|
Tume huru ya uchaguzi ya Iraq tarehe 25 ilitoa hadharani matokeo rasmi ya upigaji kura wa maoni ya raia kuhusu katiba ya taifa na kutangaza kuwa katiba mpya ya taifa ya Iraq imepitishwa kwenye upigaji kura huo.
Habari zinasema kuwa kati ya wapiga kura walioshiriki kwenye upigaji kura wa taifa wa Iraq, zaidi ya asilimia 78 walipiga kura za ndio. Mbali na asilimia 55 ya wapiga kura wa mkoa wa Ninevah waliopiga kura za hapana na theluthi mbili za wapiga kura wa mikoa ya Anbar na Salahuddin walipiga kura za hapana, wapiga kura wanaounga mkono katiba mpya katika mikoa mingine wote wanazidi nusu ya wapiga kura wote. Kutokana na katiba ya muda ya Iraq, katiba mpya inapitishwa kwa kuungwa mkono na wapiga kura wanaochukua zaidi ya nusu ya wapiga kura wote, lakini kama theluthi mbili ya wapiga kura wa mikoa mitatu yoyote kati ya mikoa 18 nchini Iraq watapiga kura ya hapana kwa katiba mpya, basi katiba hiyo haitapitishwa. Hivyo, katiba mpya imepitishwa kwa ushindi mdogo. Vyombo vya habari vinaona kuwa matokeo hayo yamechukuliwa kama ni jambo kubwa katika maisha ya kisiasa nchini Iraq ambayo yatahimiza mchakato wa ukarabati upya wa kisiasa nchini humo.
Kwanza, kupitishwa kwa katiba mpya ya taifa kumeondoa vikwazo kwa mpango wa ukarabati upya wa kisiasa wa hatua zijazo. Kutokana na ratiba, katiba mpya ya Iraq itafanya uchaguzi wa bunge mwezi Desemba mwaka huu na kuunda serikali mpya itakayowakilisha watu wote wa Iraq. Katiba mpya ikiwa sheria kubwa ya kimsingi ya taifa imesafisha mpango wa kisiasa nchini Iraq katika siku za usoni. Kupitishwa kwa katiba mpya ni hatua muhimu ya kwanza iliyopigwa kwenye mchakato wa ukarabati wa kisiasa na kidemokrasia nchini Iraq.
Pili, kupitishwa kwa katiba mpya ni matokeo ya usuluhishi wa madhehebu mbalimbali, ambako kunasaidia kurejesha utulivu na usalama nchini humo. Kundi la madhehebu ya Sunni halikupata faida halisi kutokana na kususia uchaguzi wa bunge la mpito na kuelewa hatua kwa hatua umuhimu wa kulinda maslahi yake na kushiriki kwenye mchakato wa kisiasa kwa kupiga kura. Kwa hiyo makundi muhimu ya madhehebu ya Sunni yameshiriki kwenye mchakato wa kutunga katiba ulioongozwa na madhehebu ya Shia na Wakurd. Madhehebu za Shia na Wakurd pia wamejua kuwa ni kwa kufanya usuluhishi tu, ndipo itakapowezekana kuyafanya madhehebu ya Sunni yasisusie upigaji kura za maoni ya raia kuhusu katiba na kuhakikisha uhalali wa upigaji kura.
Zaidi ya hayo, kupitishwa kwa upigaji kura wa katiba mpya pia kumeweka msingi wa kuondoka nchini Iraq kwa jeshi la Marekani. Hivi sasa idadi ya askari wa jeshi la Marekani nchini Iraq ni laki 1.5 ambayo imekuwa kisingizio cha makundi ya kisilaha kushambulia jeshi la Marekani. Marekani inashikilia kuwa hadi hali ya kisiasa na usalama nchini Iraq itakapokuwa nzuri, ndipo jeshi la Marekani litakapofikiri kuondoka nchini humo. Kadiri mchakato wa kisiasa wa Iraq unayoendelea hatua kwa hatua, ndivyo Marekani itaweka ratiba yake ya kuondoa jeshi lake kutoka nchini Iraq.
Inatubidi tuone kuwa ingawa pande mbalimbali za Iraq zimesuluhishana kwa hatua fulani katika mchakato wa kutunga katiba, lakini tofauti kati ya madhehebu mbalimbali kimsingi bado hazijatatuliwa. Katika muda mfupi ujao, matokeo ya upigaji kura yatayakatisha tamaa makundi na raia wa madhehebu ya Sunni wanaopinga katiba, hata wanaweza kuyafanya makundi hayo yaanzishe tena mashambulizi mapya dhidi ya jeshi la Marekani.
Lakini kupitishwa kwa upigaji kura wa raia wa katiba mpya kunaonesha kuwa ingawa bado kuna tofauti mbalimbali, lakini madhehebu mbalimbali ya Iraq yana maslahi ya pamoja. Kulinda mamlaka ya Iraq na kutimiza kuifanya Iraq itawaliwe na wairaq kunaambatana maslahi ya pamoja ya madhehebu hayo. Watu wanaamini kuwa madhehebu hayo yatapunguza tofauti zao na kutimiza kuifanya Iraq itawaliwe na wairaq.
Idhaa ya kiswahili 2005-10-25
|