Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-19 15:24:02    
Iraq yaanza hukumu ya karne dhidi ya Saddam Hussein

cri

Mahakama maalum ya Iraq tarehe 19 huko Baghdad itamhukumu rais wa zamani wa Iraq Bwana Saddam Hussein na maafisa 7 waandamizi wa serikali ya zamani ya nchi hiyo pamoja na wanachama wa chama cha Baath. Mahakama hiyo itawahukumu rasmi Bw. Saddam Hussein na maofisa wengine 7 kwa hatia ya kupinga ubinadamu kwa kushiriki katika tukio la mauaji makubwa ya kijiji cha Dujail kilichoko kaskazini mwa Baghdad, tukio hilo lilitokea mwaka 1982 na kusababisha vifo vya watu 143. Kama hatia hiyo ikiweza kuthibitishwa Bw. Saddam na wengine 7 watahukumiwa adhabu ya kifo.

Kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kuwahukumu viongozi wa utawala wa zamani wa Iraq baada ya Marekani kuuangusha utawala huo kwa vita iliyoanzishwa mwaka 2003, na Bw. Saddam mwenyewe anachukuliwa kuwa alishika hatamu za serikali ya Iraq kwa miaka 23 kwa njia ya kidikteta, hivyo hukumu hiyo inachukuliwa kuwa ni hukumu ya karne nchini Iraq. Pia hukumu hiyo itawaoneshea wanamgambo wa Iraq wanaopinga Marekani na utawala wa sasa wa nchi hiyo wa madhehebu ya Sunni na mabaki ya nguvu za chama cha Baath kuwa, zama ya Saddam imekwisha, ili kusaidia kurudisha utulivu wa hali ya kisiasa ya Iraq.

Kutokana na msaada wa kifedha na kisheria wa Marekani, Mahakama maalum ya Iraq imefanya maandalizi ya makini kwa ajili ya hukumu hiyo. Majaji 5 wa Iraq walipewa mafunzo ya miezi 18 nchini Uingereza, mahakama hiyo imefanya uchunguzi na uthibitishaji wa makini kuhusu mashtaka husika dhidi ya Saddam, hatimaye imelifanya tukio la mauaji ya kijiji cha Dujail kama mashtaka ya kwanza dhidi ya Saddam. Jaji mkuu wa mahakama hiyo alisema kuwa, licha ya tukio la mauaji ya kijiji cha Dujail, Bw. Saddam pia atahukumiwa kuwa na hatia nyingine 12 za kivita, kupinga ubinadamu na kukiuka haki za binadamu. Mahakama maalum imedokeza kuwa, katika tukio la mauaji la kijiji cha Dujail, mahakama imekusanya mashtaka na mashahidi wa kutosha wa kumhukumu Bw. Saddam adhabu ya kifo.

Kuhusu hukumu hiyo, wakili mtetezi wa Saddam Bw. Khalil al-dulaimi aliainisha kuwa, mahakama maalum ya Iraq ilimkabidhi taarifa ya kusikiliza kesi kabla ya siku zaidi ya 20 tu badala ya siku 45, jambo hilo limeenda kinyume na utaratibu wa kisheria. Isitoshe, mahakama maalum ya Iraq iliundwa wakati nchi hiyo ilipokaliwa na jeshi la Marekani, ingawa iliidhinishwa kwenye bunge la mpito la Iraq mwezi Agosti mwaka huu, lakini sheria husika bado haijaanza kufanya kazi, hivyo kundi la mawakili wa utetezi wa Saddam linaweza kutia mashaka kuhusu hadhi na madaraka ya kisheria ya mahakama hiyo.

Tarehe 18 baada ya kukutana na Bw. Saddam kwa dakika 90, wakili al-Dulaimi alisema kuwa, hivi sasa Bw. Saddam anajisikia vizuri, akiona kuwa yeye hana hatia yoyote. Bw. Dulaimi alisema kuwa, ataiomba mahakama iahirishe kesi hiyo kwa miezi mitatu ili kujipatia muda mrefu zaidi wa kumtetea Saddam , na kuwaalika mawakili wa nchi za kiarabu na nchi za magharibi kujiunga na kundi la mawakili wa utetezi la Bw. Saddam.

Jumuiya ya kimataifa inafuatilia sana mahakama maalum ya Iraq iliyoelekezwa na kusaidiwa na Marekani itaweza au la kufuata kanuni za kimsingi za sheria ya kimataifa katika hukumu hiyo. Mshauri wa kisheria wa kikundi cha mawakili wa utetezi wa Saddam, waziri wa zamani wa sheria wa Marekani alisema kuwa, baadhi ya haki za kimsingi za Bw. Saddam zimekiukwa baada ya Saddam kukamatwa. Jumuiya kadhaa za haki za binadamu duniani zimeona kuwa, katika hali ya hivi sasa, ambayo sheria ya Iraq bado haijakamilika, mchakato wa kisheria wa kumhukumu Saddam na wengineo bila shaka utakwenda kinyume na vigezo vya kimsingi vya sheria ya kimataifa.

Wachambuzi wanaona kuwa, kwa vyovyote hukumu hiyo itakuwa alama muhimu katika mchakato wa maendeleo ya kisiasa ya Iraq.

Idhaa ya Kiswahili 2005-10-19