Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-25 16:48:31    
Mwendeshaji Tamthilia wa Kisasa Zhang Guangtian

cri

Bw. Zhang Guangtian ni mtu anayezungumzwa sana katika nyanja ya tamthilia, watu wanaomwunga mkono wanaona kuwa, yeye ni mtangulizi wa mageuzi ya tamthilia, na watu wanaompinga wanaona kuwa yeye si mtaalamu wa tamthilia hata kidogo.

Hata hivyo Bw. Zhang Guangtin ni mtu anayejulikana sana katika nyanja ya utamaduni nchini China. Mapema mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, alianzisha kwaya ya kienyeji katika maskani yake, mji wa Shanghai. Hii ilikuwa ni kwaya ya kwanza kabisa ya kienyeji mjini Shanghai. Katika siku hizo alitunga nyimbo nyingi na kushiriki kwenye maonesho mengi ya michezo ya sanaa. Mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita Bw. Zhang Guangtian alihamia Beijing na kushughulika na kazi ya utengenezaji wa santuri na utunzi wa tamthilia.

Ingawa kwa kiasi fulani alikuwa amepata mafanikio katika utunzi wa nyimbo na muziki, lakini hakujulikana katika nyanja ya tamthilia, alitaka kujiendeleza katika nyanja hiyo. Mwaka 2000, alihariri na kuendesha tamthilia ya "Che Guevara" na kuoneshwa mjini Beijing. Tamthilia hiyo ilichanganya matukio mengi na watu wengi wa kihistoria na wa leo kwa pamoja. Katika tamthilia hiyo mambo ya mwanamapinduzi wa Latin Amerika Bw. Che Guevara ni kama utangulizi tu. Tamthilia yenyewe ilisifu haki na mapinduzi, na inapomalizika inatumbuizwa muziki wa The Internationale Aina ya tamthilia hiyo ambayo inasifiwa na Bw. Zhang Guangtian kuwa ni "utenzi" haikuwahi kutokea nchini China, na matukio mengi tofauti yaliyochanganywa pamoja pia ni ya ajabu na kushitusha nyanja ya tamthilia. Kutokana na aina hiyo ya ajabu Bw. Zhang Guangtian akajitokeza hadharani kwa sura ya mwendeshaji tamthilia wa kisasa. Alisema, "Tamthilia hiyo ilipooneshwa ilikuwa shida sana, hatukufanya matangazo yoyote ya kuwavutia watazamaji, bali tuliwaachia watazamaji watizame kwa hiari. Kama watazamaji wakiguswa na kusisimka, kila mtizamaji atamwambia rafiki yake kwamba nenda ukatizame tamthilia hiyo, ukiikosa utajuta."

Bw. Zhang Guangtian alisema, binadamu lazima awe na imani na matumaini na kuyafuatilia bila kulegea, mtu akiwa na uchoyo wa nyumba ya fahari, gari na maisha ya anasa atakuwa sawa na mzoga hai. Bw. Zhang Guangtian anaona kuwa watu wa hivi leo wengi wanakosa matilaba na imani. Aliifanya tamthilia yake kuwa ya kuwahamasisha watazamaji wawe na matumaini, na kweli imepokelewa vizuri na watazamaji.

Baada ya tamthilia ya "Che Guevara" kufanikiwa, alifululiza kuhariri tamthilia nyingi nyingine za "Mrembo Nyota Nyekundu", "Mwandishi Mkubwa Lu Xun", "Mtu Mashuhuri Confucius". Tamthilia hizo, zote hazikutiliwa maanani hadithi yenyewe na aligawa wahusika katika mafungu mawili, hasi na chanya. Mathalan, kwenye tamthilia ya "Mtu Mashuuri Confucius", kuna wakati alipingwa na kuna wakati alisifiwa, jukwaani waigizaji kadhaa wanatoa hotuba ya kumkosoa kwa makini na pia kwa masihara, na alichanganya mambo mengi yasiyohusika na tamthili hiyo. Hii ndio sababu muhimu ya baadhi ya watu kumpinga. Baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa tamthilia za Zhang Guantian ni ya kibiashara. Lakini Bw. Zhang Guangtian alisema, "Mimi ni mwendeshaji tamthilia wa kibiashara. Ushirikiano wangu na bosi ni uhusiano wa kazi na malipo. Baadhi ya watu wanasema, kazi ni kazi na sanaa ni utunzi, kazi lazima ifanywe kwa makini na utunzi wa sanaa unaweza kupuuzwa, ukiifanya kazi vizuri utaajiriwa na bosi, utunge muziki vizuri, uendeshe tamthilia vizuri, kama watazamaji wanaridhika, basi bosi anaridhika, na baadaye utaagizwa tena na bosi, hivyo posho yako haina wasiwasi na wafanyakazi wenzako pia watafurahi kwa sababu wanaishi kwa kukutegemea."

Mwaka 2003 Zhang Guangtian alichapisha kitabu chake cha tawasifu "Maisha Yangu Hohehahe", gamba la kitabu hicho limeandikwa "mwujiza wa kisasa na jasiri wa utamaduni". Ndani ya kitabu hicho, licha ya kukumbuka miaka aliyopitia katika ukuaji wake pia kuna picha nyingi za tamthilia ili kutilia mkazo fikra zake za mageuzi ya tamthilia na kuonesha bezo lake kwa watu waheshimiwa na mila ya sanaa ya tamthilia. Kitabu kilipokuwa kimechapishwa tu mara kikasababisha mazungumzo mengi. Lakini Zhang Guangtian hakujali. Alisema, "Mtu asiyekuwa na mzigo hujiona mwepesi, anaweza kushughulikia mambo kwa utulivu na mpango. Mtu anapoona mambo yote mbele yake ni kama ua katika majira ya kiangazi, leo lipo kesho halipo, basi hatajali chochote. Mimi ni mtu hohehahe, sina mali yoyote ya kuondoka nayo duniani."

Bw. Zhang Guangtian alisema, uvumbuzi ni maisha yake yote, ana matumaini mengi ikiwa ni pamoja na mageuzi ya Opera ya Kibeijing. Anatumai kuwa majaribio yake yangeweza kuiletea nyanja ya tamthilia sura mpya.

Idhaa ya kiswahili 2005-10-25