Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-20 20:04:47    
Wakulima wa Xinjiang wanaopata maendeleo ya kiuchumi haraka

cri

Eneo la mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur linachukua moja kati ya sita ya eneo lote la ardhi ya China, ni mkoa wenye eneo kubwa kabisa nchini China, una mashamba ya kilimo zaidi ya hekta milioni tatu. Mkoa huo unazalisha kwa wingi matunda yakiwemo matikiti maji ya Hami na zabibu, na mazao ya kilimo kama vile pamba na nyanya. Katika miaka ya karibuni, mkoa huo unapoendelea kuweka mkazo kuendeleza kilimo cha jadi, pia unawahamasisha wakazi kuanzisha shughuli nyingine maalum za kibiashara ili wapate maendeleo kwa haraka.

Bwana Rouzi Turxun wa kabila la Kazak anaishi katika wilaya ya Pahataikri ya sehemu ya Keshi, kusini mwa Xinjiang. Zamani familia yake ilitegemea tu kilimo, waliishi maisha ya hali duni, alikuwa hawezi hata kutarajia kuishi kwenye nyumba mpya, kuendesha pikipiki, na kutumia simu ya mkononi, lakini hivi sasa ndoto zake zote zimetimizwa kutokana na kufuga ng'ombe. Bwana Rouzi Turxun alisema kuwa, hivi sasa, katika wakati wa mapumziko ya kilimo, yeye anaweza hata kutalii nje ya mkoa huo pamoja na familia yake. Akisema:

"Maisha ya hivi sasa ni mazuri sana. Zamani tukitembelea mjini, tulikuwa tunabaguliwa kutokana na umaskini, lakini sasa hali yetu ya kimaisha inafanana na ile ya wakazi wa mjini."

Licha ya kufuga ng'ombe, hivi sasa Bwana Rouzi Turxun pia anazingatia kujishughulisha na mambo mengine kama vile kuanzisha ufugaji wa bata ili kuchuma pesa nyingi zaidi.

Katika wilaya ya Pahataikri, wakulima wengi wanatajirika kutokana na ufugaji, mkuu wa wilaya hiyo Bwana Tulahong alisema kuwa, serikali ya wilaya hiyo imechukua hatua nyingi kuwaunga mkono wakulima kujishughulisha na ufugaji, akisema:

"Ili kuwahimiza wakulima wa wilaya yetu kufuga mifugo, tunaipa kila familia inayotarajia kujishughulisha na ufugaji eneo fulani la ardhi bila malipo na kuzisaidia kuomba mkopo kutoka kwenye benki. Mwaka jana, kila familia ya wafugaji katika wilaya yetu ilipata mapato zaidi ya Yuan elfu 30."

Mkoani Xinjiang, wakulima na wafugaji wengi wanajiendeleza kutokana na ufugaji, hata baadhi ya watu wanaoishi mjini wamevutiwa kwenda vijijini kufuga ng'ombe na mbuzi, Bwana Zheng Xiang ni mmoja kati yao. Kabla ya kustaafu, Bw. Zheng Xiang alifanya kazi katika shule moja ya Urumqi, mji mkuu wa mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur. Baada ya kustaafu aliambiwa kuwa, kampuni moja ya kutengeneza maziwa na bidhaa zake imeanzisha mabanda ya kufugia ng'ombe wa maziwa na kutaka kuyakodisha kwa wafugaji bila malipo katika sehemu inayojiendesha ya kabila la wahui ya Changji iliyoko karibu na Urumqi. Hivyo yeye na mke wake walianzisha shughuli za kufuga ng'ombe. Akisema:

"Nadhani kuwa, kuchuma pesa kijijini ni rahisi zaidi kuliko mjini. Tena nilikuta sera nzuri kama ya kuomba mkopo, na kupatiwa banda la kufugia ng'ombe wa maziwa na vifaa vya kukamulia maziwa ya ng'ombe bila malipo, na kuweza kusaini mkataba wa kuuza maziwa yote kwa kampuni hiyo kwa miaka 20. Inamaanisha kuwa, sitakuwa na wasiwasi kuhusu soko la maziwa wa ng'ombe ninaowafuga.

Kabla ya miaka miwili iliyopita, Bwana Zheng alikusanya Yuan laki kadhaa kununua ng'ombe zaidi ya 20 wa maziwa, na kuanza maisha mapya ya kuuza maziwa. Hivi sasa ng'ombe wake wa maziwa wameongezeka na kufikia 60, ambao kila mwezi wanamletea pato la Yuan elfu kumi hivi.

Licha ya ufugaji , kulima pamba na nyanya pia kunaleta faida kubwa kwa wakulima wa Xinjiang. Pamba ni zao kubwa la biashara mkoani humo, kutokana na kuwa na mwangaza wa kutosha wa jua, pamba inayolimwa mkoani Xinjiang si kama tu ina sifa nzuri bali pia ina mavuno makubwa. Kwa miaka mingi, kiasi cha pamba iliyozalishwa mkoani Xinjiang inachukua nafasi ya kwanza nchini China, na hivi sasa mapato ya wakulima kutokana na kilimo cha pamba yanachukua asilimia 40 ya mapato yao ya jumla. Hivyo kilimo cha pamba huitwa "kilimo cheupe".

Xinjiang pia ni moja ya kati ya sehemu tatu zinazozalisha nyanya kwa wingi duniani, ambapo kila mwaka unazalisha tani milioni nne za nyanya, hivyo kilimo cha nyanya kinasifiwa kuwa ni "kilimo chekundu". Mashirika kadhaa makubwa ya mkoani humo yamejishughulisha na kilimo hicho chekundu. Bwana Tan Yelong ni meneja mkuu wa kampuni inayoshughulikia biashara ya vifaa vya ujenzi, alisema miaka kadhaa iliyopita kampuni yao ilianza kujishughulisha na utengenezaji wa bidhaa za mazao ya kilimo kutokana na bidhaa hizo kuwa na mustakabali mzuri. Hivi sasa, kampuni hiyo imekuwa moja ya kampuni kubwa kabisa nchini China katika kuzalisha sosi ya nyanya nchini China. Bwana Tan Yelong akisema:

"Mwaka jana kampuni yetu ilizalisha tani laki 2.7 za sosi ya nyanya, ambazo nyingi zinasafirishwa ng'ambo, zikichukua asilimia 17 ya biashara hiyo duniani."

Bwana Tan alisema kuwa, kampuni yake ina mashirika 15 yanayotengeneza bidhaa za nyanya, ambayo kila mwaka yananunua zaidi ya tani milioni 3.7 za nyanya mbichi kutoka kwa wakulima.

Serikali ya mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur imeyahimiza mashirika makubwa kuwekeza vitega uchumi katika eneo la kilimo, ambayo si kama tu yatahimiza marekebisho ya muundo wa kilimo wa mkoani humo, bali pia yatazisaidia familia mbalimbali kuzalisha mazao kutokana na mpango. Imefahamika kuwa, hivi sasa mkoa wa Xinjiang umekuwa na mashirika makubwa 100 yanayojishirikisha shughuli za kilimo, ambayo yamezinufaisha familia milioni 1.5.