Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-04 17:35:13    
Kikundi cha matibabu cha ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo

cri
Kikundi cha matibabu cha China nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kilichoko karibuni na uwanja wa ndege huko Kindu, mji wa mashariki wa nchi hiyo, kimeweka rekodi nyingi mpya katika historia ya kikundi cha ulinzi wa amani cha China, yaani China kwa mara ya kwanza kupeleka wanajeshi wanawake katika nchi ya nje, kwa mara ya kwanza kutoa huduma ya matibabu katika kazi ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa, na kwa mara ya kwanza kushiriki kwenye kazi hiyo katika bara lisilo la Asia.

Hadi kufikia mwaka huu, China imepeleka vikundi vinne vya matibabu vya ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo tangu mwezi Aprili, mwaka 2003. Hivi sasa wanajeshi wanawake 10 wanaotoka kwenye hospitali nne za kijeshi mkoani Liaoning, China wanatekeleza majukumu ya ulinzi wa amani nchini humo. Wanajeshi hao wameonesha sura nzuri ya wanajeshi wanawake wa China kutokana na vitendo vyao.

Bibi Leng Hui ni mwuguzi wa kikundi hicho cha matibabu. Tarehe 17, Aprili, mwaka huu, ilikuwa siku yake ya kufunga ndoa. Harusi yake ilichanganya furaha na masikitiko, kwani alikuwa amepokea amri ya kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutekeleza kazi ya ulinzi wa amani. "Usiwe na wasiwasi, nitarudi salama." Leng Hui alimwambia mume wake usiku alipofunga ndoa. Siku ya pili, alivaa sare za kijeshi na kuagana na mume wake. Bibi Leng Hui alisema, "Hilo ni somo la kwanza katika maisha yetu mapya, vilevile ni thibitisho la upendo wetu."

Siku ya wafanyakazi duniani iliwadia siku kadhaa baada ya kikundi cha matibabu cha China kufikia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Usiku ule, watu wengine walikuwa wakisherehekea katika tamasha la siku hiyo, mwuguzi Han Shuang alimkumbuka mchumba wake aliyeko China akiwa anaangalia mwezi angani.

Han Shuang na mchumba wake walikuwa wamejiandaa kufunga ndoa siku hiyo, lakini alipokea amri ya kushiriki kwenye shughuli za kulinda amani. Alipojadiliana na mchumba wake kuhusu kuahirisha harusi yao, mchumba wake alishangaa. Lakini mchumba wake ambaye vilevile ni mwanajeshi alikubali uchaguzi wa Han Shuang, na kumwambia: "Nauweka upendo wangu kwenye mwezi angani, ukiona mwezi barani Afrika ni kama kuniona."

Kwenye kikundi cha matibabu cha China, wanajeshi wanawake watano wana watoto. Kati ya watoto hao, mkubwa zaidi anasoma katika shule ya sekondari, mdogo zaidi bado ni mtoto mchanga. Wakiwa wanawake, wanapaswa kubeba majukumu ya mama na wake; wakiwa wanajeshi wa ulinzi wa amani, wanapaswa kutekeleza jukumu la wanajeshi, na walionesha moyo wa dhati kwa watoto wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Tarehe 1, Juni ilikuwa Siku ya watoto duniani. Wanajeshi watano akiwemo mkuu wa wauguzi Zhao Xiaohong walizawadia watoto wanaosoma kwenye shule za msingi za huko vifaa vya masomo, vitu vya kuchezea, kama vile penseli, vitabu vya ziada, vifutio, na mipira ya kikapu na ya wavu. Mkuu wa Idara ya elimu ya mkoa alisifu sana shughuli hiyo. Ujumbe maalum wa Umoja wa Mataifa vilevile ulitoa makala nyingi kuhusu tukio hilo katika magazeti na tovuti mbalimbali kwenye mtandao wa Internet.

Ingawa mazingira ya kazi ya Kikundi cha matibabu cha China si mazuri: maeneo ya hospitali ya ulinzi wa amani ya China ni mita za mraba elfu 10, sawa na uwanja wa mpira wa soka. Seng'enge inauzunguka. Wanajeshi hao hawana fursa nyingi za kwenda nje, lakini walifanya juhudi kubwa kuondoa matatizo mbalimbali na kuyazoea maisha ya huko.

Tangu China ipeleke kikundi cha kwanza cha wanajeshi wanawake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mwezi Aprili, mwaka 2003, mpaka sasa jumla ya wanajeshi wanawake makumi wametekeleza kazi ya ulinzi wa amani nchini humo. Wanajeshi hao walichaguliwa kati ya madaktari na wauguzi waliojiandikisha kwa hiari nchini China, na wamefanya mazoezi mbalimbali kabla ya kufanya kazi katika nchi za nje. Mazoezi hayo ni pamoja na uokoaji wa dharura, ulinzi maalum, huduma za matibabu, upashanaji wa habari, jiografia ya kijeshi, uongozi, matumizi ya silaha nyepesi na uendeshaji wa magari, aidha walipata mafunzo ya lugha ya kiingereza.

Aidha, wanapaswa kufanya mazoezi ya uwezo mwilini. Kiwango chao ni kukimbia mita 3000 ndani ya dakika 18. Ingawa mwanzoni hakukuwa na mtu aliyeweza kumaliza safari yote, lakini walitiana moyo na kusaidiana, na kushinda matatizo yote. Askari wote waliweza kumaliza safari ya mita 3000 ndani ya dakika 17.

Wakiwa wanajeshi wa kikundi cha matibabu, walitafuta habari nyingi kuhusu magonjwa mbalimbali nchini humo na kufanya maandalizi ya kutosha ya kukabiliana na magonjwa hayo.

Ingawa wanabeba jukumu kubwa walilopewa na taifa na matatizo mbalimbali ya maisha, wanajeshi hao wanaona kuwa, utekelezaji wa kazi ya ulinzi wa amani ni sehemu yao muhimu sana katika maisha yao, pia ni fahari kubwa kwao kuliwakilisha taifa kushiriki kwenye kazi hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-11-04