Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-28 12:46:44    
China yaandaa mafunzo ya hifadhi ya mazingira kwa maofisa wa mazingira kutoka nchi za Afrika

cri

Mwezi Septemba mwaka huu, maofisa zaidi ya 20 wanaoshughulikia hifadhi ya mazingira kutoka nchi 19 za Afrika walishiriki kwenye mafunzo ya hifadhi ya mazingira yaliyoandaliwa na idara kuu ya hifadhi ya mazingira ya China. Ofisa wa idara kuu ya hifadhi ya mazingira ya China anayeshughulikia mafunzo hayo Bwana Hong Shaoxian alisema kuwa, mafunzo hayo yametoa nafasi nzuri kwa maofisa hao kujifunza uzoefu na teknolojia za usimamizi wa hifadhi ya mazingira ya China, yatahimiza sana maingiliano na ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika katika eneo la hifadhi ya mazingira.

Bara la Afrika ni sehemu yenye nchi nyingi kabisa zinazoendelea. Nchi hizo za Afrika zinapojitahidi kuendeleza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi, zinakabiliwa na matatizo mengi ya hifadhi ya mazingira. Ili kuimarisha ushirikiano na maingiliano kati ya China na nchi za Afrika katika eneo la hifadhi ya mazingira, mwezi Februari mwaka huu, pande hizo mbili zilifanya mkutano wa kazi wa hifadhi ya mazingira huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya. Kwenye mkutano huo, naibu waziri mkuu wa China Bwana Zeng Peiyan alisema kuwa, China inapenda kuimarisha maingiliano na ushirikiano wa pande nyingi kati yake na nchi za Afrika katika eneo la hifadhi ya mazingira, kuwaandaa maofisa watakaoshughulikia hifadhi ya mazingira kwa nchi za Afrika, na kuwafahamisha uzoefu na tekinolojia za China katika eneo hilo.

Afrika ni sehemu yenye upungufu mkubwa wa raslimali za maji, mgawanyo wa maji katika bara hilo hauna uwiano, na tena zinakabiliwa na tatizo kubwa la uchafuzi. Bwana Hong Shaomin alisema:

"China iliwahi kukabiliwa na matatizo ya aina mbalimbali katika hifadhi ya mazingira, mazingira ya China yanafanana na yale ya nchi za Afrika, China ina ukanda wa jangwa, ukanda wenye mvua chache, hivyo uzoefu wa China katika kukinga na kuzuia uchafuzi wa maji na matumizi ya raslimali za maji utazifaa sana nchi za Afrika. Lengo la kuandaa mafunzo hayo ni kuwafahamisha maofisa husika wa nchi za Afrika uzoefu wa China katika eneo la hifadhi ya mazingira."

Kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo, naibu mkurugenzi wa idara kuu ya hifadhi ya mazingira ya China Bi. Wang Jirong alisema kuwa, ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika katika hifadhi ya mazingira bila shaka utachangia maendeleo endelevu duniani. Aliainisha kuwa, tatizo la maji ni tatizo la dunia nzima, kukinga na kushughulikia uchafuzi wa maji, kutimiza matumizi endelevu ya raslimali za maji, na kuhakikisha maendeleo endelevu ya uchumi na jamii, ni changamoto kubwa inayozikabili nchi nyingi duniani.

Mkurugenzi wa ofisi inayoshughulikia mambo ya nchi za Afrika ya shirika la mpango wa hifadhi ya mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP Bwana Dur alitoa hotuba kwenye ufunguzi akiainisha kuwa, kufanya mafunzo hayo ya hifadhi ya mazingira ni hatua moja muhimu iliyochukuliwa na serikali ya China katika kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika eneo la hifadhi ya mazingira.

Katika muda wa siku zaidi ya 20, maofisa kutoka nchi 19 za Afrika ambazo ni pamoja na Kenya, Tanzania, Niger, Liberia, Afrika ya kusini, Mauritius na Cote d'ivoire walikuwa wamefahamishwa uzoefu kuhusu hifadhi ya raslimali za maji, jinsi ya kushughulikia majitaka, na mfumo wa usimamizi wa hifadhi ya mazingira. Maprofesa kutoka vyuo vikuu maarufu nchini China walitoa maelezo kwa kinaganaga kuhusu tekinolojia na ustadi wa China katika kushughulikia uchafuzi wa mazingira. Zaidi ya hayo, maofisa hao wa nchi za Afrika pia walitembelea kituo kikuu cha ukaguzi wa hifadhi ya mazingira ya China, kituo cha usimamizi cha idara kuu ya hifadhi ya mazingira ya China, mashirika yanayoshughulikia majitaka na upimaji wa ubora wa maji na kadhalika.

Imefahamika kuwa, kwenye mafunzo hayo, maofisa wa nchi za Afrika si kama tu wamejifunza ujuzi wa hifadhi ya mazingira na uzoefu wa kusimamia mazingira, bali pia wamefahamu zaidi tekinolojia ya hifadhi ya mazingira ya China. Maofisa wengi wameona kuwa, tekinolojia na zana za China zinazotumika katika kushughulikia ukaguzi na upimaji wa mazingira na majitaka zinazifaa sana nchi za Afrika. Wanatumai kuwa, China itazipatia nchi za Afrika msaada wa kiteknolojia, ili kuzisaidia kushughulikia uchafuzi wa maji kwa ufanisi. Bwana Hong Shaomin alisema kuwa, maofisa wanaoshughulikia hifadhi ya mazingira wa nchi za Afrika walikuwa na maoni mengi kuhusu mafunzo hayo. Akisema:

"Maofisa hao wanatumai kuwa, nchi zao zitaweza kutuma watu wengi zaidi kuja kupata mafunzo nchini China. Ambao si kama tu wataweza kufahamishwa nadharia ya hifadhi ya mazingira, bali pia wataona kwa macho yao yenyewe jinsi China inavyoshughulikia mambo ya mazingira baada ya kujipatia maendeleo makubwa ya kiuchumi. Waliona kuwa, uzoefu wa China utatoa mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi za nchi za Afrika."

Bwana Hong Shaomin alidokeza kuwa, mafunzo ya pili ya hifadhi ya mazingira kwa nchi za Afrika yanatarajia kufanyika mwezi Desemba mwaka huu. Na Idara kuu ya hifadhi ya mazingira ya China imeamua kufanya mafunzo hayo kwa muda mrefu.

Idhaa ya kiswahili 2005-10-28