Mahakama maalum ya Iraq tarehe 19 itawasomea mashitaka rais wa zamani wa Iraq na wasaidizi wake saba wakubwa katika "sehemu ya kijani" mjini Baghdad kwa hatia ya kupinga ubinadamu ambayo walishiriki kwenye mauaji yaliyotokea mwaka 1982 katika kijiji cha Dujail walikoishi Waislam wa madhehebu ya Shia, kaskazini mwa Baghdad na kusababisha vifo vya watu 143.
Mshitakiwa wa kwanza ni rais wa zamani wa Iraq Saddam Hussein.Alizaliwa mwaka 1937 mjini Tikrit, katikati ya Iraq. Alishiriki kwenye kampeni za kisiasa alipokuwa na umri wa miaka 18. Alijiunga na chama cha Baath alipokuwa na umri wa miaka 20 na kuingia kwenye kikundi cha uongozi hatua kwa hatua. Mwaka 1968 alichaguliwa kuwa makamu wa mwenyekiti wa kamati ya mapinduzi ya uongozi wa Iraq na kuwa mtu wa pili kwenye ngazi ya madaraka nchini Iraq. Kuanzia mwaka 1979 alikuwa rais wa Iraq, mwenyekiti wa kamati ya mapinduzi, waziri mkuu na katibu mkuu wa chama cha Baath na kuhodhi madaraka makubwa yote ya chama, serikali na jeshi.
Marekani iliwahi kuwa rafiki mkubwa wa serikali ya Saddam. Katika vita vilivyotokea kati ya Iraq na Iran miaka ya 80 karne iliyopita, Marekani iliipatia Iraq misaada mikubwa ya silaha na fedha. Lakini baada ya mwaka 1990, Saddam aliamuru jeshi lake kuishambulia Kuwait, jeshi la nchi nyingi lililoongozwa na Marekani lililifukuza jeshi la Iraq kutoka nchini Kuwait. Mwaka 2003, Marekani ilianzisha vita vya Iraq na kuipindua serikali ya Saddam mwezi Aprili mwaka huo kwa kisingizio cha kukataa kutekeleza maazimio husika ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na kutengeneza na kuficha idadi kubwa ya silaha kali za maangamizi. Mwezi Desemba mwaka huo, Saddam alikamatwa na jeshi la Marekani mjini Tikrit, kwenye maskani ya Saddam na kutiwa nguvuni hadi leo.
Habari zinasema kuwa mbali na kushitakiwa kwa hatia ya kushiriki kwenye mauaji yaliyotokea katika kijiji cha Dujail, Saddam pia atashitakiwa kwa hatia za vita, kupinga ubinadamu na kukiuka haki za binadamu. Kama hatia ya kwanza itathibitishwa, Saddam atahukumiwa kifo.
Mshitakiwa wa pili ni makamu wa rais wa Iraq Taha Uassin Ramadan. Alizaliwa mwaka 1938. Alifahamiana na Saddam baada ya kujiunga na chama cha Baath, katikati ya miaka 50 ya karne iliyopita na alikuwa mtu mwenye madaraka makubwa katika kikundi cha uongozi cha serikali ya Saddam. Bw Ramadan atashitakiwa kwa hatia ya kushiriki kwenye mauaji yaliyotokea katika kijiji cha Dujail na makosa mengine.
Mshitakiwa wa tatu ni jamaa ya Saddam ambaye pia alikuwa mshauri wake Barzan Ibrahim Al-Tikriti.
Mshitakiwa wa nne ni jaji mkuu wa mahakama ya kimapinduzi ya serikali ya Saddam Awad Hamed Al-Bander.
Washitakiwa wengine wote ni maofisa wa tawi la kijiji cha Dujail la chama cha Baath cha Iraq.
Habari zinasema kuwa baada ya kuwasomea mashitaka tarehe 19, mahakama itasimamisha kesi hiyo kwa wiki kadhaa na kuchagua siku kuendelea tena na kesi hiyo.
Idhaa ya Kiswahili 2005-10-19
|