Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-02 20:27:33    
Chanjo,silaha kali katika kinga na udhibiti wa magonjwa ya maambukizi

cri

Kutumia chanjo kwa kinga na udhibiti wa magonjwa ya maambukizi kwa kutumia chanjo ni mafanikio makubwa waliyoyapata binadamu katika mapambano dhidi ya magonjwa ya maambukizi. Kwa mujibu wa ripoti moja iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani, zaidi ya watoto milioni 2 wanaokufa kutokana na magonjwa ya maambukizi kila mwaka, lakini watoto hao wangeweza kuokolewa kutokana na kupewa chanjo.

Chanjo ni nini? Mtaalamu wa kituo cha kinga na udhibiti wa magonjwa ya mambukizi cha Beijing Bw. Wujiang akifamamisha alisema:

"Kwa maneno ya kawaida, chanjo ni dawa inayotengenezwa kwa kutumia vijidudu au virusi vinavyosababisha magonjwa ya maambukizi, na virusi hivyo vikiingia kwenye mwili wa binadamu, mwili huo utatoa kitu fulani ambacho kinaweza kuzuia virusi hivyo visiingie tena mwilini. Ingawa chanjo ni vijidudu au virusi vinavyotengenezwa, lakini tofauti kubwa kati ya chanjo na virusi au vijidudu ni kuwa chanjo haisababishi magonjwa, bali inaweza kulinda afya ya binadamu."

Mwaka 1976, madaktari wa Uingereza waligundua kuwa baada ya kupewa chanjo ya ndui, watu walikuwa na uwezo wa kujikinga na ugonjwa wa ndui, na chanjo ya ugonjwa wa ndui ilikuwa chanjo ya kwanza duniani. Mwaka 1980, Shirika la Afya Duniani lilitangaza kuwa ugonjwa wa ndui umetokomezwa kabisa, na ugonjwa huo ulikuwa ugonjwa wa kwanza kutokomezwa na binadamu kwa kutumia chanjo. Hivi sasa, wanasayansi wamefanikiwa kutengeneza chanjo dhidi ya magonjwa yaliyoathiri afya ya binadamu katika nusu karne iliyopita, zikiwemo chanjo ya ndui, kipindupindu, tauni, kifua kikuu, dondakoo, pepo punda, polio na surua.

Kutokana na umuhimu wa chanjo katika kinga na udhibiti wa magonjwa ya maambukizi, nchi mbalimbali duniani zinatilia maanani sana kazi ya kutoa chanjo. Ingawa China haikuanza kufanya kazi hiyo mapema kama zilivyokuwa nchi za magharibi, lakini kadiri uchumi na jamii inavyoendelea, ndivyo kazi hiyo ya China inavyoendelea vizuri, na hatua muhimu zaidi ya China ni kutoa chanjo kwa watoto kwa mpango.

Hatua hiyo inatekelezwa kama ifuatayo: watoto chini ya umri wa miaka 7 wanapewa chanjo 5 ikiwemo chanjo moja ya mseto dhidi ya magonjwa ya aina 3, chanjo hizo 5 zitawapatia watoto uwezo kwa kujikinga na magonjwa 7, yakiwemo magonjwa ya polio, surua na kifua kikuu. Gharama za chanjo hizo zinalipwa na serikali, wazazi wa watoto wanatakiwa kulipa gharama kidogo ya huduma. Tangu miaka ya 70 ya karne iliyopita, kazi hiyo imeenezwa kote nchini China, na imepata mafanikio makubwa, kiwango cha watoto wa China cha kupewa chanjo kimeinuka kidhahiri. Mtaalamu maarufu anayeshughulikia magonjwa ya watoto Bi. Hu Yamei alisema:

"Mwaka 2003 wakati ugonjwa wa SARS ulipoibuka nchini China, hakuna mtoto hata mmoja aliyekufa kutokana na ugonjwa huo, hali hiyo iantokana na kazi yetu ya kuwapatia watoto chanjo, kwa kuwa chanjo walizopewa watoto dhidi ya magonjwa ya polio, surua na magonjwa mengine huenda zimefanya kazi mwilini mwa watoto na kuwapatia uwezo kiasi fulani wa kujikinga na ugonjwa wa SARS, hivyo wakati huo ni watoto wachache tu walioambikizwa ugonjwa wa SARS, na hakuna mtoto hata mmoja aliyekufa kutokana na ugonjwa huo."

Imefahamika kuwa katika miaka 15 iliyopita, China imetimiza lengo la kutoa chanjo kwa asilimia 85 ya watoto, na kupitishwa kwenye ukaguzi uliofanywa na Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya Duniani na Wizara ya Afya ya China. Kadiri kazi hiyo ya kuwapatia watu chanjo kwa mpango inavyoendelea, ndivyo magonjwa ya surua, kifua kikuu, dondakoo, na pepo punda yanavyokaribia kutokomezwa. kwa mfano, katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, watu 2000 kati ya laki moja wanaoambukizwa ugonjwa wa surua, lakini hivi sasa, takwimu hizo imepungua kuwa watu 10 tu kati laki moja wanaoambukizwa ugonjwa huo; aidha, katika mwaka 2000, China imetimiza lengo la kutokomeza kabisa ugonjwa wa polio nchini baada ya kutokomeza ugonjwa wa ndui mwaka 1960.

Mbali na chanjo 5 zinazowekwa kwenye mpango, wazazi wa China wanaweza kuwapeleka watoto wao hospitalini kupewa chanjo nyingine, kama vile chanjo dhidi ya mafua. Aidha, wachina wengi wanaweza kuchagua chanjo kutokana na hali yao ya afya na hali ya hewa, kwa mfano katika majira ya baridi na Spring, ambapo ni rahisi kwa watu kuambukizwa virusi vya mafua, hospitali hujaa watu wanaotaka kupewa chanjo ya mafua; na kama mtu akiumwa na mbwa, anapaswa kupewa chanjo ya kichaa cha mbwa.

Ili kulinda vizuri afya ya binadamu, hivi sasa, wanasayansi na wataalam wa tiba wa China wanafanya utafiti kuhusu chanjo mpya. Mtaalam wa Taasisi ya Kinga ya Magonjwa ya China Bw. He Xiong alifahamisha alisema:

"Hivi sasa, tunafanya utafiti juu ya chanjo ambazo hatujafanikiwa kuzitengeneza, kama vile, chanjo ya ugonjwa wa ukimwi, na tumegundua kuwa baadhi ya magonjwa yanayoathiri polepole na chembechembe za ugonjwa wa saratani pia yanasababishwa na virusi au vijidudu, hivyo tunafanya chini juu ili kufanikiwa kutengeneza chanjo dhidi ya magonjwa kama hayo, kwa mfano, hivi sasa tunafanya utafiti juu ya chanjo dhidi ya saratani ya tumbo na saratani ya tumbo la uzazi.

Idhaa ya Kiswahili 2005-11-02