Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-24 12:50:26    
Ndege yenye watu 117 ya Nigeria yapata ajali

cri

Ofisa wa serikali ya Nigeria ametangaza kuwa watu 117 wakiwemo wahudumu waliokuwa kwenye ndege iliyopata ajali jioni tarehe 22 wote wamekufa. Hii ni ndege ya pili kupata ajali kubwa nchini Nigeria katika muda wa miaka mitatu iliyopita.

Jioni tarehe 22, ndege aina ya Boeing 737-200 yenye abiria 111 na wahudumu 6 iliruka kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Lagos kuelekea Abuja, mji mkuu wa Nigeria, dakika chache baada ya ndege hiyo kuruka, rubani alitoa ombi la msaada, kisha mawasiliano na ardhi yalikatika, ndege hiyo ikaanguka kwenye msitu kilomita 30 kutoka uwanja wa ndege wa Lagos. Ndege iliyopata ajali ilichimba shimo kubwa lenye kipenyo mita 25 na kimo cha mita 10, ndege iliyozama ndani ya shimo hilo ilifuka moshi mnene. Kutokana na kutokuwepo kwa njia ya kwenda msituni, magari ya uokoaji hayakuweza kuingia. Jemadari mkuu wa usalama wa Nigeria Bw. Ade Aboluyrin kwenye mahali pa ajali aliwaambia waandishi wa habari akisema, "wote wamekufa, kwa sababu ndege imezama kabisa ndani ya ardhi, hakuna uwezekano wa mtu yeyote kunurusurika."

Ofisi ya rais wa Nigeria katika siku hiyo ilisema kuwa, rais Olusegun Obasanjo amejitokeza mwenyewe katika usimamizi wa shughuli za uokoaji. Maofisa wa shirika la ndege la Nigeria hivi sasa wako katika shughuli za kutafuta kikasha cheusi kinachorekodi hali ya usafari wa ndege. Wachunguzi wa tukio hilo walisema kuwa ndege ilipoanguka ilitokea mlipuko mkubwa, na kutokana na mahali ilipoanguka kuwa na udongo tifutifu, ndege ilizama ndani ya udongo na matope, hali hiyo ilifanya kazi ya uokoaji iwe ngumu. Uchunguzi wa mwanzo unaonesha kuwa huenda radi iliyotokea jioni hiyo au hitilafu za mashine ni chanzo cha ajali hiyo.

Habari zinasema kuwa shughuli za kutambua maiti zinaendelea. Kabla ya hapo, kulikuwa na habari kuwa kwenye ndege hiyo kulikuwa na maofisa kadhaa waandamizi wa serikali ya Nigeria, lakini nyadhifa zao hazijafahamika. Kwenye ndege hiyo pia kulikuwa abiria kadhaa wa nchi za nje, lakini pia habari zao hazijafahamika.

Kutokana na kuwepo kwa Wachina elfu 30 wanaoishi mjini Lagos, ofisi kuu ya ubalozi wa China nchini Nigeria inafuatilia sana tukio hilo. Hivi sasa ofisa husika wa ofisi hiyo amechunguza sana orodha ya majina ya abiria iliyotolewa na uwanja wa ndege, kimsingi ameondoa uwezekano wa kuwepo kwa Mchina katika ndege hiyo.

Ajali hiyo kubwa ni ya pili katika muda wa miaka mitatu iliyopita nchini Nigeria. Mei 4 mwaka 2002, ndege moja ya abiria ya Nigeria ilianguka katika mji wa Kano wenye wakazi wengi, kaskazini mwa Nigeria, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 180. Wachambuzi wanaona kuwa kutokana na matatizo ya zana, usimamizi na ukata, usafiri wa ndege za Nigeria sio salama sana.

Serikali ya Nigeria iliacha udhibiti wa sekta ya usafiri wa ndege tokea miaka ya 80 ya karne iliyopita na baada ya kubinafsisha sekta hiyo, mashirika binafsi ya ndege zaidi ya kumi yalianzishwa. Lakini kutokana na uhaba wa fedha, mashirika mengi yalipaswa kununua ndege zilizoachwa baada ya kutumika kutoka Ulaya na Marekani, ndege hizo sio tu zimepitwa na wakati tena nyingi zimetumika zaidi ya miaka 20, na baadhi ya mashirika ya ndege yana ndege kama hizo chache tu. Ili kubana gharama za matumizi, ndege hizo zinaruka katika hali ya "uchovu", hali hiyo ikiwa pamoja na kutumika bila kutunzwa, hatari ya usalama inazidi. Mwezi Aprili mwaka 2002, serikali ya Nigeria ilipiga mafuruku kwa ndege zilizotumika kwa miaka zaidi ya 22, lakini sheria hiyo ilipingwa na mashirika binafsi.

Idhaa ya kiswahili 2005-10-24