Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-27 15:10:48    
Umoja wa Mataifa waitisha mkutano wa kupambana na maafa ya tetemeko la ardhi yaliyotokea katika Asia Kusini

cri

Umoja wa Mataifa tarehe 26 mjini Geneva uliitisha mkutano wa mawaziri wa kupambana na maafa ya tetemeko la ardhi yaliyotokea Asia Kusini na kujadili masuala kuhusu kuongeza msaada wa fedha na kuzidi kufanya uratibu wa vitendo vya kutoa misaada vya kimataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan na wajumbe wa nchi 65 ikiwemo China na jumuiya za kimataifa walihudhuria mkutano huo. Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mambo ya kibinadamu Bw. Jan Egeland alitangaza baada ya mkutano huo kuwa, mkutano huo umepata mafanikio na nchi mbalimbali zimeahidi kutoa msaada wa fedha wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 525.

Kutokana na takwimu mpya zilizotolewa na idara husika za Umoja wa Mataifa, tetemeko kubwa la ardhi lililotokea tarehe 8 mwezi Oktoba katika sehemu ya Asia Kusini limesababisha vifo vya watu elfu 54 na wengine elfu 77 kujeruhiwa, watu milioni 3.3 hawana makazi na miundo mbinu mikubwa yote imeteketezwa katika eneo la kilomita za mraba elfu 28. Hivyo ukarabati wa sehemu zilizokumbwa na maafa unahitaji fedha zisizopungua dola za kimarekani bilioni 5.

Bw. Jan Egeland alieleza kabla ya hapo kuwa tetemeko kubwa la ardhi lililotokea katika Asia Kusini ni changamoto kubwa kabisa inayoukabili Umoja wa Mataifa katika utoaji misaada ya kibinadamu, lakini kiasi cha misaada iliyotolewa na jumuiya ya kimataifa kwa sehemu hizo bado hakitoshi. Alisema kuwa wiki mbili baada ya kutokea kwa maafa hayo, watu laki kadhaa waliokumbwa na maafa hawakupata msaada wowote kutokana na mawasiliano mabaya. Kutokana na kukaribia kwa siku za baridi, kiwango cha hali mbaya kinaweza kuzidi kile cha tsunami iliyotokea mwishoni mwa mwaka jana katika bahari ya Hindi.

Msemaji wa ofisi ya uratibu wa mambo ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Bw. Elisabeth Byrs alisema kuwa, ingawa ushiriki wa NATO kwenye harakati za kutoa misaada na uchukuzi wa vitu vya misaada umeongezeka, lakini hadi hivi sasa watu laki 8 waliokumbwa na maafa bado hawana makazi. Kutokana na hali mbaya ya mawasiliano, helikopta ni chombo pekee cha kupeleka vitu vya misaada.

Bw. Jan Egeland alieleza kuwa ili kuhakikisha watu hao wanapata makazi katika siku za baridi, jumuiya ya kimataifa lazima iongeze misaada ya fedha. Alidokeza kuwa lengo la mkutano huo ni kukusanya dola za kimarekani milioni 550, lakini Umoja wa Mataifa umepata dola za kimarekani milioni 102 tu, pengo hilo bado ni kubwa.

Bw. Kofi Annan alisema kuwa tetemeko la ardhi limewafanya watu milioni 3 waliokumbwa na maafa walale nje, madhumuni ya mkutano huo ni kuepusha kuleta maafa mapya ya kibinadamu siku za baridi zitakapofika, hizo ni mbio za kupambana na wakati. Alisema pia, akiba za mahema yanayotumiwa katika siku za baridi duniani karibu imekwisha, ni lazima kutafuta njia nyingine ya kuwahifadhi watu hao.

Mkuu wa ujumbe wa China, ambaye pia ni waziri msaidizi wa biashara Bw. Huang Hai alieleza katika hotuba yake kuwa baada ya kutokea tetemeko hilo kubwa la ardhi, serikali ya China ilichukua hatua za haraka na kutoa misaada ya fedha na vitu vyenye thamani ya dola za kimarekani milioni 6.2. Serikali ya China siku zote inatetea na kupendekeza harakati za utoaji misaada wa pande nyingi ziongozwe na Umoja wa Mataifa na kupenda kuzipatia misaada ya dharura sehemu zilizokumbwa na maafa katika hali inayowezekana. Ili kuitikia mwito wa dharura wa Umoja wa Mataifa, serikali ya China itaendelea kutoa misaada ya mahema na mablanketi yenye thamani ya dola za kimarekani laki 5 na Yuan laki 5 ambayo yatapelekwa nchini Pakistan wiki ijayo. Zaidi ya hayo, serikali ya China itatoa misaada mingine na kushiriki kwenye ukarabati wa baada ya maafa.

Idhaa ya kiswahili 2005-10-27