Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-20 20:02:54    
Mfaransa Olivier afuatilia watoto wenye ugonjwa wa ukimwi na watoto yatima wa ukimwi nchini China

cri

Bwana Olivier anatoka Ufaransa, hivi sasa anaishi katika mji wa Xiamen, mkoani Fujian, kusini mashariki mwa China. Akiwa mshauri huru wa biashara, siku za kawaida anashughulikia kazi za kutoa ushauri kuhusu uuzaji wa bidhaa, matangazo na uendeshaji wa mashirika. Licha ya kazi, yeye pia anapenda kuchora picha za rangi, muda si mrefu uliopita alifanya maonesho ya michoro na kutaka kutumia mapato yake yote kutokana na kuuza michoro hiyo katika kuwasaidia watoto wenye ugonjwa wa ukimwi na watoto yatima waliofiwa na wazazi wao kutokana na ugonjwa wa ukimwi.

Bw. Olivier mwenye umri wa miaka zaidi ya 40, amejipatia jina la kichina la Heping, ambalo matamshi yake yanafanana na neno la kichina Heping, maana yake ni amani. Aliwahi kujifunza uchoraji akiwa kijana, anapenda kutalii, amewahi kufika kwenye nchi na sehemu zaidi ya 20 duniani. Kabla ya miaka 7 iliyopita alikuja Xiamen na kufanya makazi yake huko. Akisema:

"Kabla ya kufika Xiamen, niliishi mjini Hong Kong. Rafiki yangu alinishauri nije kutembelea Xiamen. Mara tu nilipofika Xiamen, nilianza kuupenda mji huo, na nikaamua kuishi huko badala ya kurudi Hong Kong."

Mji wa Xiamen ulioko pwani ni sehemu maarufu ya utalii nchini China, una mandhari nzuri, na visiwa vingi. Bwana Olivier anaishi peke yake mjini Xiamen, mke wake anaishi nchini Ufaransa kutokana na kazi yake. Lakini Bwana Olivier hasikii upweke hata kidogo, ana kazi nyingi za kufanya, na wakati wa mapumziko yeye hupenda kutembelea maeneo ya karibu kwa kupanda baiskeli, na kuogelea baharini. Yeye pia anapenda kutembelea visiwani kwa kupanda ngalawa, kutembelea sehemu mbalimbali na kuchora picha.

Bwana Olivier alisema kuwa, sababu nyingine iliyomvutia aishi mjini Xiamen nchini China kwa miaka mingi kiasi hicho ni mikahawa inayoonekana hapa na pale yenye chakula kitamu cha bei nafuu. Akisema:

"Naupenda sana mji wa Xiamen pamoja na wakazi wake. Xiamen ni mji wa bustani, miti na majani yamepandwa kila mahali."

Japokuwa ameishi mjini Xiamen kwa miaka 7, lakini bado hafahamu lugha ya huko. Lakini kutofahamu lugha hakumzuii kufanya maingiliano na wakazi wenyeji, ameshuhudia mabadiliko makubwa yaliyopatikana mjini Xiamen.

Kabla ya miaka mwili iliyopita, Bwana Olivier alipata habari kutoka kwenye kipindi cha televisheni kuhusu hali ya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi nchini China, baadhi ya wanakijiji wa kijiji maskini walikufa kutokana na ugonjwa wa ukimwi, na watoto wao wameachwa yatima. Kuanzia hapo alikuwa na wazo la kufanya maonesho ya michoro ili apate fedha za kuwasaidia watoto walioathirika na ukimwi.

"Michoro yangu ni sehemu moja ya maisha yangu, siwezi kuuza sehemu hiyo ya maisha yangu. Lakini kwa ajili ya kuwasaidia watoto walioathirika na ukimwi nimeamua kuuza michoro yangu."

Maonesho yake ya michoro yaliwavutia watu wengi. Bi. Zhang Li alikuwa mmoja kati yao, alimsifu sana Bwana Olivier kwa kitendo chake cha kuwasaidia watoto wenye ugonjwa wa ukimwi, akisema:

"Maonesho yake ya michoro yamenivutia sana. Mgeni kama Bwana Olivier anaweza kufuatilia shughuli za China, sembuse sisi wachina wenyewe, tunapaswa kujishughulisha zaidi mambo yetu wenyewe."

Kitendo cha Bw. Olivier cha kufanya maonesho ya michoro kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa ukimwi na watoto yatima wa ukimwi kimepata uungaji mkono kutoka kwa watu wa sekta mbalimbali nchini China. Mashirika kadhaa ya NGO ya nchini China na ng'ambo yameunga mkono maonesho hayo, hoteli ya maonesho ya kimataifa ya Xiamen imemtolea mahali pa kuoneshea michoro bila kumtoza fedha yoyote.

Rafiki yake Bwana James Pongrass kutoka Marekani aliposikia kuwa Bwana Olivier atafanya maonesho ya michoro, alikuja China kumtembelea. Akisema:

"Mimi nashangazwa na kitendo cha Olivier cha kufanya shughuli zinazohusiana na ugonjwa wa ukimwi, ni wazo zuri kufanya maonesho ya michoro, litawasaidia watu wengi zaidi kufuatilia suala la ukimwi."

Ingawa Bw. Olivier hakupata mapato makubwa kwa kufanya maonesho ya michoro, lakini alitumai kuwa, kitendo chake kitawahimiza watu wengi zaidi kufuatilia ugonjwa wa ukimwi, wagonjwa wa ukimwi na watoto yatima wa ukimwi.

Bw. Olivier alisema kuwa, huenda atafanya maonesho ya michoro huko Hong Kong na nchi za Ulaya, ili kuwahamasisha watu wengi zaidi wafuatilie na kuwasaidia watoto wenye ugonjwa wa ukimwi na watoto yatima wa ukimwi.

Idhaa ya Kiswahili 2005-10-20