Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-01 19:24:38    
Kwa nini azimio la baraza la usalama halijaiwekea vikwazo Syria

cri

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 31 mwezi Oktoba lilipitisha azimio kuhusu uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Bw Rafik al-Hariri, ambalo linaitaka Syria kushirikiana kikamilifu na tume ya uchunguzi ya kimataifa. Lakini azimio hilo halikuweka tishio la kuiwekea vikwazo Syria lililotolewa na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing kwenye mkutano wa ngazi ya mawaziri wa baraza la usalama alisema kuwa, uchunguzi wa tukio hilo bado haujakamilika, na China inapinga kuiwekea vikwazo Syria hivi sasa.

Waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Bw Rafik al-Hariri aliuawa katika mlipuko wa gari lenye mabomu mwezi Februari mwaka huu. Kwa hiyo nchi za magharibi siku zote zinailenga Syria. Mwezi Aprili mwaka huu, Syria ililazimika kuondoa jeshi lake kutoka Lebanon kutokana na shinikizo la nchi hizo. Hatua hiyo imesababisha kukomeshwa kwa uhusiano maalum wa kiwenzi uliokuwepo kati ya Syria na Lebanon zaidi ya miaka 20 iliyopita. Tarehe 20 mwezi Oktoba, tume ya uchunguzi ya kimataifa iliyoteuliwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan ilitoa ripoti ikisema kuwa, kuna ushahidi unaoonesha kuwa maofisa waandamizi wa usalama wa Syria walishiriki kwenye tukio hilo. Ingawa ripoti hiyo ni ya mwanzo tu, lakini kutokana na kutumia ripoti hiyo, Marekani, Uingereza na Ufaransa zililikabidhi baraza la usalama mswada wa azimio, zikiilaani Syria kuunga mkono ugaidi, na kutishia kuiwekea vikwazo. Mswada huo ulisababisha mgongano mkubwa ndani ya baraza la usalama. China, Russia na Algeria zinaona kuwa, haifai kutishia kuweka vikwazo kabla ya uchunguzi kukamilika. Kutokana na kupingwa na nchi nyingi wajumbe wa baraza la usalama, Marekani, Uingereza na Ufaransa zilikubali kufuta yale ya tishio la kuiwekea Syria vikwazo kwenye mswada huo, na kuhimiza mswada huo kupitishwa mwishoni.

 

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Bw. Farouk al-shara baada ya azimio husika la baraza la usalama kupitishwa alisema kuwa, serikali ya Syria itaendelea kushirikiana kikamilifu na tume ya uchunguzi ya kimataifa. Pia alizikosoa Marekani na Uingereza kuwa na lengo la kutumia ripoti hiyo kuitishia Syria. Kwa kweli, ukosoaji wa Bw. Share una msingi. Marekani siku zote inaichukulia Syria kuwa nchi inayounga mkono ugaidi, na kuilaani Syria kuzuia mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Baada ya vita dhidi ya Iraq, Marekani inaona kuwa Syria ni kikwazo kikubwa kwake katika kutekeleza mpango wa demokrasia ya Mashariki ya Kati, hivyo inatoa shinikizo mara kwa mara. Vyombo vya habari vya kiarabu vinaona kuwa, madhumuni halisi ya Marekani sio kufanya uchunguzi wa tukio hilo, bali ni kuiwekea shinikizo Syria. Ripoti ya tume ya uchunguzi ya kimataifa inatoa fursa nzuri kwa Marekani kuishinikiza Syria.

 

Kushughulikia uhusiano wa kimataifa, njia pekee ya kutatua migogoro ya kimataifa ni kupitia mazungumzo na mashauriano, si kuweka vikwazo au kutishia kuweka vikwazo. Lengo la Marekani, Uingereza na Ufaransa kutaka kuiwekea vikwazo Syria kwa kupitia azimio la baraza la usalama halijafanikiwa, hii inaonesha kuwa kuweka vikwazo visivyofaa hakutafanikiwa. Kama waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing alivyosema, kabla ya uchunguzi kumalizika, baraza la usalama halifai kutoa matokeo ya uchunguzi na kutishia kuweka vikwazo, kwa kuwa hii haitasaidia kutatua masuala, na itaifanya hali ya Mashariki ya Kati kuwa ya utatanishi zaidi.

 

Idhaa ya Kiswahili 2005-11-01