Tarehe 11 mwezi huu, uchaguzi wa kwanza wa rais nchini Liberia ulifanyika tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipomalizika mwaka 2003 nchini humo. Hadi hivi sasa, kazi ya kuhesabu kura bado inaendelea. Matokeo ya mwanzo yaliyotolewa tarehe 13 yanaonesha kuwa Bw. George Weah, aliyeteuliwa kuwa mwanasoka bora duniani mwaka 1995 na Bi. Johnson Sirleaf, waziri wa zamani wa fedha wanaongoza katika upigaji kura.
Wachambuzi wanaona kuwa kutokana na idadi kubwa ya wagombea urais, hali ya kutokuwa na mgombea atakayepata zaidi ya nusu ya kura za raia huenda itaonekana katika duru ya kwanza ya upigaji kura. Kwa mujibu wa kanuni husika za sheria ya uchaguzi ya Liberia, kama hali hiyo itatokea, wagombea wawili waliopata kura nyingi zaidi watashiriki kwenye duru ya pili ya upigaji kura. Hivyo George Weah na Bi Johnson wataendelea kupambana baadaye.
Uchaguzi mkuu wa Liberia una sehemu mbili za uchaguzi wa urais na uchaguzi wa bunge. Watu 22 akiwemo Weah wanagombea madaraka ya urais na makamu wa urais na wajumbe zaidi ya 700 kutoka vyama mbalimbali watagombea viti 94 kwenye mabaraza mawili ya bunge.
Mchazaji nyota wa zamani George Weah mwenye umri wa miaka 39 anapendwa na wapiga kura wengi hasa vijana kutokana na ustadi wake wa kucheza soka na kufanya hisani kwa watu maskini. Uchambuzi unaona kuwa kwa kuwa idadi ya wapiga kura vijana inachukua asimilia 23 ya idadi nzima ya wapiga kura, jambo ambalo litampatia nafasi kubwa zaidi ya ushindi. Wakati huo huo, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 14, wapiga kura wanataka kumchagua kiongozi asiyekuwa na uhusiano na serikali ya zamani. Bw. Weah akiwa mwanasoka hakuwahi kuingia kwenye uwanja wa kisiasa ambapo hilo limekuwa sharti la kumsaidia Weah awavutie wapiga kura. Lakini anakosa uzoefu wa kisiasa wa lazima kwa kiongozi wa taifa. Zaidi ya hayo, elimu yake ndogo pia ni udhaifu wake.
Ikilinganishwa na George Weah, Bi. Johnson Sirleaf mwenye umri wa miaka 66 ana uzoefu mkubwa wa kisiasa na kiwango cha juu cha elimu. Vyombo vya habari vinaona kuwa uzoefu wake wa kufanya kazi katika benki ya dunia utamsaidia kuiongoza Liberia ifanye ukarabati baada ya vita na kufufua uchumi wa taifa uliodidimia kwa miaka mingi. Kama Bi. Johnson Sirleaf atashinda katika uchaguzi mkuu, atakuwa rais mwanamke wa kwanza aliyechaguliwa na wananchi barani Afrika. Mambo ambayo hayamsaidii ni hali ya kuwa ofisa wa zamani wa serikali na umri mkubwa.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi mkuu ya Liberia Bi. Johnson Morris alieleza kuwa kati ya wapiga kura zaidi ya milioni 1.3 kote nchini humo, zaidi ya asilimia 70 ya wapiga kura walishiriki kwenye upigaji kura. Habari zinasema kuwa ili kuwarahisishia wapige kura, tume hiyo imefungua vituo zaidi ya 3000 katika sehemu mbalimbali nchini humo, lakini hali duni ya mawasiliano, upashanaji habari na miundo mbinu imeleta matatizo kwenye kazi ya kusafirisha masunduku na kuhesabu kura. Lakini ofisa wa Liberia alieleza kuwa kutokana na msaada wa kikundi cha kulinda amani cha Liberia cha Umoja wa Mataifa na jumuiya kadhaa za kimataifa, kazi ya kuhesabu kura inaendelea bila matatizo na matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yatatangazwa hadharani baada ya siku tatu hadi siku saba.
Jumuiya za kimataifa imetoa msaada mikubwa kwa uchaguzi wa Liberia. Wakaguzi zaidi ya 400 kutoka pande mbalimbali duniani wameshiriki kwenye mchakato wa uchaguzi huo. Hivyo, uchaguzi huo umefanyika kwa uwazi na haki.
Wakati huo huo, raia wa Liberia walioteseka kwenye vita hivyo wamejaa matarajio makubwa ya amani na utulivu nchini humo na kuonesha uchangamfu na busara kubwa katika uchaguzi huo.
Idhaa ya kiswahili 2005-10-14
|