Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-20 16:53:03    
Uokoaji wa maafa ya tetemeko la ardhi nchini Pakistan wakabiliwa na matatizo makubwa

cri

Rais Pervez Musharraf wa Pakistan tarehe 19 baada ya kukagua sehemu ya Barakot iliyoathirika vibaya na tetemeko la ardhi, alisema kuwa hivi sasa kuwapatia waathirika mahali pa kukaa ni kazi muhimu na ya haraka kuliko kati zote za uokoaji. Katika siku hiyo, mkuu wa kamati ya uratibu wa kazi za uokoaji Bw. Farooq alisema kuwa, tetemeko la ardhi limesababisha vifo vya watu wasiopungua elfu 47, watu elfu 67 kujeruhiwa na milioni 3.3 wamepoteza makazi yao. Uokoaji wa maafa unakabiliwa na matatizo makubwa.

Tarehe 19 kwenye mkutano na waandishi wa habari Bw. Farooq alisema kuwa majira ya baridi yamekaribia katika sehemu ya kaskazini ya Pakistan, kuwapatia waathirika mahali pa kukaa na chakula ni kazi ya haraka. Alisema, ingawa jumuyia ya kimataifa imeisaidia Pakistan kwa kuipatia mahema elfu 64, lakini mahema hayo hayatoshi kabisa.

Hivi sasa ingawa barabara ya kufika kwenye sehemu ya kaskazini iliyoathirika na tetemeko la ardhi inapitika, lakini waathirika walioko mbali katika sehemu za milimani hawawezi kupata misaada, kwenye baadhi ya sehemu za milimani hata helikopta zinashindwa kutua, jeshi la Pakistan licha ya kutumia helikopta kudondosha misaada, vikosi vya jeshi hilo sasa vinapeleka misaada kwa punda. Baadhi ya waathirika hata walihatarisha maisha yao kwa kuvuka mlima na kupita kwenye sehemu yenye mporomoko wa udongo kufika Muzaffarabad baada ya kusafiri kwa siku kadhaa. Jemadari wa jeshi la anga Bw. Tahir alisema, bonde la Neelum haliwezi kuwasiliana na nje na misaada haiwezi kufikishwa huko kabla ya muda wa siku 10. Alisema, barabara iliyozuiliwa na mporomoko wa udongo haitaweza kupitika kabla ya wiki kadhaa.

Isitoshe, matetemeko madogo madogo na mabadiliko mengi ya hali ya hewa pia yameleta matatizo kwenye juhudi za uokoaji. Kutokana na takwimu zisizokamilika, tokea tetemeko hilo kubwa lilotokee tarehe 8 hadi sasa matetemeko madogo madogo zaidi ya 400 yalitokea. Asubuhi ya tarehe 19 katika sehemu ya kaskazini ya Pakistan matetemeko yenye ngazi ya tano kwenye kipimo cha Richter yalitokea mara mbili. Matetemeko kama hayo yamekwamisha vibaya kazi ya uokoaji.

Kuhusu misaada ya kimataifa, shehena kutoka jumuyia ya kimataifa zinafululiza kufikishwa nchini Pakistan, lakini misaada ya fedha nyingi bado. Msemaji wa Ofisi ya Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Elizabeth Byrs alisema, hadi sasa ofisi yake imepata asilimia 5 tu ya dola za Kimarekani milioni 27 zilizoombwa, na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kimataifa pia lina wasiwasi kuhusu hali hiyo. Mkuu wa kikundi cha Shirika la Chakula Duniani huko Muzaffarabad Bw. Keith Ursel alitahadharisha kuwa kikundi hicho kinapaswa kutoa tani 570 za chakula kila siku kwa waathirika. Kutokana na makadirio ya kikundi hicho, bado kuna waathirika laki tano ambao hawakupata msaada.

Kutokana na kukumbwa na tatizo la uokoaji, rais Musharraf wa Pakistan alisema, Pakistan inafikiria kufungua mpaka wake kwenye sehemu ya kusimamisha vita katika Kashmir na kukaribisha wakazi wa sehemu inayodhibitiwa na India wajiunge na jamaa zao na kushiriki katika ukarabati. Ameitaka jumuyia ya kimataifa iendelee kuisaidia Pakistan

Idhaa ya Kiswahili 2005-10-20