Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-18 20:45:21    
Uwekezaji wa vitega-uchumi wa China wapendwa na nchi za nje

cri

Kwenye mazungumzo ya uwekezaji wa vitega-uchumi na biashara yaliyofanyika nchini China, kuvutia wafanyabiashara wa nchi za nje kuwekeza nchini China kulikuwa moja ya shughuli muhimu. Lakini katika miaka ya karibuni, pamoja na kukuzwa kwa maendeleo ya uchumi na nguvu ya ushindani ya viwanda vya China, mwelekeo wa uwekezaji wa vitega-uchumi wa viwanda vya China katika nchi za nje umefuatiliwa na kampuni na mashirika ya kigeni yanayoshiriki kwenye mazungumzo ya biashara.

Kwenye mazungumzo ya uwekezaji na biashara yaliyofanyika hivi karibuni kwenye mji wa Xiamen ulioko pwani ya kusini mashariki ya China, shirika la maendeleo ya viwanda la Umoja wa Mataifa liliandaa miradi zaidi ya 350 ya uwekezaji wa vitega-uchumi katika nchi za Afrika kwa ajili ya viwanda vya China. Miradi hiyo inahusika na maeneo zaidi ya 10 yakiwemo ya usindikaji wa mazao ya kilimo, uzalishaji wa mitambo, biashara na mambo ya fedha ambavyo thamani ya uwekezaji inaanzia dola za kimarekani elfu makumi kadhaa hadi milioni makumi kadhaa.

Mbali na hayo, kwenye mazungumzo hayo ya uwekezaji na biashara, Marekani, Canada na Italia ziliandaa mkutano wa kutoa maelezo kuhusu mazingira ya uwekezaji na sera nafuu za nchi zake ili kuvutia uwekazaji kutoka China. Idara husika za Italia ziliwekeana saini na wizara ya biashara ya China kumbukumbu ya maelewano inayolenga kuhimiza kuwekeana vitega-uchumi kati ya nchi hizo mbili. Mkurugenzi wa ofisi ya mitaji ya kigeni ya idara ya uhimizaji wa uwekezaji vitega-uchumi ya Italia Bw. Giampaolo Russo alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, idara hiyo ya Italia imeamua kuchukulia China kuwa nchi ya kwanza isiyo ya Ulaya ya kutiliwa mkazo kuvutiwa katika uwekezaji wa vitega-uchumi. Alisema,

"Tunaona uchumi wa China umepata maendeleo ya kasi na kuwa moja ya nchi zenye uchumi imara duniani. Katika miaka mitatu iliyopita, China iliwekeza kwa wingi katika nchi za nje ambazo nyingi ni nchi za Asia za karibu, Amerika ya kaskazini na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya, lakini Italia ilipata kidogo tu, lengo la safari yetu ni kuvieleza viwanda vya China kuwa uwekezaji wao ungekuwa pamoja na nafasi inayotolewa na Italia."

Ni kama Bw. Giampaolo Russo alivyoeleza kuwa zana za utalii, sekta ya usambazaji wa bidhaa, teknolojia ya mawasiliano ya habari, sekta ya magari na sayansi ya uhai ni maeneo matano ya Italia yanayotarajia uwekezaji wa China. Alitoa mfano kuwa Italia ni nchi ya kwanza kwa wingi wa watu wenye simu za mkononi hapa duniani, hivyo nchi hiyo ni soko kubwa sana kwa viwanda vya zana za mawasiliano ya habari vya China. Idara ya kuhimiza uwekezaji ya Italia itatoa huduma za tathmini kuhusu miradi, uchaguzi wa mahali pa kujenga viwanda, uchunguzi wa mahali pa ujenzi na kuanzisha shughuli za biashara kwa ajili ya wawekezaji wa China.

Licha ya mkutano wa kutoa maelezo kuhusu sera za uwekezaji, Sweden, Poland na Ubelgiji zilifanya shughuli za siku za maonesho yao katika kipindi cha mazungumzo, ili kuwa na maingiliano na maelewano ya moja kwa moja na wafanyabiashara wa China. Mwakilishi wa kwanza wa idara ya kuhimiza uwekezaji ya Sweden aliyeko nchini China Bw. Chen Yonglan alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa katika miaka 5 iliyopita Sweden ilichukua nafasi ya 11 kwa wingi wa mitaji ya kigeni iliyovutiwa duniani ikiwa ni wastani wa dola za kimarekani bilioni zaidi ya 22 kwa mwaka. China ikiwa ni mwenzi wa pili wa Sweden katika shughuli za biashara barani Asia, imekuwa nchi muhimu inayowekeza nchini mwake, ambapo viwanda vya China vimepata maendeleo makubwa katika sekta za teknolojia, hoteli na uzalishaji wa bidhaa nchini Sweden. Anaona kuwa uwekezaji wa viwanda vya China ni chaguo la kunufaishana kati ya pande hizo mbili. Alisema,

