliza mahojiano alisema, "Pengine hii ni mara yangu ya mwisho kuhojiana na waandishi wa habari" na kuomba mazungumzo yake yapelekwe kwenye vituo vingine vya televisheni.
Serikali ya Syria haijatangaza habari yoyote kuhusu sababu ya kujiua kwa Bw. Kanaan. Hata hivyo, vyombo vya habari vinaona kwa kuwa sababu Bw. Kanaan alikuwa mkuu wa idara ya upelelezi wa kijeshi nchini Lebanon katika miaka ya 80 na 90, alikuwa ni mtu mzito wa Syria nchini Lebanon, kwa hiyo kifo chake hakitengani na kifo cha Hariri.
Ingawa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Bw. Hariri alipouawa mwezi Februari mwaka huu Bw. Kanaan alikuwa nchini Syria, lakini kifo cha waziri mkuu huyo kilikuwa kimebadilisha maisha ya kisiasa ya Bw. Kanaan. Licha ya kundi la Lebanon linaloipinga Syria kumshutumu kuhusika na kifo cha Hariri, tume ya uchunguzi wa kimataifa ya kifo cha Hariri pia ilifika nchini Syria kuwahoji watu husika akiwemo Bw. Kanaan, ingawa tume hiyo haikumshutumu lakini maofisa wanne walishikiliwa na idara za sheria za Lebanon wana uhusiano wa karibu na Kanaan. Tume ya uchunguzi wa kimataifa kuhusu kifo cha Hariri siku chache baadaye itatoa ripoti kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu uchunguzi wake. Hili ni shinikizo kubwa kwa Bw. Kanaan.
Syria siku zote inashikilia kutohusika na kifo cha Hariri. Rais Bashar al-Assad wa Syria baada ya kujiua kwa Kanaan, tarehe 12 alisisitiza kuwa Syria haina uhusiano wowote na kifo cha Hariri. Lakini alipohojiwa na waandishi wa habari kwamba pengine kuna maofisa fulani walioshiriki katika njama ya kumwua Hariri bila yeye kufahamu, Bw. Bashar alisema kama tume ya uchunguzi wa kimataifa imethibitisha kwamba watu fulani wameshiriki katika mauaji ya Hariri, basi watu hao watakuwa wahaini na wataadhibiwa kisheria. Wachambuzi wanaona kuwa tukio la kuuawa kwa Bw. Hariri lilimaanisha mwisho wa maisha ya siasa ya Kanaan.
Idhaa ya kiswahili 2005-10-13
|