Tarehe 16 ni siku ya chakula duniani. Katika siku hiyo, nchi na sehemu 150 duniani zilifanya sherehe mbalimbali kuadhimisha siku hiyo, ili kuhimiza binadamu kupambana na njaa.
Kauli mbiu ya siku ya chakula ya mwaka huu ni "majadiliano ya kilimo kati ya nchi zenye tofauti ya utamaduni: Mali yetu ya urithi pamoja". Katibu mkuu wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO Bw. Jacques Diouf alitoa hotuba tarehe 16 kwenye makao makuu ya shirika hilo mjini Rome akiainisha kuwa, utamaduni tofauti umetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya kilimo duniani na jumuiya ya kimataifa inapaswa kuimarisha maingiliano ya utamaduni katika eneo la kilimo na kutimiza lengo la mwisho la kupambana na njaa na kutokomeza umaskini. Alisema kuwa kufanya mazungumzo ya kweli kati ya nchi zenye tofauti ya utamaduni ni sharti la kwanza la kutatua masuala la umaskini na uchafuzi wa mazingira duniani. Alisisitiza pia kuwa, kuimarisha maingiliano na ushirikiano kati ya nchi zinazoendelea ni jambo muhimu zaidi na mazungumzo hayo ni njia muhimu ya kupaidika na uzoefu na teknolojia ya uzalishaji wa kilimo.
Wachambuzi wanaona kuwa wakati wa kuadhimisha siku hiyo, kwa nchi zinazokabiliwa na suala gumu la usalama wa chakula na kilimo, kuimarisha ushirikiano na mazungumzo kati ya kusini na kusini kuna maana halisi ya kutatua tatizo la njaa kwa binadamu.
Kwanza, maingiliano kati ya binadamu katika ustaarabu wa kilimo yalianza katika enzi ya kale. Katika historia ya binadamu, maingiliano ya utamaduni katika aina za mazao ya kilimo na mifugo yamefanya chakula cha binadamu kutokewa na mabadiliko makubwa na kupunguza umaskini. Mazao mengi yanayopandwa na kutumiwa barani Ulaya, kama vile viazi, nyanya na tumbaku yote yaliletwa na msafiri wa bahari Columbus kutoka barani Amerika. Matunda mengi ya barani Ulaya na Asia yalisafirishwa kwenda huko kwa kupitia njia ya hariri. Mahindi ni chakula muhimu barani Afrika ambayo yalitoka nchini Mexico. Ngano, zao muhimu la kilimo cha bara la Amerika Kaskazini ilitoka barani Ulaya kwa kuvuka bahari ya Atlantic. Kwa hiyo, ushirikiano na mazungumzo kati ya nchi mbalimbali zenye tofauti ya utamaduni yanawafanya watu warekebishe uzalishaji wa kilimo kwa ujuzi mpya na kuyawezesha mazao ya kilimo yazoee mazingira mapya ya kustawi, kukidhi ongezeko la mahitaji na kutoa mchango katika kutokomeza umaskini.
Pili, Tangu vita vya pili vya dunia vilipotokea, misaada iliyotolewa na nchi zilizoendelea imetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya kilimo ya nchi zinazoendelea, lakini masharti mbalimbali ya kutoa misaada hiyo ya nchi zilizoendelea yamezitia mizigo mikubwa nchi zinazoendelea. Ingawa ushirikiano kati ya kaskazini na kusini hakutakiwi kuachwa, lakini kikomo cha ushirikiano huo kimeonekana siku hadi siku. Kwa hiyo, kazi ya ushirikiano kati ya kusini na kusini haipaswi kupuuzwa kwenye suala la kutomeza njaa.
Tatu, ushirikiano kati ya kusini na kusini umeonekana kidhahiri. Miaka ya karibuni, ushirikiano huo umeendelea vizuri kwa kusaidiwa na FAO. Wataalamu wa China wamekwenda Ethiopia na Bangladesh kufanya kazi na wataalamu wa Bangladesh wamekwenda nchini Gambia kufanya kazi. Ushirikiano huo umezidisha maingiliano ya ujuzi na uzoefu kati ya nchi zinazoendelea katika maeneo ya kilimo, chakula, uvuvi na misitu.
Wachambuzi wanaona kuwa mwaka huu ni wa 25 kuadhimisha siku ya chakula duniani, lakini njaa bado ni adui mkubwa kabisa kwa maendeleo ya binadamu. Habari zinasema kuwa watu milioni 840 duniani bado wanakabiliwa na njaa. Katika nchi nyingi zinazoendelea, uzalishaji wa chakula haulingani na ongezeko la haraka la idadi ya watu. Nchi zinazoendelea zinapaswa kushirikiana katika kupambana na njaa, utapia mlo na umaskini.
Idhaa ya Kiswahili 2005-10-17
|