Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-26 20:39:45    
China yatilia mkazo katika elimu ya vijijini

cri

Tarehe 3 mwezi Oktoba, mkutano wa 33 wa Shirika la Elimu, Sayansi, Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ulifanyika huko Paris, na ujumbe kutoka nchi wanachama 191 za Umoja wa Mataifa ulishiriki kwenye mkutano huo. Waziri wa elimu wa China Bw. Zhouji pia aliongoza ujumbe wa China kushiriki kwenye mkutano huo, na alitoa pendekezo la China kwa UNESCO linalohusu kutimiza lengo la elimu kwa wote ili kupata maendeleo makubwa zaidi.

Tarehe 5 Bw. Zhou Ji alikutana na katibu mkuu wa shirika hilo Bw. Koichiro Matsuura na kusema kuwa, China inatilia mkazo elimu ya vijijini. Bw. Zhou Ji alisema kuwa, elimu kwa wote ni moja kati ya masuala muhimu ya elimu, na pia ni suala la maendeleo, linalohusu maendeleo endelevu ya kila mtu na ya binadamu wote. Elimu ya vijijini ni sehemu muhimu ya mpango wa kutoa elimu kwa wananchi wote wa China. Serikali ya China imeahidi kuwa, katika miaka ijayo, China itatenga fedha nyingi zaidi katika kuendeleza elimu ya vijijini, hasa kuunga mkono elimu ya lazima kwenye sehemu maskini na sehemu za makabila madogomadogo. Pia alidokeza kuwa, katika mwaka 2004 elimu ya lazima ilitekelezwa katika sehemu zenye watu asilimia 93.6 ya Wachina, na idadi ya vijana wasiojua kusoma na kuandika imepungua na kufikia asilimia 4 ya vijana wote nchini China.

Bw. Koichiro alisifu juhudi zilizofanywa na China katika kutimiza kikamilifu lengo la elimu kwa wote, na kuona kuwa China imeshiriki kwa juhudi kwenye shughuli mbalimbali zilizoandaliwa na UNESCO, na kutoa mchango kwa shughuli za elimu, sayansi na utamaduni za binadamu.

Bw. Zhouji alisema kuwa, hivi sasa tatizo lililopo katika elimu nchini China ni mgongano kati ya mahitaji ya elimu na upungufu wa raslimali nzuri za elimu. Alisema, China ina wanafunzi milioni 250 na walimu zaidi ya milioni 10, ili kutoa elimu nzuri kwa idadi kubwa namna hiyo, China inapaswa kufanya juhudi kubwa zaidi. Hivyo, serikali ya China imefikiria kwa makini suala hilo, hasa suala la elimu ya vijijini, wakati ilipotunga mpango wa 11 wa maendeleo ya miaka mitano.

Mkutano wa 33 wa shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO tarehe 3 Oktoba ulifanyika mjini Paris, Ufaransa, ambao uliwashirikisha wajumbe wa nchi wanachama 191. Alipohutubia mkutano huo kwa niaba ya serikali ya China, Bwana Zhou Ji alisema kuwa, kutimiza lengo la kutoa elimu kwa wote na kupata maendeleo makubwa kutakuwa lengo la serikali ya China katika siku zijazo. Bw. Zhou Ji pia alitumai kuwa, UNESCO litafuatilia zaidi umuhimu wa sayansi na elimu katika kuhimiza maendeleo yenye uwiano kati ya binadamu na maumbile, kuhimiza zaidi mazungumzo na maingiliano kati ya ustaraabu tofauti duniani, na kujenga kwa pamoja dunia yenye maelewano.

Idhaa ya Kiswahili 2005-10-26