Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-27 16:55:45    
China yaboresha maisha ya makabila yenye idadi ndogo ya watu

cri

Kabila la Wamaonan ni moja ya makabila yenye idadi ndogo sana ya watu nchini China, wanaishi katika wilaya inayojiendesha ya kabila la Wamaonan ya mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi, kusini mwa China. Wanaishi kwenye sehemu ya milimani, eneo la ardhi la wastani linalofaa kwa kilimo ni dogo sana. Mkuu wa wilaya hiyo Bwana Tan Kejiang alipozungumzia matatizo yaliyopo katika maendeleo ya kabila la Wamaonan alisema:

"Tatizo la kwanza ni miundo mbinu dhaifu, hasa upungufu wa maji ya kunywa kwa watu wanaoishi milimani. Tatizo lingine ni mawasiliano, wanavijiji wakitaka kutoka nje ya kijiji wanapaswa kutembea kwa muda wa saa tatu hadi tano."

Hivi sasa, China ina makabila 22 yenye idadi ya watu wasiozidi laki moja, watu hao wanaishi kwenye sehemu za milima ya mipakani mwa China, mazingira yao ya kuishi ni mabaya sana. Makabila hayo huitwa makabila yenye idadi ndogo ya watu. Kama alivyosema Bw. Tan, watu wa makabila hayo wanakabiliwa na matatizo ya pamoja, yaani hali duni ya uzalishaji mali na ya kimaisha, umaskini na maendeleo dhaifu ya kiuchumi.

Kwa jumla makabila hayo 22 yana watu laki 6 na elfu 30, japokuwa wanachukua sehemu ndogo tu ya idadi kubwa ya watu nchini China, lakini serikali ya China inafuatilia sana maendeleo yao ya kiuchumi na kimaisha. Mwaka 2004, kwenye mkutano wa kimataifa wa kuwasaidia watu wenye matatizo ya kiuchumi uliofanyika mjini Shanghai, waziri mkuu Wen Jiabao aliahidi kuharakisha hatua za kuondoa umaskini kwa watu wa makabila hayo. Muda si mrefu uliopita, baraza la serikali ya China pia lilipitisha mpango wa 2005-2010 wa kuhimiza maendeleo ya makabila yenye idadi ndogo ya watu.

Naibu mkuu wa kamati inayoshughulikia mambo ya makabila madogo madogo ya China Bwana Yang Jianqiang alisema:

"Kazi muhimu katika kuhimiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya makabila hayo, ni kuimarisha ujenzi wa miundo mbinu, kuboresha hali ya uzalishaji mali na ya kimaisha, kurekebisha miundo ya kiuchumi, kuhimiza maendeleo ya sayansi na teknolojia, elimu, afya, na utamaduni, kuimarisha kazi ya kuandaa wataalamu ili kuinua sifa ya jumla za watu wa makabila hayo."

Bw. Yang Jianqiang alisema katika miaka mitano ijayo, China itatenga yuan bilioni moja kuvisaidia vijiji vya watu wa makabila yenye idadi ndogo ya watu kujenga miundo mbinu kama vile zana za umeme, simu, barabara, matangazo ya radio na televisheni, maji ya kunywa na makazi yao, ili kuboresha kimsingi hali yao ya kimaisha na ya uzalishaji mali.

Nchini China bado kuna watu maskini laki mbili wanaoishi katika sehemu za makabila yenye idadi ndogo ya watu. Bw. Yang Jianqiang alisema kuwa, sehemu hizo zina raslimali nyingi, ili kuwasaidia wakazi wa sehemu hizo kujipatia maendeleo ya kiuchumi, serikali ya China itaongeza uwekezaji katika kilimo cha mazao yasiyo na uchafuzi, mazao maalum ya kilimo, na shughuli za utalii.

Kwa mfano, kwa miaka kadhaa iliyopita makabila ya Wabulang na wakinuo wanaoishi mkoani Yunnan waliishi maisha duni. Baada ya kufanya utafiti, serikali ya mkoa huo iligundua kuwa sehemu hiyo inafaa kupanda miti ya chai isiyohitaji kutumia mbolea ya chumvi chumvi, hivyo ikawahimiza wakazi wa huko wapande miti mingi ya chai, sasa watu hao wamejipatia maendeleo ya kiuchumi kutokana na kilimo cha chai.

Makabila madogo madogo ya China yana utamaduni wa kipekee. Serikali ya China imechukua hatua nyingi ili kuhifadhi utamaduni wa makabila hayo 22 yenye idadi ndogo ya watu. Bw. Yang Jianqiang alisema:

"Hatua hizo ni kutunga sheria na taratibu husika za kulinda utamaduni wa makabila hayo, kuanzisha idara maalum zinazoshughulikia mambo ya utamaduni, na kuimarisha ujenzi wa miundo mbinu ya kiutamaduni; kutoa mafunzo kwa watu wenye ujuzi wa kiutamaduni na kisanii wa makabila hayo, na kuchukua hatua za kuokoa utamaduni wa makabila yanayokaribia kutoweka."

Kwa mfano, kabila la Wahezhe wanaoishi katika mkoa wa Heilongjiang, kaskazini mashariki ya China lina idadi ya watu 4600 tu. Ofisa husika wa kabila hilo Bi. You Jianhong anayeishi katika mji wa Tongjiang alisema, mji huo uko mbioni kukusanya na kuchapisha vitabu au CD na DVD kuhusu nyimbo na historia ya kabila hilo. Akisema:

"Mji wa Tongjiang umejenga jumba la kwanza la kitaifa la makumbusho ya kabila la Wahezhe, pia umeanzisha kikundi cha wachezaji wa michezo ya sanaa wa kabila la Wahezhe, baadhi yao wanashiriki katika shughuli za maingiliano ya kiutamaduni ya kimataifa mara kwa mara. Pia umeanzisha kituo cha kutoa mafunzo kwa watoto na idara ya utafiti wa mambo ya kabila la Wahezhe."

Idhaa ya kiswahili 2005-10-27