Shirika la biashara duniani WTO lilifanya mkutano tarehe 31 Oktoba huko Geneva, lakini mkutano huo ulimalizika bila matokeo yoyote kutokana na nchi nyingi wanachama kutoridhishwa na pendekezo jipya lililotolewa na Umoja wa Ulaya kuhusu masuala ya kilimo. Hivyo ingawa umebaki muda wa mwezi mmoja na nusu kabla ya kufanyika kwa mkutano wa mawaziri wa shirika la biashara duniani unaotarajia kufanyika mjini Hong Kong, lakini mazungumzo ya kilimo ya Doha bado hayajaondoa hali ya kukwama.
Ushuru na ruzuku ya mazao ya kilimo ni masuala makubwa yanayopaswa kutatuliwa kwenye mazungumzo ya kilimo ya shirika la biashara duniani katika kipindi cha hivi sasa. Mwanzoni mwa mwezi uliopita, mjumbe wa biashara wa Marekani Bw. Rob Portman alitangulia kupendekeza kuwa, Marekani itapunguza ruzuku ya kilimo kwa asilimia 60 katika miaka mitano ijayo, na mjumbe wa biashara wa Umoja wa Ulaya Bw. Peter Mandelson alisema kuwa, Umoja wa Ulaya uliweza kukubali kupunguza ruzuku ya kilimo kwa asilimia 70, na kupunguza ushuru wa mazao ya kilimo zitakazoagizwa kutoka nje kwa asilimia 20 hadi 50%.
Lakini Pendekezo hilo la Umoja wa Ulaya lilipingwa na nchi nyingi wanachama. Kutokana na shinikizo kutoka pande mbalimbali, tarehe 28 Oktoba, Bw. Mandelson alitoa "bei ya mwisho" ya Umoja wa Ulaya, yaani kupunguza ushuru wa mazao ya kilimo ya aina mbalimbali kwa asilimia 35 hadi asilimia 60. Marekani imeeleza kutoridhishwa kwake kwa pendekezo hilo jipya, ikiongeza kuwa, pendekezo la Umoja wa Ulaya la kupunguza aina za mazao ya kilimo zinazolindwa kwa asilimia 8 au 10 halitoshi. Hivi sasa Umoja wa Ulaya una aina 2000 za bidhaa za mazao ya kilimo zinazolindwa forodhani.
Kundi la Cains lililoundwa na nchi 17 zinazosafirisha bidhaa za kilimo kwa wingi pia limelalamikia pendekezo jipya la Umoja wa Ulaya. Kundi hilo lilitoa taarifa ikisema kuwa, "bei mpya" ya Umoja wa Ulaya haiwezi kuboresha hali ilivyo ya sasa iliyopotoshwa ya biashara ya mazao ya kilimo duniani.
Nchi nyingi zinazoendelea zinaona kuwa, japokuwa pendekezo jipya la Umoja wa Ulaya limepiga hatua, lakini bado haliwezi kutosheleza matakwa ya nchi zinazoendelea ya kuzitaka nchi zilizoendelea za Amerika na Ulaya zipunguze ushuru wa kuagiza mazao ya kilimo kwa asilimia 54 kwa wastani. Nchi kadhaa zinazozalisha pamba kwa wingi za Afrika zimeeleza malalamiko makali kwa hali ya maendeleo ya mazungumzo ya kilimo zikiona kuwa, suala la kupunguza ruzuku ya pamba kwa nchi zilizoendelea halikufuatiliwa ipasavyo, zimetishia kuwa, ikiwa suala la pamba haliwezi kutatuliwa, zitakataa kulegeza masharti yao katika mijadala mingine ya mazungumzo hayo.
Ufaransa inaona kuwa, pendekezo jipya la Mandelson tayari limepindukia kiasi alichopewa, na Japan, Uswisi, Korea ya Kusini na Norway zinaona kuwa, kupunguza kwa kiasi kikubwa cha ruzuku ya kilimo na ushuru wa kuagiza mazao ya kilimo kutaathiri umuhimu wa kilimo katika maeneo ya jamii na hifadhi ya maumbile.
Kutokana na mpango uliowekwa, nchi wanachama 148 wa shirika la biashara duniani zinapaswa kufikia makubaliano ya mwanzo ya mazungumzo ya biashara ya duru la Doha kwenye mkutano wa mawaziri unaotarajia kufanyika mwezi Desemba huko Hong Kong, ama sivyo mazungumzo hayo hayawezi kumalizika kabla ya mwishoni mwa mwaka 2006, na kufanikiwa au la kwa mazungumzo ya kilimo kutaathiri matokeo ya mkutano wa Hong Kong.
Ofisa wa shirika la biashara duniani anayeshughulikia mazungumzo hayo Bw. Crawford Falconer alisema kuwa, tarehe 7 Novemba shirika hilo litafanya majadiliano kwa mara nyingine tena ya ngazi ya mawaziri huko London ili kupata maendeleo halisi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-11-02
|