Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-27 16:49:36    
Huduma za kutafutia wachumba nchini China

cri

Bwana Ren Tian ni mkurugenzi wa kituo cha kutafutia wachumba cha Zijincheng ambacho ni kituo kikubwa kabisa cha aina hiyo mjini Beijing. Hivi sasa Bwana Ren Tian anashughulikia kuanzisha shirikisho la vituo vikubwa vya huduma za kutafutia wachumba vya sehemu mbalimbali nchini China. Bw. Rentian alisema kuwa, katika miaka miwili iliyopita, watu wengi wamekuwa wakihitaji huduma hizo, hivyo kumekuwepo na haja ya kuanzishwa kwa mtandao wa kutoa huduma za kutafutia wachumba nchini kote.

"Kituo cha kutafutia wachumba cha Zijincheng kinajulikana sana mjini Beijing, tunatumai kuhimiza maendeleo ya sekta hiyo kwa kutoa huduma bora na kuanzisha usimamizi wa kompyuta, ili kuwahudumia vizuri wateja wetu na kuwapatia watu wengi zaidi fursa za kukutana."

Kama Bw. Rentian alivyoona, katika miaka ya karibuni sekta ya kutoa huduma za kutafutia wachumba imekuwa moto moto. Kutokana na desturi ya jadi, kazi hiyo hufanywa na washenga. Zaidi ya miaka 20 iliyopita, kituo cha kwanza cha kutafutia wachumba kilianzishwa hapa Beijing na shirikisho la wanawake la Beijing. Mwanzoni shughuli zilizofanywa na kituo hicho kwa makapera wenye umri mkubwa zilikuwa kuandaa mchezo wa dansi katika bustani kila baada ya muda fulani, ili kuwapatia fursa za kukutana.

Baadaye watu wengi zaidi walitaka kupewa huduma za kutafutiwa wachumba, hivyo vituo vya kutafutia wachumba viliongezeka haraka. Hivi sasa China ina vituo zaidi ya 5000 vya aina hiyo, ambavyo si kama tu vimetoa huduma za kuwakutanisha makapera, bali pia kuwasaidia watu hao namna ya kukabiliana na matatizo yaliyotokea katika mchakato wa kufahamiana na maisha ya ndoa.

Vituo vya kutoa huduma za kukutanisha wachumba viko sehemu mbalimbali nchini China, hasa mijini. Mjini Beijing kuna makapera zaidi ya laki tano wenye umri kati ya miaka 35 hadi 50. Makapera hao wa kiume na kike wakijiandikisha kuwa wanachama wa vituo vya kutafutia wachumba, basi watapewa huduma za kuchaguliwa au kuwachagua watu wanaoambatana na matakwa yao. Imefahamika kuwa, vituo vikubwa vya kutafutia wachumba vina wanachama elfu kumi kadhaa au laki kadhaa.

Baadhi ya vituo vya kutafutia wachumba vinawahudumia wateja wa aina maalum. Kwa mfano katika mji wa Zhengzhou, mji mkuu wa mkoa wa Henan, katikati ya China, kuna kituo kimoja kinachotoa huduma kwa wasomi tu. Bi. Li Jian kutoka kituo hicho alisema:

"Lengo letu ni kuwahudumia wasomi tu . Kwa sababu watu hao wanazongwa na kazi, hawana wakati wa kutafuta wachumba, hivyo wanahitaji msaada."

Wafanyakazi wengi wa vituo hivyo ni wanawake wa makamo, labda kutokana na kuwa, wanawake wa umri huo wana subira na makini zaidi, pia wamekuwa na maarifa fulani ya kimaisha na kindoa. Licha ya kutafutia wachumba, wafanyakazi hao pia wanatoa ushauri kwa wateja wao wenye matatizo katika kutafuta wachumba.

Nchini China bado haijulikani watu wangapi wanapata ndoa kwa kupitia vituo hivyo. Mwandishi wetu wa habari alipokusanya habari katika mji wa Dalian, sehemu ya pwani ya China alimkuta Bwana Xin Tianxing aliyempata mke wake kwa kupitia kituo cha utoaji huduma za kutafutia wachumba. Akisema:

"Nilifanikiwa kupata mke wangu katika kituo cha kutafutia wachumba. Mke wangu pia ni mkazi wa Dalian, anafanya kazi katika kampuni moja. Tunapendana na tunaishi maisha mazuri."

Bwana Lu bin mwenye umri wa miaka 27 anafanya kazi katika kampuni moja ya Beijing. Mwaka jana alijiunga na kituo cha kutafutia wachumba, muda si mrefu uliopita alifanikiwa kupata mchumba. Akisema:

"Mimi nina kazi nyingi sana, sina muda wa kutafuta mchumba, hivyo nilijiandikisha kuwa mwanachama wa kituo cha kutafutia wachumba."

Mtaalamu wa suala la ndoa wa China alichambua kuwa, makarani wengi wa China kama Bw. Lu Bin, wanakabiliwa na ushindani mkali na shinikizo kubwa kazini, hawana muda wa kutosha kuwasiliana na watu walio nje ya kazi zao, hivyo ni vigumu kwao kujipatia wenyewe wachumba wanaofaa, hivyo wengi wao wanaomba msaada kutoka kwenye vituo vya kutafutia wachumba.

Lakini, sekta hiyo bado ina dosari nyingi. Kwa mfano, ili kuchuma pesa nyingi zaidi, baadhi ya vituo vidogo vinawaajiri watu maalum wajifanye kama wanachama ili kuwadanganya wateja halisi, na vituo vingine vinatoza pesa nyingi kupita kiasi.

Ili kusawazisha shughuli za vituo vya ndoa, muda si mrefu uliopita, wizara ya mambo ya raia ya China ilianzisha kamati inayoshughulikia vituo vya kutafutia wachumba, ambayo itatunga utaratibu halisi kuhusu utoaji huduma za aina hiyo, kuandaa mafunzo kwa wafanyakazi wa vituo hivyo, na kuvifahamisha vituo bora kwa jamii. Inaaminika kuwa, chini ya uingiliaji kati wa serikali na kuanzishwa kwa shirikisho la vituo vya ndoa, soko la kutafutia wachumba nchini China litapata maendeleo mazuri.

Idhaa ya kiswahili 2005-10-27