"Kampuni za Huawei, Zhongxing na nyingine zilijiendeleza nchini Sweden, kutokana na ushirikiano na kampuni za huko kampuni za China zilipata uzoefu wa usimamizi na teknolojia ya kisasa, pia zinaweza kuzalisha bidhaa nzuri ambazo ni rahisi kuingia kwenye masoko ya nchi za Ulaya. Kwa upande mwingine, kampuni za Sweden zinazofanya ushirikiano na kampuni za China katika utafiti zinaweza kuingia kwa urahisi kwenye soko la China.

Wakati kampuni na mashirika ya nchi za nje yanapochunguza mwelekeo wa uwekezaji wa viwanda vya China katika nchi za nje, serikali ya China nayo inahimiza na kuunga mkono viwanda bora vya China kwenda kuwekeza katika nchi za nje. Takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, viwanda zaidi ya 5,100 vya China vimewekeza vitega-uchumi vya dola za kimarekani bilioni 44.8 katika nchi na sehemu 150 duniani. Habari zilizotangazwa na mkutano wa biashara na maendeleo wa Umoja wa Mataifa zinasema kuwa China inachukua nafasi ya 4 miongoni mwa wafanyabiashara wanaowekeza moja kwa moja katika nchi za nje. Pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji wa viwanda vya China katika nchi za nje, viwanda hivyo vimefahamu vyema masoko ya nchi za nje na kuwa na uzoefu mkubwa katika shughuli za uwekezaji wa vitega-uchumi. Mkurugenzi wa kamati ya uchumi ya mji wa Zoetermeer wa Uholanzi Bw. Hans Mayer alipozungumzia hali ya uwekezaji wa viwanda vya China nchini Uholanzi alisema,

"Viwanda vya China vilivyoko nchini Uholanzi vimekuwa na uzoefu mkubwa siku hadi siku katika mauzo ya sokoni, na vimejifunza mambo mengi katika uzoefu wa mauzo sokoni, hivi sasa ubora wa bidhaa zao unainuka kwa mfululizo na vimepata maendeleo makubwa."

Mratibu mkuu wa mkutano wa biashara na maendeleo wa Umoja wa Mataifa Bw. Supachai Panitchpakdi pia alipongeza hadharani kuhusu hamasa ya uwekezaji wa viwanda vya China katika nchi za nje. Alisema kuwa viwanda vya China vikiwa wawekezaji vinafanya kazi muhimu siku hadi siku kwa maendeleo ya uchumi wa dunia. Alisema,

"Ninaona kuwa China imeendelea kuwa nchi moja inayokwenda kuwekeza katika nchi za nje kutoka nchi iliyovutia wafanyabiashara wa kigeni kuwekeza nchini mwake, hii ni hali nzuri kabisa. Ninachukua mfano wa sekta ya nguo, si kama tu China inasafirisha bidhaa zake za nguo kwa nchi za jumuiya ya ushirikiano na maendeleo ya uchumi, bali pia imenuia kuwekeza katika sekta ya nguo ya nchi hizo, hivyo licha ya kuweza kuimarisha hadhi ya kuongoza ya viwanda vya China katika eneo hilo, tena inaweza kutoa misaada kwa maendeleo ya nchi maskini. Uwekezaji wa China katika sekta ya nishati ya nchi za nje pia unaleta manufaa kwa nchi nyingine."

Bw. Supachai Panitchpakdi alisema kuwa, kuwekeza moja kwa moja kumekuwa mtindo muhimu wa kushiriki kwa China katika ugawaji wa kazi na upangaji wa uzalishaji mali duniani. Uchunguzi wa mkutano wa biashara na maendeleo wa Umoja wa Mataifa unaonesha kuwa idara za kuhimiza uwekezaji za nchi nyingi zinaichukulia China kuwa nchi muhimu inayowekeza moja kwa moja katika nchi washiriki tokea mwaka 2005 hadi mwaka 2008.

Wizara ya biashara ya China ilisema kuwa, katika siku za baadaye itaendelea kuhimiza viwanda vya China kuimarisha ushirikiano na nchi za nje katika shughuli za kilimo, kuchukua kandarasi ya ujenzi wa miradi na kuhimiza ushirikiano na nchi za nje katika mambo ya sayansi, teknolojia na elimu na kuinua kiwango cha ushirikiano katika shughuli za nguvu-kazi na huduma za biashara.

Idhaa ya Kiswahili 2005-10-18